Bunge la Katiba: Taarifa ya UVCCM Pwani kuhusu posho

Kwanza kabisa nimshukuru Mungu kwa kutukutanisha hapa leo. Pia nawashukuru kwa kuitikia wito wetu hapa ili tuweze kuzungumza nanyi juu ya Jambo hili la Msingi na la ki historia katika nchi yetu. Japokuwa historia hii imeanza kwa kujengwa na aibu kubwa, aibu kubwa ya wahusika wa kuu wa kushiriki jambo hili la kizalendo badala yake wao kutanguliza roho ya ulafi na ubinafsi.

Ndungu zangu wana habari;

Sisi vijana wa CCM wa Mkoa wa Pwani tunaomba mtufikishie haya yafuatayo kwa wabunge wa Bunge maalum la katiba na Jamii kwa ujumla

  1. Sisi UVCCM Mkoa wa Pwani tumesikitishwa sana na Hatua ya Wateule hao kutoka kwenye makundi yao mbali mbali na kuthibishwa/kuteuliwa na Rais ili kushiriki katika Bunge Maalum la kutunga katiba ya Nchi yetu, badala yake kusahau kilichowasukuma wale waliowaona na kuwapendekeza wao na kuja kufanya Posho ni kipaumbele nambali wani. Ni jambo la fedheha na wamewakatisha tamaa watanzania walio wengi
  2. Tumepata mashaka na dhamira zao kwa Taifa hili Masikini, Lenye Matatizo Lukuki, njaa, ukosefu wa huduma za maji safi, afya, matatizo ya madeni ya watumishi, kufikiria posho ya shilingi 300000 kwa siku kwa kila mjumbe kwa watu 600 kwa kipindi cha miezi mitatu ni kiasi kidogo. Huu ni usaliti mkubwa, ni matusi makubwa na dharau kwa watanzania Masikini walio wengi.
  3. UVCCM Mkoa wa Pwani tumeanza kupungukiwa na imani ya kupata katiba yenye maslahi ya watanzania walio wengi kutoka kwa wajumbe walioanza kuonyesha kutanguliza maslahi binafsi. Sisi tunaamini ya kwamba, ni uwendawazimu mkubwa kutegemea kupata asali kutoka kwenye kikundi cha siafu.
  4. UVCCM Mkoa wa pwani tumefikiria kujiridhisha kwamba, ubinafsi ndio sababu kubwa sana unaofanya maendeleo katika sekta na taasisi mbali mbali za taifa letu yasipatikane kwa haraka, kwani viongozi na washiriki wa taasisi hizo wengi wao ni wa binasfi na hawafanyi mambo kwa maslahi ya taasisi zao na kwa maslahi ya taifa lao. Tunaamini hivyo kwasababu, wadai posho hawa ndio viongozi wa taasisi na makundi mbali mbali ya jamii zetu ambao ndio wasimamizi wa maendeleo yetu. Hatuwezi kupata maendeleo yanayosimamiwa na wasimamia ongezeko la posho katika masuala ya kimsingi na ya kizalendo kama hili la kutunga katiba ya Taifa letu Masikini
  5. UVCCM Pwani tunatoa wito kwa wabunge wote wa bunge la katiba wanaofikiria kuuaga umasikini kwa gharama za masikini wa Taifa hili kupitia ongezeko la posho wajiuzulu na kuendelea na shughuli zao zinazowapatia pato la zaidi ya 300000 kwa siku. Wawaachie watanzania wazalendo watakaoifanya kazi hiyo kwa moyo wa kizalendo bila kusababisha kusimama huduma zingine kwa jamii kwa kuelekeza rasilimali kubwa kuhudumia watanzania 600.

Mwisho kabisa tunaiomba serikali kuchunguza kwa ukaribu mwenendo wa ulipaji kodi kwa wale wabunge wote wanaoomba ongezeko la posho kwenye bunge la katiba. Kwani inaonyesha wana kipato cha zaidi ya shilingi 300,000 kwa siku, hivyo serikali haina budi kujiridhisha kwamba kipato chao kama kinalingana na kiwango cha kodi wanacholipa kwa serikali yetu.

Wenu katika ujenzi wa Taifa
Mohamed Nyundo
M/kiti UVCCM MKOA WA PWANI
MNEC (W) MAFIA
0654326405