Mambo ya Tz ni ya Tz! Mume, mke wanusurika kujamiiana hadharani

Polisi wa Tarime jana walilazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya kundi la watu waliotaka kumlazimisha mwanamke anayedaiwa kushikwa ugoni,afanye mapenzi na mumewe hadharani.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tarime/Rorya, Constantine Masawe leo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Tarime mjini. Amewaeleza waandishi wa habari ofisini kwake kuwa, kabla ya kuokolewa na polisi, mume wa mwanamke huyo nusura afanye tendo la ndoa na mkewe huku umati ukishuhudia.  Mwanamume huyo alimfumania mkewe na mwanamume mwingine jana saa 10 jioni katika nyumba ya kulala wageni ya mfujaji iliyopo mjini Tarime.

Kamanda Masawe amesema, wanandoa hao, ni wakazi wa Kijiji cha Rebu nje kidogo ya mji wa Tarime. “Tulilazimika kuwatawanya wananchi kwa mabomu ya machozi kwa sababu umati wa watu ulizingira Kituo cha Polisi ukitaka tumuachie huyo mwanamke ili wamuadhibu kwa kufanya mapenzi nje ya ndoa au afanye mapenzi na na mume wake mbele yao,” amesema Masawe.  Hadi leo asubuhi, wanandoa hao walikuwa katika kituo cha polisi kwa sababu za kiusalama. “Tunamshikilia mtu na mke wake kwa usalama wao, lakini tutawaachia baadaye tukijiridhisha na hali ya usalama wao,” amesema Masawe.

Kwa mujibu wa Kamanda Masawe, mwanamume anayedaiwa kufumaniwa na mwanamke huyo alikimbia.
Habarileo.co.tz