Yah. Hotuba za Mwalimu: Leo ntasema tu, mlochukia mjue nami pia sijafurahishwa kwa kauli zenu

Jambo la kushangaza sana kwa jinsi tunavyopenda kushikilia heshima za uongo na adabu za woga.

Mwaka ulopita, na kisha juzi na jana nilitoa linki zenye hotuba za Marehemu muasisi wa Taifa la Tanzania, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Nilipokea maoni ya watu mbalimbali walioonesha furaha yao kwa kuweza kumsikiza tena marehemu Mwalimu kwa kauli zake alizokuwa akizitoa katika mihadhara  na kwa kuhutubia. Hotuba hizi zinaturejeza kuwaza na kufikiri juu ya mustakabali (maisha ya sasa na mbeleni) wa nchi na Taifa letu. Ama kwa hakika Mwalimu alisema mambo ambayo kwa wakati ule alioyasema, alionekana kana kwamba ni mtu mkali na anayekaripia tu, na kwa hivyo kila alichosema alionekana kama vile aliwazuia watu fulani kutekeleza azma na nia zao wanazozijua wao wenyewe ( ama kwa uzuri au kwa ubaya, wanajua wao) kuhusu nchi yetu kwa ujumla wa rasilimali zake na watu wake.

Kinachonishangaza, ni kwa jinsi ambavyo mtu anadiriki kunitumia ujumbe kuwa hizi hotuba hazikupaswa kuwekwa hewani bure bure hivi ili watu wazisikize na kuziona!
Ama? 
Ati kwa sababu ya hati, sijui haki, (ama vyote) miliki. Inanishangaza sana kuwa mtu au watu wenye akili timamu wanaweza kufanya hotuba za Marehemu Mwalimu mtaji na mradi wa kuzalisha fedha.
Ndiyo ninashangazwa kwa kuwa, katika hali tuliyo nayo nchini sasa hivi, nilitarajia tuwe na umoja na tuungane katika kusikiliza hotuba hizi na kujifunza kuhusu yale yanayotufaa na kuacha yale tusiyoyaona yanatufaa. Nina imani kuwa, mwenyewe marehemu Mwalimu aliongea hivi wazi wazi kwa madhumuni ya kufikisha ujumbe kwa wananchi. Sasa ninyi mnaokatazia hotuba zake, hata kwa sisi tuliozipata kwa njia tunazoziua sisi, mna lengo gani hasa? Nikufahamuni vipi ajenda zenu?

Kuzuia kauli za Mwalimu kwa kuwa zinawasuta nyoyo zenu kwa kukemea uovu wenu ni ujinga. Lakini ujinga wenu utawaaminisha kuwa kauli za Mwalimu hazina maana, haziendani na wakati na zinapoteza muda (kwa mtizamo wa akili zenu?) kwa hivyo mzizuie zisisikike.

Mnanishangaza sana mnapodhani kuwa, kwa vile zilirekodiwa na vyombo kadhaa vya habari, basi iwe ni mali binafsi ya vyombo hivyo. Mnachoshindwa kufahamu ni kuwa, upo ukomo wa kuhodhi kazi ya mtu tena aliyoitoa bure. Nadhani mwenyewe angekuwa hai angewaona ninyi wajinga kabisa kabisa kwa kuzuia hotuba zake kichoyo kichoyo tu, na pengine angekusemeni hadharani ili mpate soni.

Hivi, unawezaje kujisifu kuwa bingwa wa kuzuia na kuficha elimu? Hizo ndizo sifa za kijinga na kipuuzi kabisa. Huu si ndiyo upumbavu ambao umesababisha Tanzania tukawa nyuma kielimu tangu tulipopata ile sifa ya miaka ya kati ya 80 kuwa Taifa lenye watu wake wengi wenye kujua kusoma na kuandika iliyochapishwa na Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Elimu (UNESCo)?
Sikiza bwana n'kwambie msingi mmoja wa biashara, kama ilivyo kwa bidhaa adimu, na kwa elimu ndivyo, "ukishindwa kuitoa elimu bure, walao uiuze ili ikufaidie wewe na anayeinunua. Wewe upate kipato, na anayeinunua apate elimu (a win-win situation). Sasa ninyi mu wajinga, kwa maana mnaiatamia na hamjui siku gani itatotoa kitu gani.

Sijui niwaweke fungu gani ninyi mnaodhani kuwa kuzificha hotuba za Mwalimu itakufaidieni sana hapo siku za usoni. Imekuwa hisa hizo? Mmezigeuza lulu na vito vya thamani kwa faida yenu wenyewe ili mvune jasho la mtu aliyezungumza bure pasina visa wala hiyana. Gharama za kurekodia na uhifadhi isiwe chanzo cha kutesa wananchi wasipate fursa ya kuzisikiza, kumbe mlizirekodi kwa kazi gani hasa? Ni nyara za Serikali?

Mnaudhi kweli kweli kwa mawazo yenu myembamba na finyu. Mjifunze kubadilika au "endeleeni kubana, mkichoka mtaachia", na siku mtakapoachia mtajiona wajinga sana. Zitakaposikizwa na watoto wa watoto wenu, watakuulizeni ni kwa nini mlizibania, na ninyi msivyokuwa na dogo wala lepe la aibu, hamtakosa majawabu hata japo kwa kuwaongopea watoto wenu wa kuwazaa wenyewe. Mnaudhi kweli kweli ninyi!

Mwalimu angefufuka na kukuta upuuzi huu mnaoufanya sasa hivi, nina hakika angekufa tena ghafla!