Mgao wa umeme mikoa sita - TANESCO

Kutokana na kuzidiwa kwa gridi ya Taifa, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), limetangaza magawo wa umeme kwa kipindi kisichofahamika kwa mikoa sita ya Tanzania Bara.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Ofisi ya Mawasiliano Makao Makuu ya TANESCO imetaja mikoa hiyo kuwa ni Mwanza, Shinyanga, Arusha, Kilimanjaro, Tabora na Dodoma.

Mgawo huo, utahusisha vitongoji tofauti katika maeneo yote ambayo yatahusika na mgawo. Mkoa wa Mwanza, umeme utakatika kuanzia saa 12 jioni hadi saa nne usiku. Katika maeneo mengine ya mkoa huo, umeme utakatika kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 12 jioni.

Mkoani Dodoma, umeme utakatika kuanzia saa 12 jioni hadi saa nne usiku kwa kuhusisha vitongoji mbalimbali kama ilivyo kwa mikoa mingine ya Shinyanga na Kilimanjaro.

Shirika hilo limesema taarifa kamili ya mgawo kwa mikoa ya Tabora na Arusha itatangazwa baadaye.