Marufuku kuvaa nguo zenye rangi ya jeshi

Picha zimetoka kwenye tovuti mbalimbali mtandaoni.
Habari imeandikwa na Hussein Kauli wa gazeti tando la Mwananchi


JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limewataka wananchi kuacha mara moja vitendo vya kununua sare zake zinazouzwa na baadhi ya watu huko mitaani badala yake, watoe taarifa hilo wanapoziona zikiuzwa.

Akizungumza na Mwananchi katika maadhimisho ya miaka 45 ya JWTZ yaliyofanyika katika viwanja vya Airwing, Ukonga jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Huduma na Mavazi, Kapteni Changu Ndile, alisema mavazi hayo wanapaswa kutumia na wanejeshi tu wakiwa kazini, vitani na kwenye sherehe. Kaptemni Ndile alisema hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni, kumeibuka mtindo wa baadhi ya watu kuingiza nchini, sare zinazofanana za JWTZ, chini ya mwamvuli wa nguo za mitumba, jambo ambalo limewafanya wananchi kuzinunua na kuzitumia.

"Kuna sare katika baadhi ya majeshi ya nje zinafanana na za Jeshi la Wananchi wa Tanzania, hizi ni pamoja na za Jeshi la Majini la Marekani, sare hizi huingizwa nchini kama mitumba na kuuzwa kwa wananchi ambao baadaye huzitumia kama mavazi ya kawaida," alisema Kapteni Ndile. Alisema hata hivyo wananchi wanapaswa kujua, utumiaji wa sare hizo ni makosa na kwa hiyo wanapaswa kuachana nazo. "Hairuhusiwi kwa mwananchi yeyote kutumia sare hizi, tafadhali wale wanaouza mitumba wanapopata sare hizi naomba waziwasilishe kwetu kwa sababu kuziuza ni makosa," alisisitiza.

Alisema mara kwa mara jeshi hilo, limekuwa likiendesha misako katika sehemu mbalimbali, kutoka katika mikono mwa raia. Alielezea kufurahishwa kwake na hatua ya baadhi ya wananchi wanaosalimisha sare hizo kwa hiari na kwamba kuna haja kwa wengine kuiga mfano huo.