Haya! Huko Tanganyika ziwani: Dini yakataza elimu

Na Sylvia Kombe, Kakonko, Kigoma — DINI mpya iitwayo Matengenezo imeingia wilayani Kakonko mkoani Kigoma ambapo waumini wake hawaendi sekondari wala hospitali kwa madai kuwa Biblia inawakataza kufanya hivyo.

Dini hiyo imegundulika juzi katika kijiji cha Rumashi kata ya Nyabibuye wilayani huko wakati Mkuu wa Wilaya hiyo Peter Toima alipokuwa akifanya ziara ya elimu katika shule za sekondari za wilayani hiyo mpya ambapo aligundua wanafunzi wengi kutokuripoti shuleni kwa ajili ya kuanza kidato cha kwanza.

Toima alipohoji kulikoni idadi kubwa ya wanafunzi kutoripoti katika shule walizapangiwa huku wale walioandikishwa darasa la kwanza pia nao kutokuripoti alielezwa kuwa wengine ni sababu za kiimani zinazowakataza kusoma.

Mkuu huyo wa wilaya alikatiza ziara yake na kuanza msako wa kuwasaka wanafunzi hao ambao hawajaripoti shuleni pamoja na waumini wa dini hiyo ya Matengenezo kwa madai kuwa inawakosesha watoto haki yao ya msingi na kukiuka sheria za nchi kwani ni haki ya kila mtoto kupata elimu.

Katika msako huo ambao alikuwa ameongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo pamoja na watendaji wa Halmashauri wakiwemo Maafisa elimu msingi na Sekondari walifika katika familia ya
Mchungaji wa Kanisa la Matengenezo Medad Laurent (40) ambapo aliwakuta mabinti watatu waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu ila hawajaenda kutokana na kile Mchungaji huyo alichodai kuwa sekondari wanafundisha uongo kinyume na maandiko matakatifu yanavyosema.

“Biblia imeandika kuwa mtu aliumbwa  na mungu lakini shule za sekondari wanafundisha uongo kuwa binadamu alitokana na nyani,na pia wanafundisha dunia imemeguka kutoka kwenye sayari wakati maandiko
yanasema Mungu aliumba dunia tena kwa kutamka tu na dunia haizunguki ila jua ndiyo linazunguka na siku huanza jioni saa kumi na mbili na siyo saa sita usiku kama wanavyofundisha”
Alisema mchungaji huyo.

Aidha kufuatia hali hiyo Mkuu wa wilaya hiyo aliamuru Mchungaji huyo pamoja na mabinti zake wawili kushikiliwa na jeshi la Polisi wilayani humo huku utaratibu wa kuwapeleka mabinti hao shule ukiendelea na mchungaji huyo kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za elimu.

“Hatukubaliani na imani hiyo ambayo inavuruga jamii,hatuwezi kuwaacha watoto wadogo kama hawa wapotelee kwenye imani za ajabu ajabu,nitawapeleka shule leo hii na Diwani, Afisa elimu mshirikiane kuhakikisha watoto hawa wanasoma na muda wote wanakuwa shuleni”
alisema.

Siku iliyofuata Toima na kamati ya ulinzi na usalama walifanya kikao na kukubaliana kuwapeleka mabinti hao Naomi Medard(16) na Anastazia Medard(14) katika shule za sekondari zenye mabweni kwa kuwatenganisha ili wasiendelee kuenezeana sumu ya kukataa shule ambapo Naomi alipelekwa shule ya Sekondari Nyamtukuza na Anastazia shule ya sekondari Kanyonza.

Hata hivyo katika familia hiyo binti mmoja Beatrice Merdad (19) alibaki nyumbani kwa madai kuwa hakuchaguliwa kuendelea na kidato cha kwanza na kudai kuwa hata angechaguliwa asingeweza kuendelea kwani wanafundisha uongo na siku akifa hatakuwa na la kwenda kumwambia muumba wake kutokana na elimu hiyo ya dunia kuwapotosha.

Katika familia hiyo ya watoto saba wawili kati yao walifariki dunia kutokana na kutokwenda hospitali na mama wa watoto hao Julitha Sebastian (39) alipohojiwa baada ya mtoto wake mchanga kuonekana kudhoofika na nywele kubadilika rangi alisema kuwa dini yao haiwaruhusu kwenda hospitali na hakuwahi kumpatia motto huyo mchanga chanjo ya aina yeyote wala hakuwahi kujifungulia hospitali na waliokufa biblia inasema “ni heri wafao katika bwana”.
Kwa upande wake kaimu afisa elimu msingi wa wilaya hiyo Jackson Jeremiah alisema kuwa ni lazima wanafunzi hao kwenda shule na kama watajifunza uongo waweze kutumia elimu walioipata kufanya utafiti kugundua kama ni uongo au la badala ya kuendelea kushikilia imani ya ajabu isiyokuwepo.
Jeremiah alisema kuwa watu wanabadilika kutokana na maisha wanayoishi na kazi wanazozifanya na hakuna dini hata moja inayowakataza watu wake kupata elimu na hata maandiko yanasema mshike sana elimu usimwache aondoke zake sasa anashangaa hiyo biblia ya dini hilo la matengenezo ni ya aina gani inayokataa elimu.
Naye Kaimu afisa elimu sekondari Florida Gandye alisema waumini wa kanisa hilo awali walikuwa wakristo wasabato kisha wakajiengua na kuanzisha dini hiyo yenye imani za ajabu na kusisitiza kuwa biblia inasisitiza utii hivyo ni vyema waumini hao kuitii mamlaka iliyopo kwani imewekwa na mungu kwa kuwapeleka watoto wao shule kwa ni ndivyo sheria ya nchi inavyoagiza.

Alisema serikali haitakuwa tayari kuwaona watoto wakikosa haki hiyo kwa sababu zisizo za msingi badala yake watoto hao watapelekwa shule kwa lazima kwa mujibu wa sheria na wazazi hao watashughulikiwa kwa kosa hilo.

Wilaya ya Kakonko ni miongoni mwa wilaya zenye wanafunzi wengi ambao hawajaripoti shule katika mhula huu wa masomo, wanafunzi wa darasa la kwanza walioandikishwa kutokuripoti shuleni pamoja na wanafunzi wengi watoro na wazururaji.
Waumini wa dini hiyo wapatao saba wote wanashikiliwa na jeshi la Polisi wilayani Kakonko kwa kueneza imani inayopotosha huku uchunguzi zaidi ukiendelea.