Kongamano la Mtandao wa Wasomi lasimamishwa huko Mbeya

Bado hii sijaielewa... ila najua iko namna! Lazima ipo tu. Haiwezekani wakataze bure bure tu, ipo namna ndani yake.
Waraka wa Kanisa Katoliki umezua jambo mkoani Mbeya baada ya Jeshi la Polisi mkoani hapa kupiga marufuku kufanyika kwa kongamano lililoandaliwa na Mtandao wa Wasomi na Wataalam la Mbeya Professionals Network mkoani hapa ambalo pamoja na mambo mengine washiriki wangepata fursa kuujadili kujua nini kilichoandikwa katika waraka huo ambao umezua malumbano makali hapa nchini.

Kongamano hilo ambalo mgeni rasmi alikuwa Mhashamu Askofu Mkuu wa Jimbo la Mbeya, Evarist Chengula, lilipigwa 'stop' katika dakika za mwisho wakati askofu akiwa njiani kwenda kufungua baada ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) kupiga simu na kuwaeleza wandaaji kuwa hawaruhusiwi kufanya kongamano hilo.

"Wakati nikiwa nyumbani kwangu kabla sijafika ukumbini, nilipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) kwamba anamuhitaji ofisini kwake nilipokwenda akanieleza kuwa ameagizwa na wakubwa zake kongamano hilo lisifanyike," alisema Mwenyekiti wa Mtandao huo, Prince Mwaihojo.

Mwaihojo alisema kuwa mgeni rasmi alikuwa njiani kuelekea kwenye ukumbi, ilibidi amjulishe asiende tena kutokana na polisi kutoa agizo la kutofanyika kongamano hilo na kisha kuwajulisha washiriki ambao walilaani viongozi wa Jeshi la polisi mkoa na serikali ya mkoa kwa kupiga marufuku kongamano hilo.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti nje ya ukumbi wa OTTU ambako kongamano hilo lililikuwa lifanyike, walisema wanawashangaa viongozi wa polisi kuamua kupiga marufuku kongamano hilo wakati lilikuwa na lengo la kuwaelimisha wananchi kupata fursa ya kujadili waraka wa kanisa Katoliki ili waweze kuuelewa kwa undani zaidi. Washiriki hao walisema viongozi wa Serikali ya CCM wanaogopa waraka huo usijadiliwe kwa sababu ya kuogopa kuumbuliwa kwani wamekuwa na tabia ya kuficha mambo ya msingi wasiyafahamu wananchi ili waendelee kuwanyonya na vitendo vyao vya ufisadi.

Walisema kitendo cha polisi ambao wana imani wamepewa shinikizo kutoka kwa viongozi wa CCM na serikali yao kupinga waraka huo usiweze kujadiliwa na wananchi unatia shaka kuwa kuna ajenda ya siri katika Uchaguzi Mkuu ujao na kwamba hata hivyo wananchi wamepata somo na watajua nini cha kufanya kwenye uchaguzi ujao.
Washiriki wa kongamano hilo walikuwa ni pamoja na viongozi wa dini waislamu na wakristo,wanasiasa wa vyama vyote, wasomi na waandishi wa habari na wananchi ambao wote ni wadau wa maendeleo ya mkoani wa Mbeya.