Pale wanafunzi wa kidato cha nne walipofanya mitihani usiku, kwa mwanga wa karabai!

Elimu katika karne ya Sayansi na Teknolojia ambapo mwanafunzi anafanya mtihani kwa mwanga wa karabai, kisha hapo mwanafunzi anatakiwa akimaliza shule awe mwepesi wa kutumia kompyuta na zana za kisasa za kupambana na karne hii ya teknolojia. Wakati wa kuomba kazi, ole ni wake ikiwa yote hayo hayajui, ataula wa chuya!

Habari hii imeripotiwa toka Arusha na Hemed Kivuyo wa gazeti tando la Mwananchi
WANAFUNZI wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Elerai, iliyopo Kata ya Elerai Arusha, juzi walifanya mitihani mpaka saa tatu usiku kwa kutumia mwanga wa taa aina ya karabai. Taarifa zilizothibitishwa na wanafunzi na baadhi ya wazazi wa shule hiyo zimesema kuwa, mitihani hiyo ilichelewa kufika shuleni hapo, badala yake ilifika saa11:12 jioni, hivyo kuwalazimu kufanya mitihani hiyo usiku kwa kutumia mwanga wa karabai, kwa sababu shule hiyo haina umeme.

Akizungumza na gazeti hili mmoja wa wanafunzi hao, Mariam Kassim alisema: "Ni kweli tumefafanya mitihani mpaka saa tatu kasoro usiku, kwasababu ilichelewa kufika shuleni". Alilalamika kuwa baadhi yao walishindwa kuona vizuri maswali licha ya kuwepo mwanga wa karabai. Alisema mitihani hiyo ilifika shuleni hapo saa 11:00 jioni na ilipofika majira ya saa moja usiku, baadhi ya wanafunzi waliacha kujibu maswali kutokana na kuumwa macho. "Tulifanya mitihani mpaka saa tatu kasoro usiku na giza lilipoongezeka tuliletewa karabai, lakini wengine waliokuwa wakiumwa macho walishindwa kuendelea kujibu maswali yaliyosalia," alisema Mariam.

Mwanafunzi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Aisha Athumani (19), alisema walisubiri mitihani kwa muda mrefu hadi jioni wakiwa wamekata tama; ndipo ikafika lakini walifanya kwa shida kutokana na mwanga hafifu wa karabai ambao ulikuwa ukiwaumiza macho.

Mmoja wa wazazi wenye watoto wa kidato cha nne katika shule hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Zuberi Hamadi(43), mkazi wa Majengo alisema kuwa alishtuka baada ya mtoto wake kuchelewa kurudi nyumbani na ilipofika saa mbili za usiku aliamua kwenda kumtafuta shuleni. Alipofika shuleni alikuta wako katika chumba cha mitihani. Alisema kuwa hali hiyo iliwashtua wazazi wengi kwani alipofika shuleni hapo alikutana na watu wengine ambao walifika kuwatafuta watoto wao baada ya kuchelewa kurudi nyumbani. "Tuliamua kwenda shuleni baada ya kuona watoto wamechelewa kurudi nyumbani na nilipofika shuleni nilikutana na wazazi wengine. Tukaambiwa na walimu kwamba, bado wanafanya mitihani,"alisema Athumani.

Awali akiongea na kituo kimoja cha redio, Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha, Rafael Mbunda alisema hafahamu kama wanafunzi hao walifanya mitihani mpaka usiku na kuahidi kuwa muda huo huo anaondoka kwenda kulifuatilia jambo hilo. Baada ya muda alipopigiwa simu yake ya kiganjani, hakuipokea na baadaye ikazimwa na kutopatikana kwa muda mrefu. Afisa Elimu wa Manispaa ya Arusha anayeshughulika na sekondari, hakupatikana ofisini kwake na msaidizi wake alisema kuwa yupo nje ya ofisi kikazi na yeye hawezi kusema kwa sababu hana mamlaka hayo.

Naye Diwani wa kata hiyo, Anaelsoni Ole Joel alisema hana taarifa za wanafunzi kurejea nyumbani usiku baada ya kuchelewa kufanya mitihani na kuahidi kwamba atafuatilia.