Benki Kuu Tanzania yachapisha noti mpya ya shilingi 2,000

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa noti mpya za Sh2,000 ambazo zitatumika sanjari na zilizopo kwenye mzunguko kwa sasa.

Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu alisema jana kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba, lengo la kutoa noti hizo mpya ni kukidhi mahitaji yake kwenye mzunguko wa fedha nchini.

"Noti hizi mpya zinatofauti moja tu na zile ambazo zimo kwenye mzunguko kwa sasa nayo ni saini zilizopo.

Saini zilizopo kwenye noti mpya ni za Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo na Gavana wa Benki kuu ya Tanzania,” alisema.

Profesa Ndulu alisema kuwa noti hizo bado zina rangi ya kahawia, zikiwa na michoro inayoonyesha mandhari ya kitanzania kiuchumi, kiutamaduni pamoja na urithi wetu na mazingira.

"Mbele ya noti, bado kuna picha inayoonyesha utajiri wetu wa kuwa na mojawapo ya wanyama pori wakubwa yaani simba ,alama ya kificho ya twiga ambayo bado ipo kama ilivyo katika noti nyingine zinazozunguka sasa" lilifafanua tangazo hilo.

Alama nyingine zilizopo katika noti hiyo ambazo hazina tofauti na iliyopo kwenye mzunguko ni nyuma ya noti kuna picha inayoonyesha picha ya ngome kongwe illiyopo Forodhani jijini Zanzibar.

Vile vile, alisema zina picha ya kinyago cha kuchonga na alama ya usalama inayobadilika rangi ikigeuzwa.

”Benki kuu inawashauri wananchi kuwa hakuna haja ya kubadili noti hizo kwani thamani yake ni ileile na kwamba haina mpango wa kuzifuta zilizokuwepo katika mzunguko wa awali.

Habari imeandikwa na Burhani Yakub wa gazeti la Mwananchi.