Chanjo ya UKIMWI yagundulika Tanzania (ni kweli?)

Habari hii nimeotoa kama ilivyoripotiwa na Peter Mwenda na kuchapishwa katika gazeti tando la Majira.co.tz

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS), Profesa Kisali Pallangyo, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu matokeo mazuri ya utafiti wa tiba ya ugonjwa unaodhoofisha kinga ya mwili kupambana na maradhi (UKIMWI) waliofanya kwa kipindi cha miaka 19 ambao umeonesha mafanikio makubwa. Kushoto ni mmoja wa watafiti ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa David Ngassapa. Utafiti huo umegharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 5. (Picha na Charles Lucas)
CHUO Kikuu Cha Afya na Sayansi Kishiriki, Muhimbili (MUHAS) kimesema majaribio ya utafiti wa chanjo ya kutengeneza kichocheo cha kinga dhidi ya maabukizi ya virusi (VVU) umeonesha mafanikio makubwa.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Kisali Pallangyo akizungumza Dar es Salaam jana alisema utafiti ulioanza mwaka 2007 na unaondelea katika chuo hicho umepata mafanikio ambayo yamesaidia kupatikana kwa chanjo ya kukinga maambukizi ya virusi vya UKIMWI. "Majibu ya utafiti wa chanjo ya kukinga maambukizi ya VVU katika Chuo cha MUHAS ni mazuri sana, walioshiriki wote ambao tumewachanja asilimia 100 miili yao imetengeneza kinga ya UKIMWI," alisema Profesa Pallangyo. Alisema baada ya mafanikio hayo MUHAS inatarajia kuwasilisha ripoti hiyo wiki ijayo kwenye hoteli ya Ngurdoto, Arusha na baadaye kwenye mkutano wa chanjo ya UKIMWI utakaofanyika Ufaransa Oktoba 19. Profesa Pallangyo alisema matokeo ya majaribio hayo ambayo yameonesha kutengeneza vichocheo vya kinga dhidi VVU, yanafanana na majaribio ya awamu ya kwanza nchini Swideni,nchi ambayo pia ilitoa fedha za kufanya utafiti kupitia Shirika lao la Maendeleo la Kimataifa (SIDA) ambalo lilitoa fedha za kununulia vifaa na kufanya utafiti.

Mkurugenzi wa Mafunzo wa MUHAS, Dkt. Muhammad Bakari alisema majaribio ya chanjo ya VVU kwa binadamu yalifanywa kwa askari polisi baada kutimiza masharti ya kutokuwa na maambukizi ya VVU ambao wamefanyiwa majaribio ya chanjo ya kuangalia usalama na uwezo wa kutengeneza kinga. Dkt. Bakari alisema japokuwa chanjo hiyo imeonesha mafanikio katika kuzuia maambukizi ya VVU lakini hakuna uhakika kwamba inaweza kuua virusi vya UKIMWI kwa wagonjwa ambao tayari wanaugua ugonjwa huo. Alisema chanjo hiyo inawezesha mwili kutengeneza vichocheo vya kinga ambavyo huenda vikatoa kinga dhidi ya maambukizi ya VVU na kuimarisha zaidi uwezo wa kitaalamu katika kufanya majaribio ya chanjo dhidi ya VVU nchini Tanzania. Dkt. Bakari alisema utafiti huo ambao umefanyiwa majaribio kwa washiriki ambao ni miongoni mwa askari Polisi polisi 60 wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao walikubali kwa utashi na ridhaa yao na katika majaribio hayo hapakuwa na madhara yaliyotokea baada ya kupatiwa chanjo hiyo. Alisema majaribio hayo yalianza kufanyiwa polisi hao baada ya kutimiza vigezo vya kutokuwa na maabukizi ya UKIMWI,afya njema na wenye uwezekano mdogo wa kupata VVU ambao kutokana na ujasiri wao wanastahili kupewa heshima ya kishujaa kama wale wanaokwenda mstari wa mbele vitani.

Katika warsha hiyo, Mratibu wa Maabara wa MUHAS, Profesa Eligius Lyamuya alisema washiriki 24 kati ya 52 walipatiwa chanjo hiyo walifanikiwa kutengeneza vichocheo vya kinga dhidi ya VVU, baada ya kupata chanjo 3 za DNA. Alisema washiriki 35 kati ya 48 nao walitengeneza vichocheo baada ya kupata chanjo ya kupiga jeki na katika chanjo ya tatu washiriki 23 kati ya 59 wametengeneza vichocheo na wengine 34 kati ya 50 walipata chanjo hiyo walipata mafanikio kwa asilimia 100. Profesa Lyamuya alisema pamoja ya mafanikio hayo chuo hicho kinakabiliwa na changamoto ya kuongeza maabara, wafanyakazi wa maabara na kuongeza vifaa vya maabara.

Naye mtaalam wa kinga na magonjwa yanayosababishwa na virusi, Profesa Fred Mhalu na alisema chanjo hiyo isiwe kichocheo cha kufanya ngono bila kufuata ushauri wa kitaalamu wa kuacha kujamiiana na kuchelewesha ngono kwa vijana hadi umri wa kuoana au kuishi pamoja, uaminifu kwa wenye ndoa ambao wamepima na matumizi ya mipira ya kiume au ya kike ambayo ikitumiwa vizuri hukinga kwa asilimia 90. Alisema Tanzania yenye watu watu milioni 40, kati yao, watu milioni 1.4 wameambukizwa virusi vya UKIMWI. Kati yao 760,000 ni wanawake na watoto wanaoishi na virusi ni 140,000. Profesa Mhalu alisema kutoka utafiti huo uanze kufanyika MUHAS umetumia gharama za majaribio ya kutafuta chanjo ya VVU ya Sh.bilioni tano ambazo zimetumika ajili ya kununua vifaa vya kupima vinasaba na kwa sasa imeanzisha programu kwa ajili ya kutoa mafunzo ya mafundi wa maabara.