Watu wasiojulikana wamwaga sumu kwenye mto Ruvu

Habari imeripotiwa katika gazeti la Alasiri
Katika hatua inayozua hofu kubwa, watu wasiojulikana wamemwaga sumu kwenye mto Ruvu, mto ambao maji yake hutumiwa na wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam, Pwani na kwingineko. Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Absaloom Mwakyoma imeeleza kuwa, sumu hiyo ilimwagwa ndani ya mto huo juzi, Oktoba 4 majira ya saa 4:00 asubuhi.

Taarifa hiyo inaeleza zaidi tukio hilo kama hivi:
Juzi majira ya asubuhi katika maeneo ya Kware wilaya ya Kibaha mkoa wa Pwani, watu mbalimbali walionekana wakiuza samaki wabichi kwa bei ndogo sana. Polisi walipofuatilia, walipata taarifa kwamba katika maeneo ya Kigogo Kimara Misale, wilayani Kisarawe ambayo iko mpakani mwa mkoa wa Morogoro na Pwani, watu wasiojulikana waliweka sumu kwenye maji ya mto Ruvu na kusababisha samaki wengi wa mto huo kufa ovyo. Baada ya Polisi kupata taarifa hiyo, walifanya msako na kuwakamata watu wanne ambao walikuwa wakiuza samaki hao. Watu waliotiwa mbaroni na Polisi ni Said Hucha, 42, mkazi wa Mlandizi, Hassan Shaaban, 22, mfanyabiashara wa Mlandizi, Salum Mohamed, 23, mkazi wa Mlandizi na Khalfan Simba, 19, mkazi wa Dutuini. Watu hao wanne walikamatwa wakiwa na samaki ambao inasadikiwa wamevuliwa kwa sumu, lakini walipohojiwa wakadai kuwa waliuziwa na watu wasiowafahamu.

Kutokana na tukio hilo, Polisi wamewatahadharisha wananchi wa maeneo mbalimbali jirani na mto Ruvu kutotumia maji hayo, kutonunua wala kula samaki waliokotwa katika maeneo hayo katika kipindi ambacho upelelezi unaendelea. Kamanda Mwakyoma amesema Polisi mkoani Pwani imekubaliana na uongozi wa mitambo ya maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini, kuyafanyia uchunguzi maji hayo kabla hayajasafirishwa kwenda katika maeneo mbalimbali kama vile Jijini Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Pwani kwa ajili ya mtumizi ya binadamu. Amesema uchunguzi huo unatakiwa kufanyika kila baada ya dakika 15 badala ya utaratibu wa kawaida ambao maji hayo yalikuwa yakichunguzwa kila baada ya saa moja. Kamanda katika taarifa hiyo amesema watuhumwa waliokamatwa wanahojiwa na watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika. "Upelelezi unafanyika kutafuta watuhumiwa wengine waliohusika kuweka sumu kwenye maji hayo, pamoja na hayo, sampuli ya maji yanayohisiwa kuwa na sumu imechukuliwa pamoja na samaki wanaohisiwa kufa kwa sumu, ili kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali," imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Afisa Uhusiano wa Hospitali Teule ya Tumbi, Bw. Gerald Chami amesena hadi jana mishale ya saa 6:00 usiku hapakuwa na mgonjwa aliyefikishwa hospitalini hapo kwa kudhurika na maji hayo.

Akizungumza na Alasiri jana, Meneja wa Mitambo wa Ruvu, Bw. Khalfan Kefa alisema amepokea simu nyingi kuhusiana na uvumi huo, lakini akasisitiza kuwa sumu iliyowekwa mtoni haina madhara kwa binadamu. Uchunguzi uliofanywa na Alasiri umebaini kuwa baadhi ya wananchi hivi sasa wanaogopa kunywa maji ya bomba wakihofia usalama wao.

Mitambo ya kusukuma maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini, ndiyo inayosambaza maji katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Pwani kama vile katika miji ya Chalinze na Kibaha.