Askofu Pengo asema, 'Nchi imeoza'

ASKOFU wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo ameibuka tena na kutangaza mapambano mapya dhidi ya mafisadi huku huku akidai nchi imeoza na kamwe kanisa halitakaa kimya na kulea hali hiyo.


“Sisi viongozi wa dini hatuwezi kunyamaza huku tukiona nchi inaendelea kuozeshwa na viongozi wasiozingatia maadili ya utawala bora. Lazima tukemee kwa nguvu zote! ”alisema.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki aliyasema hayo jana wakati wa Jubilee ya Miaka 75 ya Shirika la Masista wa Bibi Yetu Kilimanjaro iliyokwenda sambamba na harambee ya kuchangia Shule ya Sekondari Henry Gogat iliyopo wilayani Rombo.

Aliwataka wananchi kushirikiana na viongozi wa dini kuwafichukua mafisadi na kuwakemea popote pale walipo.

“Wananchi tusaidieni katika vita hii. Viongozi wa dini hawawezi kuwajua mafisadi wote, unaweza kumjua mmoja wapo lakini ninyi mnawajua wengi na wametapakaa nchini kote, hata hivyo tutapambana nao hata angekuwa nani, ”alisema Kardinali Pengo.

Kardinali Pengo alisema Kanisa Katoliki halina mgombea wa urais linayemwandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na baadhi ya watu nchini.

Alisema kanisa halina ugomvi na Rais Jakaya Kikwete katika uongozi wake bali lina ugomvi na mafisadi ambao hutumia nafasi zao kuiangamiza nchi.

Alisema ni jukumu la kanisa katika kuwaelemisha waumini wake na wananchi kwa ujumla kuhusu athari za ufisadi ambazo zimeendelea kulingamiza taifa.

Kardinali Pengo alisema Kanisa halitasita kukemea viongozi wanaotumia madaraka yao kuendeleza na kuwatetea mafisadi bali lipo tayari kuwasaidia watu wote wenye nia njema na nchi katika kuongoza vita ya kupinga vitendo hivyo.

Alisema nyaraka za kichungaji zipo na zinalenga kuamsha wananchi kwa ujumla kwa vile wananchi hao wanawajua mafisadi zaidi kwa sababu wanawatembelea mara kwa mara hususani wakati wa kampeni ili wawachague katika nafasi mbalimbali.

Kardinali Pengo alisema waraka wa Kanisa Katoliki haulengi kutangaza dini hiyo wala kuligawa taifa kwa misingi ya kidini bali unazingatia zaidi kuelimisha wananchi kuhusiana na athari za ufisadi na umuhimu wa kuwa na viongozi waaadilifu.

“Kanisa halina ugomvi na yeyote aliyepo madarakani wala dhehebu lolote la dini. Anayejijua ni msafi waraka wetu haumuhusu, lakini anayehusika na ufisadi hafai kuwa kiongozi wa wananchi,”alisema.

Alisema Kanisa Katoliki halina ugomvi na madhehebu ya dini yanayofuata mipango ya Mungu inavyoelekeza, lakini wasiofuata mipango ya Mungu lazima wakemewe na hawatafumbiwa macho.

Alisema vita dhidi ya ufisadi haichagua dhehebu la dini na kwamba hata kama fisadi huyo atakuwa mkatoliti lazima akemewe na kumueleza waziwazi kwamba kanisa haliko pamoja naye.

Akitoa salamu za serikali,Waziri wa Maliasili na Utalii, Bibi. Shamsa Mwangunga ambaye alimwakilisha Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, alisema serikali itaendelea kushirikiana na taasisi zote kuendeleza sekta ya elimu.

Katika harambee hiyo Waziri Mwangunga alichangia shilingi milioni 11.5.
Chanzo cha habari Na Martha Fataely, Rombo akiliandikia gazeti la Majira.co.tz