Misaada kwa ajili ya mapacha 4 na yatima yapokelewa na walengwa

Joseph Mwaisango wa Mbeya yetu akiwakilisha msaada toka kwa familia ya mama Masawe wa DSM kwa kituo cha kulelea watoto yatima cha NURU kilichopo Uyole, mkoani Mbeya.
-----------------------

Kituo cha Mtandao wa kijamii cha Mbeya Yetu kimepokea Misaada mbalimbali kutoka kwa wasamaria wema kwa ajili ya Kituo cha kulelea watoto wa mitaani cha Nuru kilichopo Uyole Jijini Mbeya na Aida Nakawala (25) mkazi wa kijiji cha Chiwanda, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Mbeya, ambaye alijifungua watoto wanne kwa mkupuo (Quadruplets) usiku wa kuamkia Mwaka mpya wa 2014 katika Hospitali ya Wazazi ya META jijini Mbeya.

Msaada wa kwanza ulipokelewa hivi karibuni wenye thamani ya shilingi Laki Moja kutoka Familia ya
Masawe wa Dar es salaam kwa ajili ya kituo cha Nuru ambapo Mbeya yetu iliuwasilisha kama ulivyo.

Mbali na msaada huo pia Mtandao huu ukishirikiana na mtandao wa kijamii wenye makao yake makuu Jijini Dar es Salaam wa Michuzi Blog ulipokea kutoka kwa Msamaria mwema wa Uingereza, Bi Gladness Sariah, ambaye alitoa maboksi mawili yenye nguo na vitu kadhaa vya watoto.

Misaada toka kwa Bi Gladness Sariah wa Uingereza, Dar es salaam kwa Norah SilverBoutique

Aidha katika kuonesha wengi wameguswa na tukio la Mwanamke huyo kujifungua watoto wanne ambao wanaendelea vizuri, pia Msamaria mwema mwingine aliyejulikana kwa jina la Dada Norah SilverBoutique toka Dar es salaam naye ametoa Maziwa Lactogen makopo 24 pamoja na nguo ambavyo vimewasili salama katika ofisi ya Mbeya Yetu.

Shukrani kwa Wazee wa Kazi, Serengeti Freight Forwarders ya huko Uingereza na ofisi za Michuzi Media Group (MMG) kuwezesha kufika kwa mizigo hii Mbeya.

Kutokana na kupokelewa kwa mizigo hiyo ambapo kituo cha Nuru kilikabidhiwa Katoni Mbili za Sukari, Sabuni na Biskuti pia Tunatarajia kuanza safari ya kwenda huko Chiwanda Wilaya ya Momba Kilomita zaidi ya 260 toka Mbeya mjini kufikisha misaada ya Mama wa mapacha wanne.

Hivyo ni wito wetu kwenu kuendelea kutuombea na kutuunga mkono katika safari hiyo ili tuweze kuifikisha salama mizigo hiyo ikiwa ni pamoja na kuangalia maendeleo ya Watoto hao ambapo watakuwa wameshatimiza mwezi mmoja na siku 24.

Aida Nakawala (25) mkazi wa kijiji cha Chiwanda, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Mbeya, ambaye alijifungua watoto wanne kwa mkupuo (Quadruplets) usiku wa kuamkia Mwaka mpya wa 2014 katika Hospitali ya Wazazi ya META jijini Mbeya.

Tunawashukuru sana tena sana wote mliojitolea na Mungu awabariki sana.

Kama umeguswa na hili na unataka kutoa msaada tafadhali wasiliana na: [email protected] ama [email protected]

Nasi tutafikisha ubani wako.

Wazee wa Kazi Serengeti Freight wametoa ofa ya kusafirisha bure misaada ya aina hii toka Uingereza.

Mbarikiwe sana Wazee wa Kazi.