Audio & Text: Kauli ya Naibu Waziri kuhusu madai ya Walimu

Image and video hosting by TinyPic
Siku chache baada ya ziara ya Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu na Ufundi, Mwantumu Mahiza, kumalizika mkoani Ruvuma, baadhi ya wadau wa sekta ya maendeleo ya elimu wamekuwa na maswali mengi kuhusiana na baadhi ya kauli na vitendo vilivyofanywa na waziri huyo akiwa mkoani humu.

Baadhi ya kauli ambazo zimezua mjadala ni ile aliyoitoa wakati akijibu mawali ya walimu wanafunzi wa Chuo cha Ualimu cha Songea waliotaka kujua mikakakati ya wizara na serikali ya uboreshaji wa masilahi na mazingira magumu ya walimu, ambapo aliwajibu wanafunzi hao kuwa kama wanaona masilahi ya ualimu ni madogo waache na waende wakasomee kada nyingine.

Kauli hiyo mbali ya kuwakwaza wanafunzi hao pia iliwakwaza walimu walioko makazini na hasa ilipotolewa na waziri mwenye dhamana katika wizara nyeti inayobeba kila sekta nchini.

Wakizungumza na Nipashe baadhi ya wananchi waliosikia kauli hiyo walisema kuwa kwa mtazamo wao waliona wanafunzi hao pamoja na walimu nchini wana haki ya kujua mikakakati ya serikali ya kuboresha masilahi ya walimu na mazingira magumu yanayowakabili katika kazi hiyo ngumu.

Walisema haikuwa sahihi kwa waziri kuwabeza na kuwataka waachane nayo na kwenda kusomea kada nyingine huku akitambua kuwa sekta hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi na kila alipokwenda wakuu wa shule katika risala zao walisema kuhusu upungufu mkubwa wa walimu na yeye akitoa ahadi kuwa serikali inafanya juhudi za makusudi kukabiliana na tatizo hilo.

“Mimi namashangaa mheshimiwa kwa nini anaibeza sekta yake na kutushawishi tuiache na twende tukasome kitu kingine anatuonyesha kuwa tumekuja huku kimakosa,” alisema John Swai mwanafunzi wa ualimu Songea.

Aidha katika tukio jingine akiwa ziarani wilayani Namtumbo alipelekwa kuona shule ya msingi Rwinga, ambayo ni chakavu kimajengo na sakafu ikiwa imebomoka kitendo ambacho kilionyesha kumkera na kudai kuwa ni dharau kwake kupelekwa kuonyeshwa shule hiyo iliyochakaa kiasi kikubwa.

Kitendo hicho kilimfanya Mahiza kuujia juu uongozi wa Wilaya ya Namtumbo na hasa Ofisa Elimu kwa kudai kuwa amemdharau, kauli ambayo nayo ilizua maswali mengi wakidai kuwa viongozi hawapendi kuonyeshwa hali halisi ya mazingira bali wanapenda kuonyeshwa vitu vizuri tu.
Kauli hii ilitolewa baada ya kuulizwa ufafanuzi kuhusiana na madai hayo hapo juuHabari chanzo: IPPmedia.com
Picha katuni: Dr. F. Mashili (MD)
Audio: TBC + DulloNet.com