Bibi ajinyonga kwa kuchukizwa kuozwa mjukuu wake aliyekuwa akisubiri matokeo ya mtihani

Habari imeripotiwa katika gazeti tando la Majira.co.tz
Kinachonisahangaza ni kwa jinsi watu wa'kisasa' wanavyojidai kuwa wameendelea sana na hivyo kudharau ama kutupilia mbali wosia tunaopewa na wakubwa zetu waliotutangulia kiumri. Fikira zetu potofu zinatutuma kusaidiki kuwa hao wamepitwa na wakati hivyo hawatuambii lolote la maana. Ndiyo yale yale tumekuwa tukiyazungumzia kuhusiana na wosia wa marehemu Mwalimu, Baba wa Taifa.
Kwa upande mwingine, huenda hali ya uchumi na siasa imewasababisha wazazi wa binti huyu kuona hakuna mwelekeo katika elimu na hivyo kilichobakia ni kuoza tu binti yao ili kupata ndururu za mahari. Inanipa picha kuwa wazazi hawa hawana elimu na hivyo hawawezi kuthamini wala kuona umuhimu wa elimu.
Ninatumai binti huyu atapata fursa ya kuendelea na masomo.
AJUZA mwenye umri unaokadiriwa miaka kati ya 80 na 90 mkazi wa Kijiji cha Mighala, Kata ya Njoro wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Fatuma Kanyorota, amejiua kwa kile kinachodaiwa kukerwa na kitendo cha mjukuu wake,mwenye umri wa miaka 14 (jina tunalihifadhi) kuozwa na wazazi wake wakati akisubiri majibu ya mtihani wa darasa la saba. Bibi huyo aliyejinyonga kwa kitenge, inadaiwa enzi za uhai wake alisisitiza sana umuhimu elimu kwa mjukuu wake huyo aliyemaliza elimu ya msingi mwaka huu.

Tukio hilo lilitokea Oktoba 5 mwaka huu usiku ambapo mwili wake ulikutwa asubuhi Oktoba 6, kwenye mti nje ya nyumba aliyokuwa akiishi. Baadhi ya majirani wa eneo hilo walisema ajuza huyo kabla ya kifo chake aliacha ujumbe kuwa endapo mjukuu huyo aliyekuwa akiishi naye ataozwa katika umri mdogo asije kwenye msiba wake wala asirudi tena kwao na atapata matatizo maishani mwake.

Mjukuu wa marehemu, Bw. Rashidi Irema alisema baada tukio hilo, alitoa taarifa ya kifo hicho katika ofisi ya Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho Bi. Zaituni Abeid ambaye alikiri kutokea tukio hilo na kueleza kuwa iliwalazimu kutoa taarifa Polisi.

Habari zaidi kutoka kijijini hapo zilieleza kuwa baada ya ajuza huyo kujinyonga, majirani walimshusha kwenye mti huo na kwenda kumzika haraka kisha kukata mti huo na kuuchoma kwa mujibu wa mila zao.

Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Bw.Lucas Ng’ohoboko alikiri kupokea taarifa za tukio hilo na kueleza kuwa jeshi hilo linaendelea na uchunguzi kubaini kiini cha tukio hilo.Aidha Kamanda Ng'ohoboko alitumia nafasi hiyo kuwaonya wazazi kuacha tabia ya kuwaozesha mabinti zao na kueleza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wazazi wa aina hiyo.