Mch. Msigwa aitwa msaliti kwa kuituhumu Serikali kupitia Daily Mail

Umoja wa Wabunge wa Hifadhi ya Wanyamapori na Mazingira (TPGSNRCU), umemshukia mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msingwa (CHADEMA), ukidai ni msaliti na mnafiki.

Umoja huo umesema kauli zilizotolewa na Msigwa alipozungumza na mwandishi wa gazeti la Daily Mail la Uingereza, kuwa serikali haifanyi juhudi za kulinda rasilimali hazina ukweli.

Pia umemtaka Msigwa kuwa mzalendo na kuacha kutoa kauli zinazolidhalilisha taifa kwa lengo la
kujipatia umaarufu kisiasa kwa mambo yasiyo na chembe ya ukweli.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, katika Ofisi Ndogo za Bunge mjini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa TPGSNRCU, Athumani Mfutakamba, alisema serikali imekuwa mstari wa mbele katika kupambana na ujangili.

Mwandishi wa gazeti la Daily Mail, Martin Fletcher, katika chapisho la Februari 8 na 9 mwaka huu, alimshutumu Rais Kikwete, akidai ameshindwa kutimiza wajibu wake wa kuwalinda tembo na faru.
Gazeti hilo lilimnukuu Msigwa, ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa, serikali haifanyi juhudi za kulinda rasilimali, taarifa ambazo hazina ukweli.

Kwa mujibu wa Mfutakamba, Rais Kikwete yuko mstari wa mbele kupambana na ujangili na aliidhinisha Operesheni Tokomeza Ujangili.
“Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele kupinga biashara hii haramu kwa nguvu zote, kusema haonyeshi juhudi ni kumdhalilisha”
Alisema mwandishi wa gazeti hilo, alipaswa kumuuliza Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maliasili na Mazingira, James Lembeli, ili kupata ukweli na si Msigwa, ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo.

Mfutakamba alisema umoja huo unafikiria kuiomba serikali imtake mwandishi huyo aombe radhi kwa kuandika taarifa za uongo na udhalilishaji kwa taifa.

Kwa upande wake, Katibu wa umoja huo, Sylvester Mabumba, alisema wataitaka serikali imuamuru mwandishi huyo kuomba radhi kutokana na taarifa hizo.

Alisema kabla mwandishi huyo hajachapisha habari, alitakiwa kumuuliza Lembeli na serikali ili apate ukweli wa mambo.

--- via gazeti la Uhuru