MADAI YA MADAKTARI
Baada ya majadiliano ya kina, na vikao vingi kufanyika, jumuiya ya madaktari ikakubaliana katika hoja za msingi ambazo zinahitaji nguvu ya ziada ili kushinikiza mabadiliko ya msingi katika sekta hiyo nyeti kwa ustawi wa Taifa letu na kufikikia maazimio yafuatayo:
Uboreshaji wa maslahi ya madaktari na watumishi wengine wa afya
Kimsingi madaktari na watumishi wa afya kwa ujumla, kwa kipindi kirefu sasa wamekuwa wakiishi katika hali duni ya maisha kutokana na mishahara isiyokidhi viwango na kukosekana kwa stahili zingine kama vile nyumba, bima ya afya inayokidhi, risk allowance (Posho ya mazingira hatarishi), Posho ya zamu (Call Allowances). Vyote hivi ni vikwazo katika utoaji wa huduma bora za afya kwa watanzania.
Maazimio
A. Posho [Allowances]
1. Posho ya kulala kazini [On-Call Allowance]
Toka mwaka 2004, serikali imekuwa ikiwalipa madaktari posho ya shilingi 10,000 mpaka hii leo bila kujali mabadiliko ya hali ya ugumu wa maisha ambayo yametokea toka mwaka huo na hilo linalidhihirishwa na vigezo mbalimbali ikiwemo mfumuko wa bei, kwa sasa mfumuko wa bei ni zaidi ya asilimia 18, mwaka 2004, mfumuko wa bei ulikuwa takribani asilimia 3 ikimaanisha kuwa hali imekuwa mbaya mara sita zaidi. Standing order ya serikali inaelekeza wazi kuwa Posho ya kulala kazini ilipwe kwa utaratibu wa half per diem ya mkoa husika. Hili limepuuzwa na watendaji wa serikali na halikuwahi kutekelezeka.
Azimio - Madaktari walipwe posho hii kwa kiwango cha asilimia kumi ya mshahara na utaratibu huu utolewe kwa maandishi na uanze kutumika mara moja.
2. Posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi [Risk Allowance]
Madaktari wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira ambayo yanawapelekea kuwa katika hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali kama vile homa ya ini-hepatitis B virus( ambao hupelekea kansa ya ini), Ukimwi kutokana na virus vya HIV, kifua kikuu na mengineyo. Katika hili hakuna utaratibu wowote unaomuwezesha Daktari kujikimu na kujilinda kama vile posho na chanjo kwa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.
Azimio - Madaktari kupewa posho ya asilimia 30 ya mshahara, utaratibu wa posho hii uwe wa maandishi na uanze kutumika mara moja.
3. Nyumba
Standing order ya serikali inalelekeza wazi utaratibu wa kutoa nyumba kwa madaktari ambao kimsingi ni maofisa.
Azimio - Madaktari wapewe nyumba kama inavyoelekezwa kwenye mwongozo na pale inaposhindikana posho ya nyumba (Housing allowance ilipwe kwa asilimia 30 ya mshahara kama inavyoelekezwa). Utaratibu wa kulipa posho hii uanze kutumika mara moja.
4. Posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu [Hardship Allowance]
Ni ukweli usiofichika kuwa madaktari wamekuwa wakipangiwa kufanya kazi katika maeneo magumu kufikika na mazingira yake ya kazi pia ni magumu. Hii imepelekea wengi wao kutofika maeneo husika na hivyo kuzorotesha huduma za afya katika maeneo hayo.
Azimio - Tunaitaka serikali iwalipe madaktari wanaofanya kazi katika mazingira tajwa, walipwe posho ya asimilia 40. Utaratibu huu uanze kutumika mara moja na uwe kwa maandishi.
5. Usafiri- kwenda na kurudi maeneo ya kazi
Azimio – Posho ya kiwango cha asilimia 10 ya mshahara ilipwe kwa Madaktari. Kinyume cha hapo madaktari wakopeshwe magari. Utaratibu wowote kati ya huu uanze kutumika mara moja na uwe katika maandishi.
B. Mshahara.
Mshahara wa sh laki 7 kwa daktari anayeanza kazi ni mdogo sana kukabiliana na hali halisi ya maisha. Kulingana na ripoti ya utafiti wa tathmini ya uzito wa kazi kwa watumishi wa umma iliyotolewa mwaka 1998 (Civil Service Benchmark Job Evaluation Study), uzito wa kazi wa madaktari ulionekana kuwa na kiwango kimoja na senior managers katika utumishi wa umma. Viwango vya malipo vya senior managers viliboreshwa na vipo juu sana wakati madaktari wakibaki na hali mbaya.
Azimio - Madaktari wanapendekeza ongezeko la mshahara unaofikia 3,500,000 kuanza kulipwa ili kukabiliana na ugumu wa maisha uliopo sasa.
C. Bima ya Afya [medical insurance]
Madaktari wapatiwe green card kama namna ya kuwawezesha kupata tiba iliyo bora mara watakapougua wao na familia zao. Utaratibu huu uwekwe kwa maandishi na uanze kutumika mara moja.
Watendaji wakuu wa wizara ya Afya
Azimio - Watendaji wakuu wa Wizara ya Afya wamedhihirisha uwezo mdogo wa kiutendaji na kiungozi na kushindwa kuwajibika ipasavyo na hivyo kupelekea kuharibika kwa utaratibu wa kawaida wa kutoa huduma, kuwaumiza wananchi na kuharibu sura ya serikali kwa wananchi wake. Kinara wa haya yote ni mtendaji mkuu wa Wizara hii, Katibu Mkuu-Blandina Nyoni. Huyu tunapendekeza awajibishwe mara moja kwani kuna ushahidi wa unyanyasaji mkubwa ambao ameshaufanya kwa wataalamu mbalimbali wa afya kutoka vitengo mbalimbali, kwa kuendelea kuwepo kwake, itaweza kusababisha madaktari kupoteza imani tuliyonayo kwa serikali. Wendine ni Waziri wa Afya (Haji Mponda), Naibu Waziri wa Afya (Lucy Nkya) na Mganga Mkuu wa serikali (Dr. Deo Mtasiwa) ambao kwa wakati mbalimbali wametoa kauli za kashfa na dharau kwa madaktari. Jumuiya ya madaktari ikiwa kama mdau mkubwa wa sekta ya afya, tumeazimia kukutaarifu umshauri Mh Rais awawajibishe wateule wake ambao wameshindwa kumsaidia katika utendaji wa sekta nyeti ya wizara ya afya.
Madaktari waliofukuzwa kazini.
Azimio - Madaktari wote waliokuwa katika mafunzo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na baadae kurudishwa wizarani, warejeshwe Muhimbili bila masharti yoyote na walipwe haki zao za msingi mara moja. Utaratibu huu ni vizuri ukawekwa kwa maandishi.
Huduma Duni wanazopata wananchi.
Uboreshaji wa huduma za afya; Wakati viongozi wakikimbizana kwenda nchini India kwa matibabu,kumekuwa na hali ya kuzorota kwa huduma za afya katika kiwango ambacho hakivumiliki tena, na hali hii kwa kiwango kikubwa inasababishwa na ukosefu wa vifaa tiba, madawa na wataalamu wa afya katika hospitali zetu, mfano ni katika hospitali za manispaa ya Temeke, Mwananyamala na Amana ambapo wagonjwa wanalazimika kujinunulia vifaa tiba na dawa kwa gharama kubwa licha ya wagonjwa kuchangia katika mfuko wa matibabu ya kijamii.
Wakati huo huo, ni kitendo cha aibu na fedheha katika karne hii kwa wagonjwa kulala chini hasa katika hospitali ya rufaa kama Muhimbili na kwingineko. Hali hii licha ya kuwa kero kwa wagonjwa na ndugu zao lakini pia inajenga mazingira magumu kwa watumishi wa afya.
Mungu ibariki Afrika!
Mungu ibariki Tanzania!


RSS Feed