Mtuhumiwa aliyakamatwa kwa mauaji ya Tarime afariki dunia

Mtuhumiwa wa mauaji ya watu tisa na unyang'anyi wilayani Tarime mkoani Mara, aliyeripotiwa kukamatwa wiki iliyopita Februari 6, 2014 huko mkoani Tanga na kuwa mikononi mwa Polisi akihojiwa, ameripotiwa kufariki dunia katika Hospitali ya Wilaya wakati akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa pumu.

Kamanda wa Polisi Tarime na Rorya, Kamishina Msaidizi Justus Kamugisha, alisema kuwa mtuhumiwa huyo jina lake halisi ni Charles Kichune (38) na alifariki usiku wa kuamkia jana. Majina mengine aliyokuwa akiyatumia kwa mujibu wa Kamanda Kamugisha ni pamoja na Josephat Chacha na Charles Msongo.
"Mwili wa marehemu upo chumba cha maiti katika Hospitali ya Wilaya ukisubiri kufanyiwa uchunguzi na kuchukuliwa na ndugu zake,"
alisema Kamanda Kamugisha.

Kamanda Kamugisha alisema marehemu mtuhumiwa Kichune alikodisha pikipiki kutoka kijiji cha Kenyamanyori alikokuwa akiishi, hadi Musoma ambapo alipofika huko, inadaiwa alihifadhi bunduki aina ya SMG na risasi kadhaa kwa mshirika wake, Marwa Keryoba katika maeneo ya Bweri. Alipokamatwa, alimtaja Keryoba kuwa ndiye anayetunza silaha hiyo.

Februari 7 mwaka huu, Polisi walifuatilia silaha hiyo kwa Marwa na kumkuta na kumtaka kujisalimisha lakini, alikaidi na kuanza kurushia risasi askari.
"Marwa aliuawa Februari 7 alfajiri Bweri Musoma, wakati alipotakiwa kujisalimisha na kukaidi na kuanza kurushiana risasi na askari," 
alisema Kamanda Kamugisha.
Kwa mujibu wa Kamanda Kamugisha, kuna mtuhumiwa mwingine sugu wa mauaji ya watu zaidi ya 10, Senso Magabe ameuawa katika majibishano na Polisi wiki iliyopita.

Hata hivyo katika majibishano hayo, wenzake watatu walifanikiwa kutoroka na msako unaendelea wilayani hapo ambapo wananchi wameombwa kutoa ushirikiano Polisi ili kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao.

Kamanda Kamugisha alisema tayari watu wanne waliokuwa katika mtandao huo wa ujambazi wamefikishwa mahakamani kwa mashitaka ya unyang'anyi na mauaji.

Watuhumiwa waliofikishwa mahakamani ni pamoja na Kyoma Manguh, Marwa Mwita , Yohana Mgosi na Chacha Bugichere ambapo kesi zao zitatajwa Februari 19 mwaka huu.

Jana mamia ya wananchi wilayani Tarime walifurika kuona mwili wa Kichune maarufu Kenonke ambaye amekuwa tishio kwa wakazi wa wilaya hiyo.

Polisi imetangaza zawadi ya Sh milioni moja kwa atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kukamata silaha za moto katika wilaya za Tarime na Rorya.

via gazeti la HabariLeo