Mama aliyejifungua quadruplets apokea msaada kutoka Uingereza

Aida Nakawala na quadruplets wake

Aida Nakawala (25) mkazi wa kijiji cha Chiwanda, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Mbeya, hivi karibuni alijifungua watoto wanne mapacha kwa mkupuo (quadruplets) katika usiku wa kuamkia mwaka mpya 2014 anaendelea vizuri.

Mwanamke huyo ambaye kwa hivi sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wazazi ya Meta akiwa na watoto wake wote wanne alijifungua majira ya saa 10 alfajiri usiku wa kuamkia Januari Mosi Mwaka huu katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi na watoto wakiwa na uzito wa kawaida tofauti na matarajio ya Wengi.

Misaada ya hali na mali imeanza kumiminika.

Msamaria mwema wa Uingereza, Bi. Gladness Sariah, ametuma maboksi mawili yenye nguo na vitu kadhaa vya watoto, ambavyo vimewasili salama katika ofisi za Michuzi Media Group (MMG) inayoendesha Globu ya Jamii jijini Dar es salaam baada ya kusafirishwa bure na Wazee wa Kazi, Serengeti Freight Forwarders ya huko Uingereza. 

Misaada kwaajili ya Aida Nakawala mara baada ya kufikishwa katika makao makuu ya Globu ya Jamii jijini Dar es Salaam baada ya kusafirishwa bure toka Uingereza na Wazee wa Kazi, Serengeti Freight.



Hivi sasa MMG ikishirikiana na waratibu wa misaada kwa mama huyo, Mbeya Yetu Blog, wanaandaa utaratibu wa kumfikishia Mama Aida mizigo yake haraka iwezekanavyo.

Kwa niaba ya mzazi wa mapacha hao, Michuzi Blog na Mbeya Blog zinatoa shukrani za dhati kwa msamaria mwema Gladness Sariah kwa wema na upendo aliouelekeza kwa mzazi huyo. Huo ni mfano wa kuigwa, na tunatarajia misaada zaidi itatolewa na wasamaria wema ambao tunajua mko wengi kila kona ya dunia.

Kama umeguswa na hili na unataka kutoa msaada tafadhali wasiliana na: [email protected] ama [email protected] nasi tutafikisha ubani wako.

Serengeti Freight wametoa ofa ya kusafirisha bure misaada ya aina hii

ASANTENI SANA

Michuzi Blog/Mbeya Yetu Blog