Askofu Anthony Mayala afariki dunia

Habari hii ya kusikitisha imeripotiwa katika gazeti tando la Majira na Daud Magesa kutoka Mwanza. Blogu hii inatoa pole kwa WaTanzania wote hasa wale walioguswa na msiba huu kwa namna yoyote ile.

ASKOFU wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki Mwanza Mhashamu Anthony Mayala (pichani) amefariki dunia. Askofu Mayala alifariki dunia jana saa nane mchana katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) iliyopo Jijini hapa kwa ugonjwa wa shinikizo la damu.
Habari zilizopatikana kutoka makao makuu ya jimbo hilo yaliyopo Kawekamo, zilisema Askofu Mayala aligua ghafla juzi na kupelekwa hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu.
Askofu Mayala aliteuliwa kuwa askofu wa jimbo la Mwanza baada ya mtangulizi wake, aliyekuwa Askofu marehemu Renatus Butibubage, kuhamishiwa jimbo la
Geita.

Kifo cha askofu huyo kimepokelewa kwa majonzi makubwa na wakazi wa Mwanza hususan waumini wa kanisa Katoliki ambao Jumatatu ya wiki hii walimwona akiwa mzima
akiendelea na huduma za kiroho.Wiki iliyopita alimsimika na kumpa Bw. Paul Nzungu, daraja la Upadrisho.

Katika uhai wake alisaidia kuleta maendeleo ya jamii ikiwemo elimu na kushiriki kikamilifu kuanzisha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Bugando (BUCHS).Mkurugenzi wa Hospitali ya Bugando Dkt. Charles Majinge, alipotafutwa kuzungumzia kifo hicho hakupatikana kwani simu yake ilikuwa haiko hewani.