Maoni ya Mnyika kuhusu matokeo ya Mtihani Kidato cha Nne 2013

Maoni yangu kuhusu matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne wa mwaka 2013 yaliyotangazwa na kuelezwa kuwa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 15.17 yamedhihirisha tahadhari niliyotoa kuhusu mabadiliko ya viwango vya ufaulu yaliyotangazwa na Serikali tarehe 30 Oktoba 2013.

Serikali kwa barakoa (veil) ya kutekeleza Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) imeamua kulificha taifa juu ya Matokeo Mabaya ya Sasa (Bad Results of Now). Hivyo, wachambuzi wa masuala ya elimu wanapaswa kutoa takwimu za matokeo yangekuwa namna gani iwapo viwango vya awali vya ufaulu vingetumika ili
nchi ijue hali halisi kwa manufaa ya wananchi.

Aidha, natoa mwito kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuweka wazi kwa umma ripoti za uchunguzi zilizoundwa kuwezesha wananchi kuihoji Serikali iwapo kupanda huko kwa ufaulu ni matokeo ya kuboresha mazingira ya kufundisha na
kujifunza au ni kiini macho cha mabadiliko ya wigo wa alama na madaraja?

Ukweli ni kuwa hali ya mazingira ya kujifunza na kujifunzia katika shule nyingi za msingi na sekondari hasa za umma sio nzuri kutokana na kutokuwa na vitabu vya kutosha, maabara za kutosha, waalimu wenye sifa wapo wa kutosha na kuboresha maslahi ya waalimu ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kwa siku nyingi.

Ikumbukwe kwamba miaka mitatu mfululizo, mfumo wa elimu wa Tanzania, na hususani kwa upande elimu ya msingi na sekondari umekuwa ukiporomoka kwa kasi ya ajabu. Kufuatia kuporomoka huko, na hasa kushuka kwa viwango vya
ufaulu, Serikali kwa vipindi totauti (mwaka 2010 na 2012) imeund Tume kuchunguza sababu za kushuka kwa viwango vya ufaulu.

Ingawa ripoti za tume zilizoundwa kuchunguza sababu za kushuka kwa ufaulu hazijulikani kwa wananchi ambao ni wadau wakuu wa elimu, Serikali imeendelea kutoa maagizo na matamko mbalimbali kuhusu viwango vya ufaulu.

Ikumbukwe kuwa mwezi Mei, 2013 Serikali ilitangaza kufutwa kwa matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012 kutokana na kushuka mno kwa viwango vya ufaulu ambapo zaidi ya asilimia 65 ya wanafunzi walipata daraja sifuri na kuamuru
matokeo hayo kupangwa upya.

Takribani miezi sita baadaye, yaani 30 Oktoba 2013 Serikali ilitangaza kubadili viwango vya ufaulu bila kutoa ufafanuzi kuhusu msingi wa mabadiliko hayo na kuwasilisha bungeni ripoti za kamati/timu zilizochunguza kuporomoka kwa ufaulu.

Hivyo hata baada ya kauli ya Serikali kuwa "kundi la watahimiwa walioshindwa Mtihani na ambalo awali lilikuwa likiandikwa kama 'failures' litaendelea kujulikana kama Daraja Sifuri (Zero) bado Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inapaswa kutoa ufafanuzi juu ya athari za mabadiliko hayo kuwezesha Bunge kusimamia Serikali ipasavyo.

Pamoja na mpango wa Serikali wa kuficha matokeo mabaya ya kidato cha nne ya mwaka 2013 bado idadi ya waliofeli imeendelea kuwa kubwa kwa kuwa watahiniwa 151,187 sawa na asilimia 42.91 wamepata sifuri. Kati ya hao, wavulana ni 78,950 sawa na asilimia 41.54 na wasichana ni 72,237 sawa na asilimia 44.51. Aidha, katika matokeo hayo hali ya watahiniwa kutokuweza kufanya mtihani kabisa kwa kiwango cha kuacha karatasi tupu, kuchora vitu vya ajabu au kuandika matusi inadhihirisha udhaifu mkubwa uliopo katika mfumo wetu wa elimu kwa kuwa wahusika wameweza kupanda kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne wakiwa hawana uwezo wa kufanya mitihani.

Hivyo, Serikali ihojiwe ieleze dhamira ya kweli ya mabadiliko ya viwango vya ufaulu na kutakiwa kushughulikia vyanzo vya matatizo katika elimu badala ya kuficha matokeo mabaya na hali halisi za wahitimu.

Serikali inafanikiwa kuficha udhaifu kwa sababu ripoti kamili za uchunguzi juu ya ufaulu duni wa wanafunzi hazijawahi kuwekwa hadharani ili kujua kiini cha tatizo. Mara zote Serikali imekuwa ikifanya maamuzi bila kuzingatia ripoti za uchunguzi na ndio maana Serikali haikusita kuunda tume ya kuchunguza sababu za kufeli kwa wanafunzi wa kidato cha nne 2012 wakati kulikuwa na tume iliyofanya kazi hiyohiyo mwaka 2010.

Endapo tutaendelea kufikiri kwamba kulegeza njia za ufaulu ndio kuboresha elimu, tutajikuta tuna taifa la watu wenye vyeti vizuri vya elimu lakini wasioweza kufanya kazi inayoshabihiana na alama za ufaulu katika vyeti vyao.

Wataalamu wa elimu waitake Serikali kuacha kufanya mambo yanayohitaji utaalamu kwa ajili ya kujitafutia sifa kisiasa kwa mipango mibovu. Suala la elimu lisichukuliwe kama ajenda ya siasa chafu kwani kwa kufanya hivyo
tunaiua elimu yetu.

Ni vema kabla Serikali haijafanya maamuzi ya jambo linaloathiri maisha ya watanzania wengi kama hili la mitihani ikaleta kusudio la kufanya hivyo bungeni ili wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi wajadili na kuishauri Serikali Ipasavyo.

Mwisho kabisa, napenda wananchi wafahamu kwamba kwa mujibu wa kitabu kinachoonyesha viwango vya ufaulu duniani kila mwaka cha "International Qualification", baada ya Tanzania kutangaza alama mpya za ufaulu, sasa inakuwa nchi inayoongoza duniani kwa kuwa na alama za chini za ufaulu. Maana yake ni kwamba, tumeshusha ubora na thamani ya elimu yetu.

Hivyo naitaka Serikali kutoa ufafanuzi ni kwanini isifute uamuzi wake wa kubadili viwango vya ufaulu ambayo tayari umeanza kuficha hali hali ya matokeo mabaya katika mitihani. Na badala yake itoe kwa umma na iwasilishe bungeni ripoti za uchunguzi zilizoundwa na kuliwezesha Bunge kufanya maamuzi ya kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunza.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)
22/02/2014