Malinzi akabidhi kombe bingwa michuano shule za Sekondari Dar

Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Dionizi Malinzi (wapili kulia) akikabidhi kombe kwa kapteni wa timu ya sekondari ya Mugabe Laurian Didas baada yakuibuka mabingwa katika michuano maalumu ya Community Sports Cup ambapo walishinda jumla ya bao 1-0 dhidi ya shule ya sekondari ya Kawe, (wa pili kutoka kushoto) ni Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Tanzania, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Leonard Tadeo, Katibu Mkuu wa BMT Henri Lihaya (wakwanza kutoka kulia). Michuano hiyo imemalizika rasmi kwa udhamini wa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania.

Dar es Salaam, Februari 23, 2014 -- Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania, Dionizi Malinzi amekabidhi kikombe kwa mshindi wa michuano maalum ya shule za sekondari iliyopewa jina la ‘community sports cup’ timu za shule ya Mugabe katika mchezo uliowakutanisha na Kawe Kwamani katika uwanja wa shule ya sekondari ya Turiani wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi kwa washindi Bw. Malinzi amepongeza jitihada za dhati zilizoonyeshwa na kampuni ya mawasiliano ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania kwa kushirikiana na wizara ya habari, vijana, utamaduni na michezo pamoja na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) katika kufufua michezo mashuleni.

“Kwanza niwapongeze sana waandaaji wa mashindano haya kwani tumekuwa tukilizungumza suala la michezo mashuleni kila kukicha bila ya kulitimiza kwa vitendo. Kwa kweli naweza kusema mmethubutu na mmeweza, mpaka leo hii fainali imechezeka na kumpata mshindi ni jititihada kubwa mmefanya.” Alisema Malinzi.

Malinzi aliongezea kuwa kitu kilichofanyika mwaka huu kimetoa mwanga kwa wadau mbali mbali wa michezo nchini kuwa hakuna kisichowezekana kama tukiunganisha nguvu zetu kwa pamoja. Amesema kuwa anaamini mashuleni ndio kuna vipaji vingi na vitazaa matunda kama vikiendelezwa vema.

“Nchi yetu haijafikia katika viwango vya kuwa na shuleni maalum za mpira wa miguu au ‘academy’ kama zinavyofahamika kwa lugha ya kigeni lakini kwa mashindano hayo tunaweza kupata vijana wenye uwezo mkubwa tukawakusanya kwa pamoja tukawapa mafunzo kisha wakatusaidia katika timu yetu ya taifa au hata wakasajiliwa katika vilabu vikubwa ndani na nje ya nchi. Nawaomba wadhamini wetu Vodacom wajitahidi kuwapatia vifaa timu hizi za shule ili kusaidia kufikia sehemu nzuri.” Alimalizia Malinzi

Naye Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Tanzania, Salum Mwalim amebainisha kuwa wao wamekuwa ni wadau wakubwa wa michezo nchini na wanafanya kila jitihada kuona serikali na watanzania wanafikia viwango vya kimataifa katika michezo.

“Michezo mashuleni imekuwa ni suala la kusuasua sana hivyo basi tunajaribu kuhakikisha mashindano hayo yafikie ngazi ya kitaifa na si kimkoa kama tulivyofanya mwaka huu.” Alisema Mwalim

“Ni mafanikio makubwa tumeyapata kwa hizi shule chache tulizoanza nazo na hii inatupa sisi nguvu ya kuyaboresha zaidi mashindano haya mwakani. Wito wangu ni kwa vilabu vyetu nchini kuviangazia vipaji tulivyoviona katika mashindano haya kwa kuviendeleza na sio kuishia leo ambapo tumefikia tamati ya mechi hizi, pia nawaomba wadau mbali mbali wa michezo kuunganisha nguvu zetu pamoja kuisadia serikali kuiinua hii sekta nchini.” Alimalizia Mwalim

Mugabe ndiye aliyeibuka bingwa wa michuano hiyo kupitia bao pekee lililopatikana kwa njia ya penati iliyowekwa kimyani na Lauriani Didas. Washindi hao walikabidhiwa kombe lao pamoja na mipira miwili.

Mshindi wa pili wa michuano hiyo alikuwa ni shule ya sekondari Kawe Kwamani ambayo alikabidhiwa kombe la saizi ya kati pamoja na mipira miwili.

Mbali na zawadi kwa mabingwa hao wa mara ya kwanza wa mashindano hayo pia kulikuwa na zawadi kwa mchezaji bora wa michuano hiyo ambaye alikuwa ni nahodah wa timu ya Kawe, Komanje Komanje na mlinda mlango bora ambaye ni Shabani kutoka timu ya Mugabe, kila mmoja alipatiwa mpira mmoja.

Mashindano hayo yamezikutanisha shule kumi na mbili za sekondari za mkoa wa Dar es Salaam kutoka wilaya zake tatu; kwa wilaya ya Kinondoni shule zitakazoshiriki ni Turiani, Mugabe, Kawe na Kiluvya; Ilala ni Benjamini William Mkapa, Mnazi Mmoja, Majani ya Chai na Juhudi; Temeke ni Kibasila, Temeke, Pendamoyo na Mtoni Relini.

Michuano hiyo ilianza kutimua vumbi kuanzia Februari 8 na kuhitimishwa siku ya tarehe 23 ya mwezi huu. Viwanja viilivyotumiwa ni vitatu yaani kimoja kutoka kila wailaya ambavyo ni Kibasila (Temeke), Benjamini Mkapa (Ilala) na Turiani (Kinondoni).

Mashabiki wa timu ya sekondari ya Mugabe wakishangilia baada yakuibuka mabingwa wa michuano maaalum ya Communnity Sports Cup baada ya kuichapa timu ya sekondari ya Kawe bao 1-0 katika fainali zilizopigwa kiwanja cha Turiani Sekondari. Michuano hiyo imemalizika rasmi kwa udhamini wa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania.

Meneja wa Uhusiano wa nje wa Vodacom Tanzania Salum Mwalim (aliyevaa flana nyekundu) akiwa kwenye picha ya pamoja na timu ya Sekondari ya Mugabe kabla ya fainali hiyo ya mashindano maalum ya Community Sports Cup kuanza katika kiwanja cha Turiani Sekondari. Mashindano hayo yamewezeshwa na kudhaminiwa na kampuni ya Vodacom Tanzania.

Meneja wa Uhusiano wa nje wa Vodacom Tanzania Salum Mwalim (aliyevaa flana nyekundu) akiwa kwenye picha ya pamoja na timu ya Sekondari ya Kawe kabla ya fainali hiyo ya mashindano maalum ya Community Sports Cup kuanza katika kiwanja cha Turiani Sekondari. Mashindano hayo yamewezeshwa na kudhaminiwa na kampuni ya Vodacom Tanzania.