Dar wanauziwa kambale waliovuliwa kwenye maji-taka?

Gazeti la NIPASHE limechapisha taarifa kuwa wapo baadhi ya vijana wanaouza samaki aina ya kambale wanaovuliwa kutoka kwenye mabwawa ya majit-taka kutoka katika eneo la Vingunguti-Spenco ambako mabwawa ya maji yaliyonyonywa kutoka vyooni na DAWASA humwagwa.

Kwamba, uzio uliojengwa kuzunguka makaro hayo umekatwa ili kutoa upenyo kwa watu kuingia na kuvua samaki hao ambao huwauza katika maeneo yaliyo mbali na makaro hayo.

Mjumbe wa shina la mtaa wa Kombo amekiri kupata taarifa kuhusu kukamatwa kwa vijana wawili wakiwa na samaki waliowavua kutoka kwenye makaro hayo, na kisha wananchi kuwachoma moto samaki hao.

Meneja Mahusiano wa DAWASCO, Irene Makene aliiambia NIPASHE kuwa ofisi yake haijapokea malalamiko kuhusu uvuvi wa samaki kwenye mabwawa hayo na kuomba apewe muda ili afuatilie kwenye ofisi zao nyingine.