Padre Franco Sordella na kituo cha FARAJA CENTRE, Mgongo, Iringa - Tanzania!

Ni miaka minne sasa imetimu tangu nilipofika na kushughulika kwa takriban miezi mitatu katika kituo cha Faraja Centre kilichopo mkoani Iringa katika kijiji cha Mgongo, mbele kidogo ya Kihesa na kabla ya kufika Nduli ikiwa utakuwa unatokea Iringa mjini kuelekea Kaskazini.

Historia kamili ya kituo hiki imeelezewa vyema kwa maandishi katika tovuti ya kituo, faraja.org

 
Padre Franco  Sordella ndiye mwanzilishi wa kituo cha Faraja Centre akishirikiana na Padre Giulio Belloti. Pia, katika kituo hiki wamepita na kutoa huduma mbalimbali Mapadre, Watawa na Marafiki wa watoto kutoka nchi mbalimbali, vile vile, wapo wafanyakazi wanaojipatia ujira kutokana na shughuli mbalimbali za kuendesha kituo hicho. Fedha ya kuendeshea kituo inatoka kwa wafadhili wa ng'ambo hasa nchini Italia ikiwa ni pamoja na familia binafsi ya Padre Franco.


Padre Franco (pichani kulia) na Padre Giulio (pichani kushoto - sharubu) wamekuwa wabunifu wa miradi ya kituo, ikiwa ni pamoja na kushiriki katika kuianzisha miradi husika, kuisimamia na kuiendeleza ikiwa ni ndani na nje ya kituo.

Pamoja na shughuli mbalimbali za usiku na mchana katika kuwasaidia wananchi wanaoishi kuzunguka eneo hili, kituo kinatoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na:
  1. Kuanzishwa kwa nyumba na makazi ya kulelea na kutunza watoto wanaoishi katika mazingira magumu na familia zilizoparaganyika.
  2. Kuanzishwa kwa shule ya Msingi Mgongo.
  3. Kuanzishwa kwa Zahanati ya Mgongo (inayotoa pia huduma ya nyumba kwa nyumba kwa watu wanaoishi na VVU).
  4. Kuanzishwa kwa Chuo cha Ufundi (Faraja Vocational Trainign Centre).
  5. Kuanzishwa kwa shule za awali (chekechea) za Njia Panda, Mtalagala na Msisina.
  6. Kuanzishwa kwa visima vya maji katika vitongoji vyote vitatu vya kijiji cha Mgongo pamoja na vijiji vya jirani.

Mwalimu Anneth Mwachula (pichani) ni Mzazi mlezi wa kituo ambaye amekuwa nguzo na mhimili mkubwa kwa kuwapenda na kuwalea vyema watoto wa Faraja. Ama kwa hakika Anneth ni mtu aliyejaliwa ubinadamu, huruma, hekima na moyo wa upendo. Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ampe baraka tele na maisha mema.  Na aone fahari katika kazi anayoifanya!

Kituo pia kinashirikiana na Madhehebu mbalimbali ya kiroho na vikundi vya kijamii vyenye lengo la kutoa huduma inayolenga kumsaidia mwananchi wa kawaida katika kujikwamua katika hali ngumu ya maisha.
Kituo kinafadhili baadhi ya wanafunzi wanaofanya vyema na kufaulu masomo ya msingi na sekondari hadi vyuo vikuu, ama kwa wasiofaulu kuendelea na masomo kwa kujiunga katika shule za Sekondari za Serikali, chuo kimekuwa kikiwafadhili ama kuwatoza ada ndogo wale wote wenye juhudi, vipaji na maarifa katika ngazi ya 'vocational training' ambapo huchagua fani na hujifunza ufundi chuma, au ufundi mbao ama ufundi viatu hapo hapo chuoni.

Baadhi ya watoto nyumbani Faraja wakiwa na Rita (mama mzazi wa Padre Franco) amekuwa akisafiri mara kwa mara toka Italia hadi Tanzania na kuishi kwa muda kituoni.


 
 

Blogu hii inapenda kutoa shukrani za dhati kwa Padre Franco, Padre Giulio, Wafanyakazi, Wafadhili, Watoto na Vijana pamoja na Wanafunzi wa kituo cha Faraja kwa juhudi yao kubwa wanayofanya katika kukiendeleza kituo na kujikwamua kimaisha.

Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema awape faraja wana"Faraja Centre" wote!