Bunge la Katiba: Wamwomba Rais Kikwete awateue kuwakilisha Wanamuziki


Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Muziki Tanzania (TMF), Salim Mwinyi (kulia), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi, wakati wakimuomba Rais Jakaya Kikwete kwa mamlaka aliyonayo kuwaingiza wawalikisi wa tasnia ya muziki katika Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea mjini Dodoma. Kushoto ni Katibu Muenezi wa Chama cha Muziki wa Injili Tanzania (Chamuita), Stellah Joel na Mwenyekiti wa chama hicho, John Shabani. (picha: Dotto Mwaibale)

Na Dotto Mwaibale — WANAMUZIKI nchini wamemuomba Rais Jakaya Kiktwete kuwateua wawakilishi wa kundi hilo ili kuingia katika Bunge Maalumu la Katiba kwa kuwa bado anayonafasi ya kufanya hivyo.

Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Katibu wa Chama cha Muziki wa Injili Tanzania (Chamuita), John Shabani kwa niaba ya Rais wa Shirikisho la Vyama vya Muziki Tanzania (TMF).
"Tunamuomba rais wetu kutokana na nafasi yake aliyonayo kuwaingiza wawakilishi kutoka katika kundi la wanamuziki ili kuingia katika bunge hilo ambalo limekosa uwakilishi ukiachilia mbali wabunge wanamuziki ambao wapo katika bunge hilo kupitia majimbo yao"
Alisema Shabani.

Alisema wanajua kuwa bunge hilo limekwisha anza lakini bado hatua ya majadiliano haijaanza hivyo
 watakuwa hawaja chelewa iwapo rais atawateua baadhi yao kuingia katika bunge hilo ili nao wapeleke hoja zao ziingie katiba hasa kutokana na kazi zao kuibiwa na maharamia ambapo hakuna sheria ya kuwabana.

Shabani alisema kutokuwepo mwakilishi yeyote kutoka katika vyama vya muziki ambao wanaunda shirikisho lao (TMF) ni kuwanyima fursa wanamuziki ya changamoto zinazowakabili kuingizwa katika katiba ili kuzipatia ufumbuzi.

Katibu Muenezi wa Chama cha Muziki wa Injili Tanzania, Stellah Joel alisema wana muziki wote kwa pamoja wamekuwa wakiibiwa kazi zao na kushindwa kupiga hatua ya maendeleo kwa kuwa hakuna sheria rasmi iliyopo hivyo wanapenda kuwepo kwa wakilishi katika bunge hilo ili iwekwe sheria katika katiba mpya itakayosaidia kuwashughulikia wezi wa kazi zao.
"Tuna jua rais wetu ni mtu wa watu na mpenda maendeleo ya michezo ikiwemo muziki hivyo atasikia kilio chetu"
Alisema Joel.

Katibu Mkuu mstaafu wa TMF, Salim Mwinyi alisema ni wakati muafaka wa kumaliza tatizo la kuibiwa kazi za wanamuziki kwa kuingiza sheria katika katiba hiyo kupitia wawakilishi wao kuingia katika bunge hilo maalumu la katiba.

Alisema ni vizuri kikanzishwa chombo maalumu kitakachokuwa kikisimamia ukusanyi wa kodi kutokana na kazi za wasanii wa muziki kama ilivyo kwa wenzetu wa nchi nyingine.

Mwinyi alisema wanamuziki wa Tanzania ni maskini kutokana na kutokuwepo kwa ulinzi wa kisheria wa kazi zao tofauti na wenzano kama Afrika Kusini ambapo mwanamuziki akitoa albamu moja tu anakuwa na maendeleo makubwa.
"Hapa kwetu kuna wanamuziki wanametoa albam mpaka nne lakini hata baiskeli hawana wanaishi kwa kuombaomba ni hiyo inatoka na kuibiwa kazi zao ambazo zinawanufaisha watu wengine"
 Alisema Mwinyi.