Dar es Salaam, Februari 24, 2014 --Ilikuwa ni siku ya aina yake kwa bendi ya Extra Bongo "wazee wa kizigo" walipokuwa wakizindua albamu yao ya mtenda akitendewa na kuacha gumzo kwa mamia ya mashabiki waliojitokeza ukumbini humo asante kwa udhamini wa Vodacom kufanikisha Tamasha hilo.
Palikuwa hapatoshi katika ukumbi huo wa taifa wa burudani wa Dar Live uliopo
Mbagala jijini Dar es Salaam ambapo bendi kaadhaa za muziki wa dansi na wasanii wa bongo flava zilitumbuiza kabla ya uzinduzi wenyewe kufanyika.
Kivutio kikubwa zaidi kilikuwa ni pale ambapo kiongozi wa bendi ya Extra Bongo, Kamarade Ali Choki alipoingia na gari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) ukumbini kutumbuiza mashabiki wake waliofurika kwa wingi.
Uzinduzi wa albamu hiyo iliyokwenda kwa jina la Mtenda akitendewa ulikwenda sambamba na burudani lukuki kutoka kwa wanamuziki mbali mbali mashuhuri nchini kama vile malikia wa mipasho nchini Khadija Omari Kopa, Banza Stone, Abdul Misambano, Mashujaa Band pamoja na wasanii wa bongo flava Linah na Amini ulidhaminiwa na kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom.
Wanenguaji wa Extra Bongo walifanikiwa vilivyo kuzikonga nyoyo za mashabiki ukumbini hapo kwa kupagawisho vilivyo jukwaani kwa staili mbali mbali mpya za uchezaji.
Kwa upande wa mashabiki wa muziki wa kizazi kipya wa bongo flava, Linah na Amini walidhibitisha kwa nini wao ni waimbaji bora na wataendelea kuwa hivyo kwa kuonyesha kipaji cha hali ya juu katika kulimiliki jukwaa ambapo waliimba kibao chao kitamu cha ‘Omotima wange ni wewe’.
![]() |
Mpiga tumba wa bendi ya Mashujaa akionyesha Ufundi katika kupiga ngoma wakati wa uzinduzi wa bendi ya Extra Bongo, “Mtenda akitendewa”. |