Wewe unakaa katika kiti cha rais?, kwa nini unafanya hivyo, ina maana hata siku nyingine unaweza...

Habari hii iliripotiwa na Sadick Mtulya kwenye gazeti tando la http://mwananchi.co.tz
Kikwete akataa kiti chake, afisa mwandikishaji akikalia

Aafisa wa kituo cha kuandikisha wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa, Issa Kipengere juzi alikalia kiti maalum alichoandaliwa Rais Jakaya Kikwete alipokwenda kujiandikisha baada ya mkuu huyo wa nchi kukikataa kiti chake. Lakini baada ya kukalia kwa dakika chache walinzi walimtimua ofisa huyo kwenye kiti hicho licha ya kupewa ruhusa na Rais Kikwete. Kabla ya rais kufika kwenye kituo hicho cha Shule ya Msingi ya Bunge, wasaidizi wake waliweka kiti hicho ndani ya chumba cha kuandikishia wapiga kura na baada ya kufika ofisa huyo alisimama kumkaribisa Kikwete, lakini badala yake rais alikwenda kukalia kiti kingine.

"Ahaa, wewe kaa tu mimi nitakaa katika hiki kiti (cha mwandikishaji) halafu wewe ndio ukae katika hicho kiti (cha rais)," alisema Rais Kikwete alipoombwa na ofisa huyo wa kituo hicho namba moja akalie kiti kilichoandaliwa na wasaidizi wake.

"Mimi hapa nimekuja kujiandikisha hivyo ninastahili kukaa hapa na wewe (ukae) hapo."

Hata hivyo Kipengere alikataa kukikalia kiti hicho na mara baada ya rais kuondoka kituoni hapo, ofisa huyo alikalia kiti hicho cha rais, lakini hakukifaidi kwa muda mrefu kwani afisa usalama mmoja kutoka Ikulu alimkaripia vikali kwa kitendo hicho.

"Wewe unakaa katika kiti cha rais?, kwa nini unafanya hivyo, ina maana hata siku nyingine unaweza...,"alifoka ofisa huyo wa usalama.

Kipengere, 45, ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Bunge aliiambia Mwananchi baadaye kuwa kuwa hiyo ni mara yake ya kwanza kukaribiana na Rais Kikwete. "Nimejisikia ni mtu mwenye bahati kumuandikisha, kuwa karibu naye, na kuonana naye ana kwa ana Rais Kikwete. Sijawahi kupata nafasi kama hii katika maisha yangu," alisema Kipengere.

Kikwete pia aliwahi kukataa kukaa kiti kilichoandaliwa na wasaidizi wake wakati wa misa ya kumuaga mbunge wa zamani wa jimbo la Mbeya Vijijini, marehemu Richard Nyaulawa iliyofanyika jijini Dar es salaam baada ya maofisa hao wa usalama wa taifa kumuandalia kiti ambacho kilikuwa kikitumiwa na padri aliyekuwa akiendesha misa hiyo.