Taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu Watumishi hewa ktk Sekta ya Afya

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS
MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU WATUMISHI HEWA KATIKA SEKTA YA AFYA

SEPTEMBA 26, 2009

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma imefanya uhakiki wa raslimali watu katika Sekta ya Afya na kugundua kuwepo kwa watumishi hewa 1,511 waliosababishia taifa hasara ya jumla ya shilingi
4,482,992,570/- (4.48bn/-) zilizotumika kulipa mishahara ya watumishi hewa tangu mwaka 2005 hadi Machi 2009 walipoondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara.

Zoezi la uhakiki wa raslimali watu katika Sekta ya Afya lilifanyika katika mwaka wa fedha 2008/2009 kwa lengo la kuangalia matumizi ya Raslimali watu na ubadhirifu katika eneo la malipo ya mishahara.
Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma waliofanya zoezi hili kwa kutembelea Hospitali, Vyuo vya Afya na Zahanati mbalimbali 3,519 nchi nzima walikuta watumishi 39,247. Aidha, watumishi hewa 1,511 waligundulika wakati wa zoezi la uhakiki wa raslimali watu ambao walikuwa wakilipwa mshahara kupitia Benki.

Taarifa ya ukaguzi wa raslimali watu inaonyesha kuwa Wizara ya Afya na Taasisi zake pamoja na mikoa yote ya Tanzania Bara ilikuwa na watumishi hewa waliokuwa wakilipwa mishahara na Serikali wakati ya wafanyikazi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kufariki dunia, kustaafu, kuacha kazi na kuhamia taasisi nyingine wakati wengine wamekuwa wakilipwa mishahara mikubwa kuliko stahili zao.

Taasisi za Sekta ya Afya zilizotembelewa na kufanyiwa uhakiki wa raslimali watu ni pamoja na Wizara ya Afya, Hospitali za Rufaa, Hospitali za Mikoa, Hospitali za Mashirika ya Dini, Hospitali Teule, Hospitali za Wilaya, Vyuo/Taasisi za Afya na Wakala, Vituo vya Afya na Zahanati.

Taarifa hiyo inaonyesha kuwa Wizara ya Afya na taasisi zake zimekutwa na watumishi hewa 395 kati yao 364 wanatoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo ndiyo inaongoza kwa kuwa na watumishi hewa wengi kuliko taasisi nyingine katika sekta hiyo.

Mikoa inayoongoza kwa kuwa na watumishi hewa wengi katika sekta ya Afya ni pamoja na Arusha (101), Tanga (96), Tabora (93), Pwani (83), Ruvuma (81), Mwanza (71), Lindi (71), Iringa (68) na Morogoro (62).
Aidha, idadi ya watumishi hewa waliokutwa katika mikoa mingine ni pamoja na Dodoma (49), Kagera (48), Kilimanjaro (44), Rukwa (44), Manyara (39), Mbeya (39), Shinyanga (30), Dar es Salaam (29), Singida
(28), Mara (18), Mtwara (17) na Kigoma (5).

Tatizo la kuwepo kwa watumishi hewa limeonekana kuwa sugu kwa waajiri walio wengi kushindwa kuwafuta watumishi katika orodha ya malipo ya mishahara wanaofikia tamati katika utumishi wao kutokana na sababu
mbalimbali. Tatizo hili linachangiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na ukosefu wa uwajibikaji miongoni mwa maafisa wenye dhamana ya masuala ya kiutumishi katika taasisi za Serikali.

Serikali itachukua hatua kali kwa wale wote watakaobainika kushiriki kwa namna moja au nyingine katika kusababisha kuwepo kwa watumishi hewa katika orodha ya malipo ya mishahara serikalini.

Napenda kutoa agizo kwa waajiri wote nchini kuangalia suala zima la watumishi hewa katika orodha za malipo ya mishahara kwa watumishi wao ili kuondoa upotevu wa fedha nyingi za Serikali zinazolipwa kwa watu ambao hawalitumikii taifa.

Hii ni mara ya pili kwa Serikali kufanya uhakiki wa Raslimali watu tangu Serikali ya Awamu ya Nne iingie madarakani. Katika Uhakiki uliofanywa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma katika Sekta ya Elimu mwaka 2007 jumla ya watumishi hewa 1, 413 waligundulika kulitia taifa hasara ya kiasi cha shilingi bilioni 3.044bn/=.

Hatua mbali mbali za kinidhamu zinachukuliwa kwa wahusika walioshiriki katika kufanikisha kuwepo kwa watumishi hewa kwenye sekta ya Elimu. Zoezi la uhakiki wa Raslimali litafanyika katika taasisi zote nchini na hivi sasa linaendelea katika sekta ya Sheria ambapo Mahakama zote zitapitiwa.

Imetolewa na;
Mh. Hawa A. Ghasia (Mb),
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma
26, Septemba, 2009
Dar es Salaam

Pakua nakala ya tangazo hili kupitia linki ifuatayo: http://bit.ly/VxX6h