Hasheem Thabeet Manka : Sijachukua uraia wa Marekani

Habari hii nimeipata toka kwenye blogu ya Mpoki Bukuku aka Mzee wa Sumo
“SINA 'girl friend' kwa sasa kwa kuwa ninao wengi tu sijaamua kutulia na mmoja,” 
anasema Hasheen Thabit Manka, mchezaji wa mpira wa kikapu, Mtanzania ambaye amepata nafasi ya kucheza Ligi ya Juu ya Marekani ya NBA akiwa na klabu ya Memphis Grizzlies.

Hasheem Thabeet, ni kijana mcheshi mwenye kupenda kuzungumza, lakini kwa sasa maisha yake yamebadilika kabisa baada ya kuishi Marekani kwa zaidi ya miaka mitatu akitafuta nafasi ya kujiendeleza kimaisha kupitia michezo. Watu wengi wanaomfahamu hususani walioishi naye jirani katika mitaa ya Sinza jijini Dar es Salaam wanamjua kuwa alikuwa kijana wa kijiweni ambaye alikuwa akishinda na wenzake wakipiga stori, lakini sasa amebadilika na kuwa mtu wa aina nyingine, si yule wa Sinza, si yule aliyekuwa anapanda daladala, amekuwa mtu mwingine, mtu wa hali ya juu.
“Jamaa ana nyodo kichizi tangu amekwenda Marekani anajifanya anapita anapunga mkono kwa mbali lakini powa tu,”
anasema mmoja wa rafiki zake ambao walikuwa wakiishi naye jirani na kupiga soga katika kijiwe kimoja Sinza. Lakini Hasheem hashangazwi na hali hiyo kwani alipozungumza na Mwanaspoti wiki hii jijini Dar es Salaam anasema watu wanashindwa kuelewa maisha yake kwa sasa. Ni kweli alikuwa kijiweni na alikuwa ana washikaji wengi waliokuwa wakishinda pamoja, lakini kwa sasa utaratibu wa maisha yake umebadilika.
“Kuna watu wanalaumu uvaaji wangu na wengine jinsi ninavyozungumza, lakini sasa nimekuwa mtu mwingine, siwezi tena kukaa kijiweni kwa zaidi ya saa sita na kupiga stori,” 
anaeleza Hasheem ambaye ana meneja anayemsaidia kuendesha maisha yake. Hasheem Thabeet (kama jina lake linavyoandikwa Marekani), anasema ameelekezwa mambo mengi ya kufanya ili afanikiwe katika kazi hiyo mpya ambayo itamwingizia kipato na anafuata mwongozo huo kwani bado haamini kama alipofikia ni mwisho:
“Nimefanya bidii kubwa sana kufika hapa ni lazima nifuate maelekezo ninayopewa”.
Anasema ili kufika alipo, haikuwa kazi rahisi, kwani ilikuwa ni kama bahati na bidii iliyotokana na kujituma.
“Nilikuwa naumia sana, najitahidi na kuna wakati nilikuwa nakata tamaa kabisa na kutaka kuachana na huu mchezo.”
Hata hivyo anasema mama yake alimsaidia sana na kumpa moyo na marafiki zake waliokuwa Marekani:
“Nilikuwa nawasiliana na mama yangu kila mara na kumweleza kila hatua, ilifika kipindi nilitaka kukata tamaa lakini alinisihi nijitahidi, namshukuru sana.”
Hasheem mwenye urefu wa futi 7.3 anasema mchezo huo kwa Marekani ni kitu kinachopewa umuhimu wa aina yake na kunakuwa na mfumo maalum wa kumjenga mtu ili kuwa mchezaji bora, tofauti na hapa ambapo kila mchezaji anajiendeleza kwa juhudi binafsi.
“Sidhani kama hapa nyumbani mchezo huu unaweza kufika mbali kwa kuwa viongozi wenye dhamana ya mchezo wizarani na hata katika chama cha mpira hawako makini kuendeleza mchezo huu.”
Anasema viongozi wengi wamekuwa wakijali zaidi maslahi yao binafsi na kusahau kuboresha mchezo huo pamoja na miundombinu yake kitu kinachofanya wachezaje washindwe kuendelea zaidi kutokana na uduni huo.
“Mimi nimeshangaa kwa muda wote nilipokuwa sipo viwanja nilivyojifunzia na kufanya mazoezi, viko kati hali ile ile sasa hapo utamlaumu nani? Ni viongozi wenyewe.”
Anasema kama watu hawatabadilika, itakuwa vigumu sana kwa wachezaji wa Tanzania kuendelea katika mchezo huo, kwani yeye anaona mafanikio yake ni kwa ajili ya juhudi zake kubwa.
 “Labda mmoja katika milioni anaweza kupata nafasi kwa mtindo huu.”
Lakini bado anasema kuna mchango wake ambao atajitahidi kuutoa ili kusaidia mchezo huo; “Najua sitakuwa sana hapa nchini, nitatumia muda wangu mwingi Marekani lakini nikipata nafasi nitakuwa nakuja na kuandaa kliniki mbalimbali za mchezo huo ili kuwasaidia vijana. Hasheem anasema alipokuwa hapa, hakuna kiongozi aliyemsaidia na kwenda Marekanii ilikuwa ni juhudi zake na baadhi ya watu ambao walimwona angefaa kwa ajili ya kucheza mchezo huo.
“Mimi nashangaa watu wamekuwa wakitumia mgongo wangu kujirusha, wengi wakijifanya ndio wamenifikisha nilipo, hii si kweli kabisa ni juhudi binafsi. Na kila mtu anajifanya ananijua sana sasa, lakini si kweli.”
Thabeet, ambaye ni mtoto wa Thabit Manka na Rukia Manka. Baba yake amefariki na mama yake Rukia yupo hai na amekuwa msaada kwake siku zote na ana wadogo zake wawili; Ahkbar ambaye kwa sasa anaishi naye Marekani na Sham ambaye ni wa kike. Anasema hata baada ya kuchaguliwa kuingia katika ligi hiyo baadhi ya watu hususani viongozi wamekuwa wakimfuata hadi Marekani na kudai kuwa wametumwa na viongozi wa nchi kumpongeza na kumuahidi ushirikiano. Kwa miaka miwili iliyopita, Hasheem alikuwa nyota katika timu ya mpira wa kikapu katika Chuo maarufu cha Uconn katika jiji la New York, Marekani na kimekuwa na sifa ya kuibua nyota wengi wanaocheza katika ligi maarufu ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA) ambako sasa ndio Mtanzania huyo ameingizwa.
Hata hivyo anamsifu Rais Jakaya Kikwete ambaye ni mpenzi wa mchezo huo kwa jinsi alivyokuwa akimpa moyo na kumfuatilia kwa hatua mbalimbali;
"Ana upendo sana na amekuwa akiwasiliana na mimi mara kwa mara na tumekuwa tukionana mara kwa mara anapokuja Marekani.”
Lakini, tofauti na hisia za watu wengi hapa nchini wanaofikiri kuwa kwa kuingia katika ligi hiyo, Hasheem anaweza kusaliti na kubadili uraia wake ili awe Mmarekani, yeye anasema;
"No nitatumia muda wangu mwingi sana Marekani hiyo iko wazi lakini kila mara ninapofikiria naona nimefikia hapo nilipo nikiwa Mtanzania, nitakuwa Mtanzania na ninajivunia kuwa Mtanzania na kuzaliwa katika nchi hii.”
Kwa upande wa Wamarekani wenyewe wameshtushwa na ubora wa Hasheem katika mchezo huo ambao ni maarufu sana nchini mwao, kwani mwaka 2005 wakati anakwenda huko hakuna aliyemtarajia kuwa angekuwa mchezaji mzuri hata kuchezea Ligi ya NBA. Alielezwa katika gazeti maarufu la Marekani New York Times kama mchezaji tegemeo katika timu ya chuo aliyokuwa akichezea kwani ni vigumu kupitwa na wachezaji wengine anapokuwa uwanjani.
"Tunapocheza katika timu ingawa tuko watano lakini tunaona kama kuna wachezaji sita kwa sababu ya Hasheem,” 
anasema Jeff Adrien ambaye walicheza naye katika ligi ya vyuo. Lakini Hasheem hakuwa mchezaji wa kikapu tangu alivyoanza, bali alikuwa mchezaji wa mpira wa miguu na kitu hicho kilimsababishia mwanzo mgumu kuingia katika kikapu. Wamarekani walimwona kuwa angefaa na hata alipoanza alikuwa kama kituko kwani mara nyingine alikuwa akipiga mpira kwa miguu na kusahau kutumia mikono , kitu kilichofanya makocha wake kufanya kazi ya ziada ambayo sasa imezaa matunda. Hapa nchini alianza kucheza kikapu alipokuwa Makongo na kwa mujibu wake ni kwamba hakupenda mchezo huo bali kuna siku alijaribu kucheza na rafiki yake aliyempatia viatu ili aanze kucheza na alipofika shule alichezea timu ya shule. Alishiriki mashindano ya Afrika Mashariki kwa shule za sekondari na huko ndiko maisha yake yalibadilika. Alipatiwa ufadhili wa kwenda Marekani na Mkenya mmoja ambaye aliona anaweza kunufaika.

Hasheem Thabeet alizungumza na Rais Jakaya Kikwete muda mfupi kabla ya kuweka historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kusajiliwa kwenye Ligi Kuu ya NBA. Thabeet, ambaye aliahirisha kucheza ligi hiyo mwaka jana na juzi baada ya kushauriwa na walimu wake kwenye Chuo Kikuu cha Connectict, mwaka huu alikuwa chaguo namba mbili kwenye usajili wa wachezaji chipukizi unaojulikana kama DRAFT (Data Related Analysis aliposajiliwa rasmi na klabu ya Memphis Grizzlies.

Kabla ya kwenda kushuhudia uteuzi huo Thabeet aliliambiajarida la mtandaoni la Men's Journal kuwa aliongea kwa ujumbe wa simu na rais wa Tanzania. Gazeti hilo limeandika katika toleo lake la Juni 25 kuwa mwanafunzi huyo wa zamani wa Shule ya Sekondari ya Makongo alifanya mahojiano nao mara baada ya kumaliza kumtumia ujumbe rais. Hasheem, ambaye ana urefu wa futi 7'3 alikuwa anahitajika sana kwenye klabu hiyo ya Grizzlies, ambayo wastani wake wa kushinda mechi kwa msimu ni michezo 16 kati ya 86 kwa msimu, ili aisaidie katika kiungo- akiwa na jukumu la kuzuia na kufunga.

Hasheem alizaliwa Februari 16, 1987 na sasa ana umri wa miaka 22 ambayo itamwezesha kucheza kwa muda mrefu katika ligi hiyo na kufanya awe na matumaini makubwa ya kuwa mchezaji maarufu si kwa Tanzania bali dunia nzima
Mungu ampe nini!