Madaktari, Wakunga na Wauguzi waweza kushtakiwa kwa vifo vya Mama wajawazito

Habari kwa mujibu wa gazeti tando la Majira.co.tz

Taasisi zinazotoa huduma ya afya na wataalamu wa afya wakiwemo madaktari, wakunga na wauguzi wanaweza kushitakiwa endapo watafanya uzembe unaoweza kusababisha ulemavu au vifo vya wajawazito, wanasheria wamesema.

Kila mwaka, zaidi ya wanawake 8,000 hufariki dunia kwa ujauzito hapa nchini ambapo ni wastani wa wanawake 24 kwa siku kitu kinachoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizo na idadi kubwa ya vifo vya namna hii vinavyoweza kuzuilika. Kauli hiyo ilitolewa na majaji wawili wa Mahakama Kuu, Bi. Aisha Nyerere na Eliamani Mbise wakiwa na wanasheria wengine katika jukwaa la wazi lililojadili jinsi ya kupunguza ulemavu na vifo vya wanawake.

Taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA), Bi. Ananilea Nkya iliwakariri wanasheria hao wakisema, kila mwanchi anayo haki ya kwenda mahakamani kudai haki yake kama uzembe umefanyika na kusababisha madhara au kifo cha mjamzito. Walisema kuwa taasisi au mtu aliyesababisha kifo kwa uzembe anaweza kushitakiwa kwa kutumia ibara ya 14 ya katiba ya Tanzania.

Pia wanaweza kushitakiwa na kutiwa hatiani kwa kutumia ibara ya 233 ya sheria ya makosa ya jinai inayoelekeza kuwa mtu yoyote atakayekuwa ametenda vitendo vya kizembe vinavyoweza kudhuru mtu mwingine au kutoa tiba isiyo sahihi, mtu huyo atakuwa ametenda kosa la jinai. Jaji Nyerere pamoja na Mbisa waliwataka wananchi kutumia mahakama zao kudai haki zao dhidi ya ukatili wa aina yoyote unaochangia vifo vinavyotokana na ujauzito.