Halmashauri ya Jiji la Arusha imefanya operesheni ya kubomoa nyumba zaidi ya 210 zinazomilikiwa na Halmahauri hiyo katika maeneo ya Levolosi, Kaloleni, na Themi kwa lengo la kupisha ujenzi wa miradi mbalimbali katika maeneo hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, John Mongella amesema operesheni hiyo imezingatia taratibu zote ikiwa ni pamoja na kutoa notisi miezi kadhaa iliyopita kwa wapangaji wa nyumba hizo kuhama mapema, ili kupisha ubomoaji huo.
“Bahati mbaya sana, wapangaji walikuwa wanataka kusema hoja yao kubwa ni kusema kwamba wao wamekaa humu, wamezaa watoto humu, wamejukuza humu, kwa hiyo wana haki ya hizi nyumba kuwa zao. Ndiyo tofauti yetu ilipokuwa. Sasa mimi nasema, hivi inawezekana ukajenga nyumba, mpangaji ukamwambia kaa humu akaulipa kodi miaka mitano, akishapata wajukuu kesho atasema inageuka kuwa yake? Yaani wewe ukishajukuza kwenye nyumba ya mtu hiyo inakuwa yako?”Alihoji Mhe. Mongella.