Picture
Bendi ya THT, kutoka (kulia) ni Marlow, Amin na Linah, wakitoa burudani jukwaani wakati wa hafla ya kutangaza matokeo ya Sensa 2012
Rais alisema sensa italigharimu Taifa Sh bilioni 140 ambapo kwa sasa tayari Sh bilioni 124 zimetumika. "Sensa inafanywa na kila Taifa duniani kote na ni gharama kubwa kuhesabu watu."

Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Sensa ambaye pia ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema sensa hiyo imegharimiwa kwa pamoja kati ya Serikali na washirika wa maendeleo. Alisema mchango wa Serikali katika kugharimia sensa umekuwa ukiongezeka kutoka sensa moja hadi nyingine.

Alisema sensa ya mwaka huu, Serikali imechangia asilimia 90 ya gharama zote kutoka asilimia 70 kwa sensa ya mwaka 2002. Alisema sensa hiyo pia kwa kiasi kikubwa imeendeshwa na wataalamu wa ndani  kuliko ilivyokuwa kwa sensa iliyopita.

"Hii inaonesha kukua kwa wataalamu wa ndani katika uendeshaji wa sensa na utafiti mwingine hapa nchini," alisema Pinda na kufafanua kuwa utekelezaji wa kuhesabu watu ulitoa ajira ya muda mfupi kwa wananchi hususan vijana ambao hawakuwa na ajira.

Alitaja idadi ya watu 150 kuwa walipata ajira ya kutenga maeneo  ya kuhesabia watu ambapo makarani na wasimamizi wa sensa walikuwa 200,000 wakati wachambuzi wa takwimu walikuwa 400 walioajiriwa kwa vipindi tofauti wakati wa kutekeleza sensa. Wazabuni wa ndani wapatao 29 walitoa huduma na vifaa mbalimbali kwa ajili ya la sensa kwa Sh bilioni 11.7.

Changamoto kadhaa zilizojitokeza zilitajwa na Pinda kuwa ni pamoja na watu wanne kupoteza maisha walipokuwa wakiwajibika na kazi hiyo na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Rais Kikwete alitaja pia changamoto zingine kuwa ni watendaji wa sensa kukumbana na purukushani kutokana na kundi la watu waliotishia  kuvuruga sensa na wengine kufanya kampeni ya kushawishi watu wasusie kuhesabiwa.

"Wengine katika kipindi hiki ndicho walipanga kufanya maandamano na mikutano, lakini pamoja na changamoto zote hizi, tumefanikiwa," alisema Rais Kikwete.
Picture
Sehemu ya umati uliohudhuria hafla hiyo
 


Comments


Your comment will be posted after it is approved.


Leave a Reply