Tangazo: Mgawo wa umeme Tanzania nzima

Itakumbukwa kuwa tarehe 15 ya mwezi jana ulitangazwa mgao wa umeme kwa mikoa sita nchini. Leo, taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCo), Dk. Idris Rashidi inasema kuwa, nchi nzima itakuwa katika mgao wa umeme unaoanza mara moja kwa kukatika tangu saa 3:00 asubuhi hadi saa 5:00 usiku. Meneja Mawasilino wa TANESCO, Badra Masoud, alisema ratiba kamili ya mgawo huo kwenye maeneo mbalimbali itatolewa karibuni.

Sababu za mgawo
  1. Kupungua kwa kiwango cha maji katika mabwawa ya kuzalishia umeme ya Kihansi na Pangani na hivyo kusababisha kiwango cha uzalishaji uememe kushuka katika gridi ya Taifa.
  2. Ukame katika majira ya kiangazi.
  3. Kuharibika kwa mtambo wa Songas, Kihansi na Hale (Tanga).

Mipango
TANESCO ina mpango wa kuhakikisha kuwa:
  1. Mtambo mpya wa Tegeta (Dar es Salaam) wa megawati 45, unaanza kazi mwezi ujao
  2. Mtambo wa Songas wa Unit 1 na megawati 20 matengenezo yake yatakamilika haraka iwezekanavyo kabla ya mwisho wa mwezi huu.
  3. Mtambo wa Kihansi Unit 1 wenye megawati 60, matengenezo yake yatakamilika katikati ya Desemba mwaka huu.
  4. Shirika litashirikiana na Serikali kuanza maandalizi ya ununuzi wa mitambo mingine ya kuzalisha umeme ili kukidhi mahitaji ya umeme mwaka ujao na siku za baadaye.

Matarajio?
Mvua za vuli zinategemewa kuanza Novemba na kuboresha hali ya uzalishaji umeme wa kutumia maji.


Yatokanayo
Nadhani hili suala la umeme si mlima mrefu kiasi hicho kupanda, hasa ukizingatia kuwa nchi hii imekuwa katika tatizo hili kwa miaka nenda rudi tangu tumepata uhuru toka kwa mkoloni mwaka 1961!
Miaka ya mwanzo Marehemu Baba wa Taifa (JK Nyerere) alisema tuipe muda nchi, ndiyo kwanza inajikongoja, tunahitaji wasomi na wataalamu wengi katika nyanja mbalimbali ili tuweze kutatua matatizo yetu wenyewe. Tunapozungumza hivi leo katika karne ya 21 ambapo baadhi ya nchi zinajitahidi kutengeneza umeme utokanao na nishati ya nyuklia, ni jambo la kusikitisha sana kuona kuwa sisi wa Tanzania bado tunategemea maji ya mvua kuzalisha umeme na bado hatuwezi kuyatumia vilivyoo. Naafiki tunapojitetea kuwa hatuna wataalamu wa sayansi ya nyuklia kuzalisha umeme wa uraniam, lakini hatutumii wasomi wetu na wale wa nje katika kuyahifadhi maji yanayotumika ili kuyarudia tena na tena badala ya kuyaachilia.
Nchi inakadiriwa kuwa na kiwango kikubwa cha madini ya Uraniam ambayo ndiyo yanayotumika, kuzalishia umeme pamoja na shughuli za utengenezaji vifaa vingine hasa mabomu ya vita, cha kusikitisha ni kuwa madini haya inavyoelekea yatafaidisha nchi nyingine na Tanzania tutaishia kujisifu kuwa tunapata pato ambalo mwishowe, kama ilivyo katika nyanja nyingine, tutasikia habari za pato hilo kufisadiwa.