Wale vilaza wa IFM waliofanyiwa mtihani na vijana wa Azania Sec. watajuta

Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) waliofanyiwa mtihani wa Hesabu na wanafunzi wa Sekondari ya Azania wamekali kuti kavu na mchakato wa kushughulikia adhabu yao umeanza huku ikielezwa kuwa adhabu yao ni kufukuzwa chuo.

Akizungumza na majira Dar es Salaam, Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Edwin Mjema alisema wanafunzi hao wa mwaka wa tatu walikamatwa wiki ilioyopita nje ya eneo la chuo wakisubiri wanafunzi wa Azania waliokuwa wanawafanyia mtihani. "Kwa kweli tukio hilo limenisikitisha sana kwa sababu sheria, kanuni na taratibu za mitihani zinatolewa siku ambayo mwanafunzi anajiunga kwa mara ya kwanza, lakini lazima waitwe na kujieleza kuhusina na tukio hilo ikiwa ni pamoja na kutaka kujua njia wanazotumia kufanya ujanja huo," alisema Prof. Mjema na kusisitiza kuwa adhabu ya kosa hilo ni kufutiwa mtihani na kufukuzwa chuo. Alisema Bw. Frank Kaduma aliyekuwa mwanafunzi wa sekondari ya Azania alikuwa anamfanyia mtihani Bi. Tina wakati Bw. John Kapinga mhitimu wa kidato cha sita 2003 alikuwa anamfanyia Bw. Joeli Mlengule anayesoma stashahada ya juu. Prof Mjema alisema wanafunzi hao wa Azania walipohojiwa walikiri kufanya hivyo kwa ahadi ya kupewa Sh. 150,000 kila mmoja baada ya kufanya mtihani huo.

Hatua hiyo imekuja baada ya wanafunzi hao wakiwa mwaka wa kwanza kufeli somo hilo, kuwalazimu walirudie somo sasa, na kwa kuwa hawakuwa hanalielewi vyema walilazimika kukodisha vijana hao kutoka sekondari kuwafanyia mtihani huo.

Prof Mjema alisema pamoja na kwamba wakati tukio hilo yeye hakuwepo, lakini atahakikisha zinachukuliwa hatua kali kukomesha tabia hiyo ambayo inaendelea kukithiri chuoni hapo. Alisema kabla ya kuanza kwa muhula wa mwaka huu lazima kesi zote ikiwamo ya hao wanafunzi zitajadiliwa na kutolewa adhabu ambayo itakuwa fundisho kwa wanafunzi wengine.
Grace Ndossa na Neema Kalaliche, majira.co.tz