Maelezo ya Jaji Warioba: Tafakuri na maridhiano kuelekea Katiba Mpya

MAELEZO YA MWENYEKITI WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA, JAJI JOSEPH SINDE WARIOBA KATIKA MKUTANO WA TANZANIA CENTER FOR DEMOCRACY, KUHUSU TAFAKURI NA MARIDHIANO KUELEKEA KATIBA MPYA: WHITE SANDS HOTEL, DAR ES SALAAM, 12 FEBRUARI, 2014

___________________________________


1.0 UTANGULIZI

Katika nchi yoyote, msingi wa uendeshaji wa nchi unategemea Katiba ambayo ni sheria kuu. Sheria zote hutungwa kwa kuzingatia masharti ya Katiba. Katiba huainisha misingi ya Taifa, mgawanyo wa madaraka na majukumu ya mihimili mikuu ya dola, usimamizi wake, mgawanyo na ukomo wa mamlaka ya vyombo mbalimbali vya dola. Kwa ujumla Katiba ni makubaliano ya wananchi husika kuhusu utaratibu na kanuni za uendeshaji wa mambo mbalimbali katika nchi yao.

Kutokana na maana hiyo ya Katiba, utungaji wake unatakiwa kuwa shirikishi kwa maana ya kuwahusisha wananchi katika hatua zote za mchakato wa kupata Katiba. Kadri mchakato wa kuandika Katiba unavyowashirikisha wananchi kwa mapana, ndivyo kukubalika, kuheshimika na utekelezaji wa Katiba utakavyokuwa rahisi. Wananchi wanaposhiriki katika utungaji wa Katiba, na pale matakwa yao yanapozingatiwa ndani ya Katiba, Wananchi hao huimiliki Katiba hiyo na kuiona kuwa ni Katiba yao. Wananchi huona hivyo kwa sababu licha ya kushiriki lakini pia katiba hiyo huakisi utashi wao na ndoto zao na hivyo kukubali kuongozwa na masharti yaliyomo ndani ya Katiba.

Mchakato wa katiba kwa kadri unavyowashirikisha wananchi, ndivyo unavyowezesha kupatikana kwa mwafaka wa kitaifa kuhusu misingi, malengo na namna serikali na vyombo vyake vitakavyoongoza nchi. Mwafaka huo huzaa katiba ya wananchi ambayo inaimarisha umoja, udugu, ushirikiano na mshikamano katika Taifa kwa maendeleo na ustawi wa jamii.

1.1 Maana na sababu za Mchakato wa Katiba
Mchakato wa Katiba hulenga kupata Katiba Mpya au kufanya marekebisho ya Katiba iliyopo. Michakato mingi ya Katiba hujumuisha Kanuni na hatua kama ifuatavyo:
(a) kukubaliana kuhusu mambo yote yanayohitajika na kupanga malengo;
(b) kukubaliana kuhusu vyombo vya Kusimamia na utaratibu utakaotumika;
(c) kuandaa Wananchi kwa kutoa elimu ya Katiba;
(d) kukusanya Maoni ya Wananchi wa aina zote;
(e) kushauriana na Wataalam;
(f) kujifunza kutokana na Uzoefu wa Nchi mbalimbali;
(g) kuchambua na kutathmini maoni ya Wananchi;
(h) kuandika Toleo la Kwanza la Rasimu ya Katiba;
(i) Wananchi Kujadili Toleo la Kwanza la Rasimu ya Katiba;
(j) Kuchambua na kutathmini maoni ya wananchi kuhusu Toleo la Kwanza la Rasimu ya Katiba;
(k) Bunge Maalum kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba;
(l) Wananchi kuridhia Katiba Iliyopendekezwa na Bunge Maalum kupitia Kura ya Maoni;
(m) kuzindua kutumika kwa Katiba Mpya;
(n) utekelezaji wa Katiba Mpya.
Utekelezaji wa Masuala na hatua zote zilioainishwa hapo juu ndio unatafsiriwa kuwa “Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba.” 
 
Katika mchakato wa Mabadiliko ya Katiba unaoendelea katika nchi yetu, Kanuni na hatua hizi zimeainishwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83.

Msingi wa kuwa na mchakato wa katiba ni kuhakikisha kuwa wananchi wanashiriki katika hatua zote za kupata Katiba na hivyo kuijengea uhalali.

2.0 UTARATIBU WA KUFANYA MABADILIKO YA KATIBA

Katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba, zipo njia kadhaa ambazo hutumika. Njia hizo ni:
(a) Rais kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya katiba;
(b) kuunda Tume ya kuandaa Katiba kupitia sheria zilizopo; au
(c) Bunge kutunga sheria maalum ya mabadiliko ya katiba.

2.1 Rais kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya katiba

Kama ilivyoelezwa hapo juu, mojawapo ya njia za kufanya mabadiliko ya Katiba ni kwa Rais kuanzisha mchakato huo. Katika utaratibu huu, Rais huagiza wataalamu wa kuandika katiba kutayarisha Rasimu ya Katiba. Mara baada ya Rasimu kutayarishwa, Rais humuagiza Waziri kuwasilisha Rasimu hiyo katika chombo cha uwakilishi. Chombo cha uwakilishi hupewa muda maalum wa kujadili na kupitisha Rasimu hiyo bila kujali kuwa maudhui ya Rasimu husika yanaakisi maoni au matakwa ya wananchi. Kimsingi, katiba inayopatikana kwa utaratibu huu hutokana na utashi na matakwa ya Rais au Serikali iliyopo madarakani. Utaratibu huu ndio uliotumiwa na aliyekuwa Rais wa Misri Bw. Morsi na pia unaendelea kutumiwa na Utawala wa kijeshi wa nchi hiyo.

2.2 Kuunda Tume ya kuandaa Katiba kupitia sheria zilizopo

Utaratibu mwingine wa mchakato wa mabadiliko ya katiba hufanywa kupitia Tume inayoundwa kwa mujibu wa sheria zilizopo ambazo ni mahsusi kwa ajili ya kushughulikia masuala mbalimbali katika Nchi. Chini ya utaratibu huu, Rais au Waziri mwenye dhamana ya masuala ya katiba, kwa mamlaka anayopewa na sheria husika huunda Tume au Kamati za kushughulikia mchakato wa mabadiliko ya katiba.

Tume au Kamati inayoundwa hupatiwa hadidu za rejea na muda maalum wa kukamilisha mchakato. Ripoti ambayo itaandikwa kutokana na mchakato uliofanyika, hutumiwa na Serikali kuandaa Rasimu ya Katiba au sheria ya marekebisho ya Katiba. Hata hivyo, licha ya mchakato huu kutowashirikisha wananchi kwa upana na uwazi, Serikali hailazimiki kufanya mabadiliko yoyote ya katiba na inaweza kukalia Ripoti na kupuuza matakwa ya wananchi. 

Aidha, mchakato wa mabadiliko unaofanywa na Tume au Kamati kupitia utaratibu huu huzingatia hadidu za rejea zilizotolewa na Serikali, ambazo wakati mwingine haziakisi, matakwa au madai ya wananchi. Ghana, Uganda Zimbabwe na Zambia ni miongoni mwa nchi zilizowahi kufanya au kujaribu kufanya mabadiliko ya Katiba kwa kutumia utaratibu huu.

2.3 Bunge kutunga sheria maalum ya mabadiliko ya katiba

Utaratibu mwingine wa mchakato wa mabadiliko ya katiba ni wa kutunga sheria mahsusi ya kushughulikia mabadiliko ya katiba. Katika utaratibu huu, sheria inayotungwa hueleza utaratibu wa mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya.

Utaratibu huu ni shirikishi kwani wananchi hushirikishwa kisheria katika hatua zote muhimu za uandikaji wa katiba yao. Chini ya utaratibu huu, hadidu za rejea hutolewa na sheria yenyewe badala ya Rais au Waziri. Aidha, Tume hupewa jukumu la kuratibu, kukusanya maoni ya wananchi, kuyachambua na kutathmini maoni kabla ya kuandaa ripoti na Rasimu ya Katiba. Mara baada ya kuandaa Rasimu ya Katiba, wananchi hupewa tena fursa ya kutoa maoni yao kabla ya Tume au Kamati kuifanyia marekebisho na kuiwasilisha katika Baraza au Bunge Maalum la Katiba.

Baraza au Bunge Maalum huwa na jukumu la msingi la kuijadili na kuipitisha Rasimu ya Katiba. Katika baadhi ya nchi kama vile Afrika Kusini, Ghana na Uganda, mchakato wa Katiba Mpya ulikamilishwa na Bunge Maalum. Baadhi ya nchi pia hazikutumia Bunge Maalum na badala yake, Rasimu ya Katiba ilipigiwa kura ya “Ndio” au “Hapana” baada ya kutoka kwenye Tume au Kamati. Kwetu Tanzania, Sheria inayosimamia mchakato wa mabadiliko ya Katiba imeainisha hatua zote tatu ambazo ni Tume kuandaa Rasimu ya Katiba, Bunge Maalum kujadili Rasimu ya Katiba na kupitisha Katiba ambayo itapendekezwa kwa wananchi ili kuipigia kura ya maoni.

3.0 MCHAKATO WA MABADILIKO YA KATIBA TANZANIA
Mwaka 2011, Taifa la Tanzania lilianzisha mchakato wa mabadiliko ya katiba. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Bunge lilitunga sheria mahsusi ya kusimamia mchakato wa mabadiliko ya katiba. Sheria hiyo inayoitwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 imeweka masharti kuhusu usimamizi na uendeshaji wa mchakato wa mabadiliko ya katiba. Sheria hii imempatia mamlaka Rais kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar.

Katika kutekeleza matakwa hayo, Sheria ilimtaka Rais kualika Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu, Jumuiya za Kidini, Asasi za Kiraia, Jumuiya na Taasisi zisizo za Kiserikali na Makundi ya Watu wenye Malengo Yanayofanana kupendekeza majina ya watu wanaoweza kuteuliwa kuwa Wajumbe wa Tume.

Sheria hiyo imeainisha utaratibu wa utendaji kazi wa Tume na Hadidu za Rejea ambazo ni:
(a) kuratibu na kukusanya maoni ya Wananchi;
(b) kupitia na kutafiti usahihi na ulinganifu wa masharti ya kikatiba yanayohusu mamlaka ya wananchi, mifumo ya kisiasa, demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora;
(c) kutoa mapendekezo kwa kila Hadidu ya Rejea; na
(d) kuandaa na kuwasilisha Ripoti pamoja na Rasimu ya Katiba kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Sheria hiyo pia, inaainisha Misingi ya Kitaifa na Maadili ambayo yanapaswa kuzingatiwa na Tume katika mchakato wa kupatikana Katiba Mpya. Misingi hiyo ni:
(a) kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano;
(b) uwepo wa Serikali, Bunge na Mahakama;
(c) mfumo wa kiutawala wa kijamhuri;
(d) uwepo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
(e) umoja wa kitaifa, amani na utulivu;
(f) uchaguzi wa kidemokrasia na wa mara kwa mara katika vipindi maalum kwa kuzingatia haki ya watu wote wenye sifa ya kupiga kura;
(g) ukuzaji na uhifadhi wa Haki za Binadamu;
(h) utu, usawa mbele ya sheria na mwenendo wa sheria; na
(i) uwepo wa Jamhuri ya Muungano isiyofungamana na dini yoyote na inayoheshimu uhuru wa kuabudu.

Kwa ujumla, Sheria inaainisha kazi na majukumu ya Tume kuwa ni:
(a) kuandaa na kuendesha programu za elimu kwa umma juu ya madhumuni na majukumu ya Tume;
(b) kuitisha na kusimamia mikutano au Mabaraza ya Katiba katika sehemu na nyakati mbalimbali kama itakavyoamua;
(c) kutathmini na kuchambua maoni ya wananchi yanayokubaliana na yale yasiyokubaliana; na
(d) kutayarisha na kuwasilisha Ripoti kwa kuzingatia Hadidu za Rejea.

Katika kutekeleza kazi na majukumu yake, Tume imepewa mamlaka ya:
(a) kumtaka mtu yeyote, atakayehiari, kwenda mbele yake na kufanya naye majadiliano kwa mazungumzo au kuwasilisha nyaraka;
(b) kupitia na kufanya uchambuzi wa michango, mawazo, maoni, taarifa na mapendekezo yaliyotolewa na kufanyiwa tathmini siku za nyuma, kupitia nyaraka mbalimbali zilizoainishwa katika Sheria hiyo, na nyingine zozote ambazo Tume itaona zinafaa;
(c) kumtaka Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Afisa Mtendaji wa Kata au Afisa Mtendaji wa Kijiji kuitisha mkutano wa Wakazi wa Mji, Kata, Mtaa au Kijiji kwa Tanzania Bara;
(d) kumtaka Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Manispaa, Katibu wa Halmashauri ya Mji au Wilaya, au Sheha kuitisha mkutano wa Wakazi wa Mji au Shehia, kwa upande wa Zanzibar;
(e) kuunda Kamati kwa ajili ya kazi za jumla au maalum;
(f) kumtumia au kumshirikisha mtaalamu mwelekezi au mtu yeyote kadri itakavyokuwa lazima; na
(g) isipokuwa kama mazingira yatahitaji vinginevyo, kutumia utaratibu unaofanana wa ukusanyaji na uchambuzi wa maoni ya wananchi, uendeshaji wa Mabaraza ya Katiba na uandaaji wa Ripoti.
Sheria pia imeainisha kuwepo kwa Bunge Maalum la Katiba na Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Aidha, utaratibu wa kuwapata Viongozi na Sekretarieti ya Bunge Maalum la Katiba umeainishwa katika Sheria hii. Sheria pia imeainisha utaratibu wa Bunge Maalum kuandaa na kupitisha Kanuni za Bunge Maalum la Katiba na Utaratibu wa Majadiliano ya kupitisha Rasimu ya Katiba itakayopendekezwa kwa Wananchi ili kuipigia kura ya maoni. Katiba itapitishwa kwa kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wajumbe kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wajumbe kutoka Zanzibar. Utaratibu wa kura ya maoni na Uzinduzi wa Katiba mpya pia umeainishwa.
Kwa kifupi, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, ni Katiba au Msahafu wa Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba unaoendelea hivi sasa. Sheria imeunda vyombo vyote muhimu na kila chombo kimepewa hadidu za rejea. Kila chombo kimewekewa utaratibu wa kazi na madaraka yake. Katika utaratibu huu kila chombo kina madaraka yake yaliyowekewa mipaka. Haiyamkini kwa Tume kukusanya maoni, kuandika Rasimu ya Katiba, kuiwasilisha katika Bunge Maalum la Katiba kisha nayo ishiriki kuijadili Rasimu ya Katiba. Au, Bunge Maalum la Katiba, lenye madaraka ya kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba wakati huo huo kuandika Rasimu ya Katiba mbadala au kubadili mfumo wa Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume. Hivyo hivyo, kwa Tume ya Uchaguzi na Wananchi. Kila aliyetajwa, ikiwa ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar, ana jukumu maalum lililoainishwa na Sheria.

4.0 WAPI TULIPO HIVI SASA
Kufuatia Tume kukabidhi Ripoti na viambatanisho vyake kwa Marais, kama Sheria inavyoelekeza Rais amekwishachapisha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika Gazeti la Serikali na vyombo vingine vya habari, amekwishateua Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba na kuliitisha Bunge Maalum la Katiba ili kukutana kuanzia tarehe 18 Februari, 2014, Dodoma. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba atawasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalum. Bunge hilo litakuwa na wajibu wa kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba kabla ya kupigiwa kura ya maoni na wananchi.

5.0 BUNGE MAALUM NA MAJUKUMU YAKE
Bunge Maalum la Katiba ni chombo cha uwakilishi kama lilivyo Bunge la kawaida isipokuwa Bunge Maalum la Katiba huundwa kwa ajili tu ya kutunga Katiba na kufanya shughuli zingine zinazoambata na utungaji wa Katiba. Bunge Maalum la Katiba hupewa jukumu hili la kutunga katiba badala ya Bunge la kawaida kwa sababu Bunge Maalum la Katiba linawakilisha wananchi ambao ndio msingi wa mamlaka ya nchi na vyombo vyake vyote ikiwemo Bunge la kawaida ambalo pia ni zao la Katiba.

Majukumu ya Bunge la Maalum la Katiba yanaweza kutofautina kulingana na namna utaratibu mzima wa mchakato wa mabadiliko ya katiba ulivyopangwa. Katika baadhi ya nchi, Bunge Maalum la Katiba hupewa mamlaka ya kusimamia mchakato wote wa mabadiliko ya katiba, wakati katika nchi nyingine Bunge hili hushirikiana na vyombo vingine katika kufanya na kusimamia mchakato wa mabadiliko ya katiba.

5.1 Madaraka ya Bunge Maalum
Madaraka ya Bunge Maalum yamekuwa yanabadilika kwa kutegemea aina ya mchakato unaotumika. Afrika kusini, Namibia na Cambodia Bunge Maalum lenyewe ndilo lilipewa jukumu la kuandika Rasimu ya Katiba. Katika mazingira haya, Bunge Maalum lilikuwa na madaraka ya kubadilisha mambo mengi katika Rasimu ya Katiba. Bunge Maalum lilikuwa na madaraka ya kuachana na Rasimu ya Katiba na kuandika Rasimu Mbadala.

Madaraka ya Bunge Maalum yanakuwa na mipaka endapo Rasimu ya Katiba imeandaliwa na Tume ya Maadiliko ya Katiba au Chombo cha aina hiyo. Bunge Maalum linaweza kuwa huru kurekebisha baadhi ya masharti yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba lakini si suala la kawaida Bunge Maalum kubadili hoja ya msingi. Jinsi ushirikishaji wa Wananchi unavyokuwa wa wazi na mpana ndivyo madaraka ya Bunge Maalum yanavyopungua. Mantiki ni kuzuia Bunge Maalum kunyang’anya madaraka ya Wananchi, yaani “act of popular sovereignty”. Wataalam wa masuala ya Katiba, wanaeleza kuwa madaraka ya Bunge Maalum katika mazingira haya ni kuboresha Rasimu ya Katiba.

Kwa mujibu wa kifungu cha 25(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, Bunge Maalum limepewa madaraka ya kujadili na kupitisha masharti ya Katiba, kutunga Sheria ya Masharti ya Mpito na Masharti yatokanayo na kabla ya kuanza kazi hiyo, Bunge Maalum litapitisha Kanuni za Bunge Maalum ambazo zitaongoza utekelezaji wa mamlaka ya Bunge Maalum.

5.2 Kanuni za Bunge Maalum
Kanuni za Bunge Maalum la Katiba sharti zizingatie kwamba Bunge Maalum, kwa mujibu wa madaraka liliyopewa chini ya kifungu cha 25(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, ni chombo cha kuboresha masharti ya Rasimu ya Katiba.

Katika kutekeleza madaraka ya kujadili na kupitisha masharti ya kikatiba, Bunge Maalum litazingatia msingi kwamba masharti ya kikatiba ndani ya Rasimu ya Katiba ni taswira, dira na ndoto za Wananchi ambazo zimeelezwa kupitia maoni ya mwananchi mmoja mmoja na makundi ya wananchi kupitia asasi, taasisi, jumuiya na makundi ya Watu Wenye Malengo Yanayofanana.

Bunge Maalum litafanya kazi ya kuboresha masharti ya Kikatiba yaliyomo ndani ya Rasimu ya Katiba pasipo kuweka masharti mapya ambayo kwa taathira yake yanabadilisha au kufifisha masharti ya kikatiba yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba.

6.0 MUUNDO WA MUUNGANO WA SERIKALI TATU
Muundo wa Muungano umewekwa katika Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba. Ili kupata maana kamili ya muundo wa Muungano unaopendekezwa, Tume ni vema kusoma Sura ya Kwanza, Sura ya Nane na Sura ya Kumi na tano.

Taswira ya Muungano wa Serikali Tatu unaopendekezwa katika Rasimu ya Katiba imejengwa katika Ibara ya 1 inayoieleza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni nchi na shirikisho lenye mamlaka kamili – Sovereign Federal Republic. Kwa hali hiyo Muungano wa Serikali Tatu haubadili hadhi ya Jamhuri ya Muungano katika jumuiya ya kimataifa kuwa ni nchi moja. Kupendekezwa kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika haina maana ya kuunda nchi mpya. Kinachopendekezwa ni kutenganisha mamlaka ya Mambo ya Muungano na Mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika. Tanganyika na Zanzibar hazina hadhi ya Jamhuri, na kwa hiyo si “Sovereign States” kama ilivyo Jamhuri ya Muungano.

6.1 Misingi ya Muundo wa Muungano wa Serikali Tatu
Muungano wa Serikali Tatu unaopendekezwa umezingatia mamlaka tatu zilizomo ndani ya Jamhuri ya Muungano hivi sasa:
(a) Mamlaka ya Mambo ya Muungano –Jurisdiction on Union Matters yanayosimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Ibara ya 4(2), (3) na 34(1) na (3) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977;
(b) Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Zanzibar yanayosimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kupitia Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na kwa mujibu wa Ibara ya 4(2) na (3), 64(2) na (5) na Ibara ya 102 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; na
(c) Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika ambayo kwa sasa yanasimamiwa na Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya sasa - Ibara ya 4, 34(2) na (3) na 64 (4).
Kila mamlaka sasa itakuwa na Serikali yake ambayo itasimamiwa na Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano.

6.2 Mgawanyo wa majukumu na madaraka katika Serikali tatu
Ibara ya 60 na Nyongeza ya Kwanza inaorodhesha mambo saba ya Muungano ambayo yanasimamiwa na Jamhuri ya Muungano. Haya ndiyo masuala makuu na ya msingi ya kidola (Sovereign Functions) ambayo ndiyo yalivyo katika masuala 11 ya Muungano yaliyomo katika Hati ya Muungano ya Mwaka 1964.

Katika mambo haya saba, Jamhuri ya Muungano inayo mamlaka kamili tena yasiyogawanyika. Mambo hayo 7 hayawezi kufanywa na Serikali za Nchi Washirika wa Muungano kwa sababu hazina sifa ya “Sovereign States”. Kwa mfano suala la ulinzi na usalama lipo moja kwa moja katika Jamhuri ya Muungano. Pamoja na orodha ya mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza, zipo taasisi ambazo zimetajwa katika Rasimu ya Katiba kuwa za Muungano lakini hazijaorodheshwa. Taasisi hizo na mambo hayo yamejumuishwa katika Mambo ya Muungano Yaliyokusudiwa katika aya ya 1 ya Mambo ya Muungano, yaani – Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano.

6.3 Hadhi ya Marais wanaotajwa katika Rasimu ya Katiba
Katika Rasimu ya Katiba yumo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar. Ingawa wote wanaitwa Rais, lakini hawafanani kwa hadhi na majukumu. Rais mwenye mamlaka juu ya Jamhuri ya Muungano ni Rais wa Jamhuri ya Muungano. Kwa hiyo, kwa mujibu wa Rasimu ya Katiba, Rais wa Jamhuri ya Muungano ndiye peke yake Mkuu wa Nchi mwenye mamlaka kamili (Head of State), Amiri Jeshi Mkuu na Mkuu wa Serikali ya Muungano. Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar hawana sifa hizo ingawa wao ni wakuu wa mambo yote yasiyo ya Muungano katika maeneo yao ya utawala. Kwa kuhakikisha hilo, Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar hawakupewa hadhi ya Makamu wa Rais kwa makusudi. Kwa msingi huo hawawezi kukaimu nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano akisafiri au akiwa hawezi kutekeleza kazi kwa muda. Hilo likitokea wanaweza kukaimu ni Makamu wa Rais, Waziri Mwandamizi, n.k.

6.4 Misingi ya utendaji ya Muungano wa Serikali Tatu
Muundo wa Serikali Tatu umejengwa katika Misingi ya Utendaji (Principles) ifuatayo:
(a) Muungano wa Hiari (Voluntary Union);
(b) ushirikiano ( Co-operation);
(c) uratibu (Co-ordination);
(d) Mshikamano (Solidarity); na
(e) subsidiarity.

6.4.1 Muungano wa Hiari (Voluntary Union)
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Muungano wa iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Msingi wa Muungano huu ni Makubaliano ya Muungano (Articles of Union) ya mwaka 1964 yaliyofikiwa baina ya mataifa haya mawili. Chini ya makubaliano hayo, mataifa hayo yalikubaliana kwa hiari kuachia baadhi ya mamlaka na kuyapeleka mamlaka hayo katika Serikali ya Muungano. Uhiari huu wa kukubali kuungana kwa mataifa haya mawili ni moja ya misingi ya utekelezaji wa muundo wa Muungano unaopendekezwa wa Serikali Tatu. Ibara ya 1(3) ya Rasimu ya Katiba inapendekeza pamoja na mambo mengine, Hati ya Muungano iwe ni msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

6.4.2 Ushirikiano (Co-operation)
Msingi mwingine wa utendaji katika muundo wa Serikali Tatu ni Ushirikiano. Chini ya msingi huu, Serikali ya Muungano na Serikali za Nchi Washirika zitakuwa na ushirikiano baina yao katika shughuli zote za utendaji na uendeshaji wa nchi ili mradi ushirikiano huo haukiuki Katiba. Ibara ya 65(1) inapendekeza kuwa Nchi Mshirika iweze kuomba ushirikiano kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kufanikisha uhusiano wake wa kikanda au kimataifa. Aidha, Ibara ya 66 inapendekeza masharti kuhusu ushirikiano kati ya Nchi Washirika zenyewe na baina ya Nchi hizo na Serikali ya Muungano kwa lengo la kukuza na kulinda maslahi ya Taifa na kukuza maendeleo ya wananchi.

6.4.3 Uratibu (Coordination)
Katika mfumo wa Serikali Tatu, uratibu wa uhusiano baina ya Serikali hizo ni moja ya misingi muhimu. Ibara ya 67 inapendekeza kuwepo kwa Waziri Mkaazi atakayeteuliwa na kila Nchi Mshirika atakayefanya kazi akiwa Makao Makuu ya Serikali ya Muungano. Moja ya majukumu ya msingi ya Waziri Mkaazi ni kuratibu uhusiano baina ya Serikali yake na Serikali nyingine ya Nchi Mshirika na kati ya Serikali yake na Serikali ya Muungano. Aidha, Ibara ya 109 inapendekeza kuanzishwa kwa Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali chini ya uenyekiti wa Makamu wa Rais. Kuwepo kwa uratibu kutaimarisha uhusiano wa kiutendaji baina ya Serikali zinazopendekezwa na hivyo kuimarisha Muungano.

6.4.4 Mshikamano (Solidarity)
Mshikamano (Solidarity) ni moja ya misingi muhimu ya utendaji katika mfumo wa Shirikisho. Msingi huu umezingatiwa katika Rasimu inayopendekezwa ili kuhakikisha kuwa Serikali zote tatu zinashikamana na kusaidiana katika kila hali inayoweza kujitokeza. Mathalani, Ibara ya 62(3) inapendekeza kuipa Serikali ya Muungano, kwa makubalino na masharti maalum na Serikali ya Nchi Mshirika, madaraka ya kutekeleza jambo lolote lililo chini ya mamlaka ya Serikali ya Nchi Mshirika. Aidha, Ibara ya 65 na 66 zinapendekeza kuwepo kwa ushirikiano baina ya Serikali za Nchi washirika na kati ya Serikali hizo na Serikali ya Muungano. Msingi huu ni muhimu katika kuhakikisha kuwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano wananufaika kwa usawa na mshikamano baina ya Nchi Washirika.

6.4.5 Subsidiarity
Msingi wa subsidiarity unakusudia kuweka utaratibu wa mamlaka za chini kutekeleza majukumu yaliyo ndani ya uwezo wake ikiwa mamlaka hizo zina uwezo wa kutekeleza majukumu hayo kwa ukamilifu. Msingi huu wa subsidiarity unaruhusu mamlaka ya juu kutekeleza jambo ambalo kwa kawaida hutekelezwa na mamlaka ya chini iwapo mamlaka ya juu ina uwezo wa kutekeleza jambo husika kwa ufanisi au vinginevyo. Ibara ya 65 na 66 zimeweka msingi kwamba, ingawa Serikali ya Muungano itakuwa na mamlaka ya kushughulikia Mambo ya Muungano, Serikali hiyo, kwa ridhaa ya Serikali ya Nchi Mshirika, itakuwa na mamlaka ya kushughulikia masuala yasiyo ya Muungano katika Nchi Mshirika. Msingi huu utasaidia kuimarisha utendaji katika muundo wa Serikali Tatu unaopendekezwa.

6.5 Vyombo vya kikatiba vinapendekezwa kusimamia Misingi ya Utendaji
Katika kuhakikisha kuwa Muungano unaimarika, Vyombo vipya vya kikatiba vimependekezwa kusimamia Misingi ya Utendaji. Vyombo hivyo ni:
(a) Tume ya Uratibu na Uhusiano wa Serikali;
(b) Mawaziri Wakaazi;
(c) Mahakama ya Juu;
(d) Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa.

6.5.1 Tume ya Uratibu na Uhusiano wa Serikali
Tume ya Uratibu na Uhusiano wa Serikali inaanzishwa na Ibara ya 109 na Makamu wa Rais atakuwa ndiye Mwenyekiti wa Tume hii, na wajumbe wake watakuwa ni Rais wa Tanganyika, Rais wa Zanzibar, Mawaziri Wakaazi na Waziri mwenye dhamana ya mambo ya nje wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Tume hii, pamoja na mambo mengine, itakuwa na dhima ya kusimamia na kuratibu uhusiano baina ya Serikali za Nchi Washirika na baina ya Serikali hizo na Serikali ya Muungano. Tume hii ambayo inapendekezwa kuwa na Sekretarieti ya wataalam wa fani mbalimbali, itakuwa pia na jukumu la kuwezesha uratibu na ushirikiano katika kutekeleza masharti yanayopendekezwa na Rasimu ya Katiba, sera, sheria, mipango na mikakati baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali za Nchi Washirika na baina ya Serikali hizo.

6.5.2 Mawaziri Wakaazi
Waziri Mkaazi ni nafasi ya madaraka inayopendekezwa na Ibara ya 67. Waziri Mkaazi atakuwa na wajibu wa kuratibu na kusimamia uhusiano baina ya Serikali yake na Serikali nyingine ya Nchi Mshirika na kati ya Serikali yake na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

6.5.3 Mahakama ya Juu
Mahakama ya Juu ni chombo kingine kinachopendekezwa kuanzishwa katika Rasimu inayopendekezwa. Mahakama ya Juu, pamoja na mambo mengine, inapendekezwa kuwa na mamlaka ya kushughulikia kusikiliza na kuamua migogoro baina ya Nchi Washirika au baina ya Nchi Mshirika na Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Mamlaka haya ya Mahakama ya Juu yanakusudia kusimamia misingi ya utendaji katika muundo wa Muungano unaopendekezwa

6.5.4 Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa.
Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa linapendekezwa kuanzishwa na Ibara ya 237 ya Rasimu inayopendekezwa. Baadhi ya Wajumbe wa Baraza hilo litaloongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ni Makamu wa Rais, Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar. Baraza hili litakuwa ndicho chombo pekee kitakachowakutanisha Wakuu wa Serikali Tatu zinazopendekezwa na kitakuwa chombo cha juu cha kusimamia misingi ya utendaji katika muundo wa Serikali unaopendekezwa.

_________________