Mwl. Mndeme: Wingi wa Askari Usalama Barabarani na matumizi sahihi ya muda wa kazi na rasilimali Watu

Siku za karibuni nimekua nikipita Barabara ya Morogoro kuanzia Ubungo hadi Mlandizi. Huu ni umbali wa kama 50Km hivi.

Ajabu katika umbali huu kuna polisi wa usalama barabarani wengi sana kiasi cha kufanya barabara hii ionekane kama ni ya kuogofya au kuna ukaguzi maalum au operation tokomeza madereva wabovu. Hata hivyo, sijasikia kabisa uwepo wa operation hii, labda kama inafanyika kiintelejensia zaidi na kwa mwaka mzima.

Katika kushangaa wingi wa askari hawa, nilimekua nikihesabu makundi ya askari
wa usalama barabarani ambayo yanafika zaidi ya nane (hii ni kutoa walioko mizani Kibaha). Kuna sehemu ya kipande cha umbali wa kama 5km unapotokea Kongowe kwenda Mlandizi, kunakua na polisi makundi hadi manne walioko umbali wa chini ya 2km kutoka kundi moja hadi jingine.

Vituo hivi wanaposimama polisi, kuna askari zaidi ya wawili na kuna kundi linakua na askari hadi sita. Kwa hali hii unaweza kujikuta unasimamishwa kila baada ya 2km au 5km na kila unaposimamishwa wote wanauliza mambo yaleyale; wanakutaka uoneshe leseni yako, kadi ya gari, fire extinguisher, kukagua bima na road license. Kibaya zaidi ni kuwa hakuna uratibu au mawasiliano yanayoweza kukufanya ukikaguliwa kituo hiki usikaguliwe kinachofuata. Hivyo unaweza kunajikuta unasimamishwa na kuulizwa mambo yaleyale na kukaguliwa vitu vilevile kila baada ya umbali mdogo sana.

Mazingira ya barabara hii na wingi wa magari haviruhusu sana dereva kukimbiza gari kwa mwendo wa kutisha. Lakini kuna makundi kadhaa ya askari hawa wenye tochi za kupima mwendokasi na wanafanya hivi kwa kujificha au kuvizia.

Kwa mtazamo wangu, huu mpangilio au matumizi ya askari unahitaji kutizamwa upya kwa sababu zifuatazo:

 1. Moja: ninaona kama haya ni matumizi mabaya ya nguvu kazi na rasilimali watu. Kuweka kundi kubwa namna hili la askari wa usalama katika umbali mdogo kiasi hiki ni kutumia rasilimali watu vibaya. Ni gharama kubwa sana kuajiri watu na kisha kukawa hakuna kazi ya kutosha kufanya na kufanya kazi ya mtu mmoja kuwa ya watu kumi.
 2. Mbili: Askari hawa wanatumika kwa wingi hivi sehemu moja wakati ni kweli kuwa kuna uhitaji mkubwa sana wa ulinzi na usalama kwenye maeneo mengi wanayoishi raia. Ninadhani ndugu zetu hawa wangeweza kutusaidia usalama maeneo mengi mengine na tukawa na jamii ambayo iko salama na amani zaidi ya ilivyo sasa
 3. Tatu: Ninaona kama huku ni kutesa raia na waendesha magari pale ambapo gari linasimamishwa kila baada ya muda na umbali mfupi na kuulizwa maswali yaleyale na kukaguliwa vitu vilevile. Katika kupita njia hii na kusimamishwa kwenye umbali usiozidi 2km, niilimuuliza askari mmoja ni kwa nini wana utaratibu mbaya hivyo; naye akakiri kuwa ni mfumo mbaya na anaomba tushauri njia mbadala. 
 4. Nne: kwa mtazamo wangu, hali hii inachelewesha sana maendeleo na kuongeza umaskini kwa nchi yetu. Tayari tuna tatizo kubwa la matumizi ya muda ambalo linachangia sana umaskini katika nchi yetu. Kulazimishwa kupoteza muda zaidi bararabara kwa mambo yasiyo na tija ni kushindwa kuthamini matumizi sahihi ya muda kama kiungo muhim sana cha maendeleo binafsi, familia, jamii na taifa
 5. Tano: Askari wengi hawana haraka na hawaogopi kukupotezea muda wapendavyo. Unaweza kusimamishwa ukiwa na kila kinachotakiwa na bado ukajikuta unapotezewa muda tu na mara nyingine kuambiwa unapelekwa kituoni kwa jambo ambalo halina ulazima huo. Wengi wa askari hawa wanashikwa na hasira wanapokukuta huna kosa.

Ushauri kwa Jeshi la Polisi:

 1. Jeshi la polisi na seriakli kwa ujumla, liwekeze zaidi katika kutoa elimu sahihi ya usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kudhibiti upatikanaji wa leseni bila mafunzo, ili kuhakikisha kuwa watumiaji wa barabara wana elimu na ufahamu wa kutosha kuhusu matumizi ya barabara na hivyo kuondoa ulazima wa kutumia nguvu kubwa kusimamia sheria
 2. Jeshi la polisi wajisikie vibaya kujenga kizazi na jamii inayotii sheria kwa woga na shuruti na badala yake ifurahie kuwa na jamii inayotii sheria kw akupenda. Kwa minajili hiyo, isiwekeze sana katika kutoa adhabu na kuvizia makosa ya kuadhibu, bali wawekeze katika kuelimisha, kuelekeza na kuongoza.
 3. Kuna haja ya ungozi wa jeshi la polisi kushirikiana na wataalamu wa fani zingine kama ICT kuangalia namna nzuri, rahisi, ya kisasa na yenye gharama nafuu katika kufanya ukaguzi wa kawaida wa magari barabarani. Kwa mfano, kwa magari yanayokwenda mikoani (hasa madogo) kunaweza kuwekwa utaratibu kuwa, likashakaguliwa mambo ya msingi katika kituo cha kwanza (mfano kikawa baada ya mbezi mwisho), kunakua na alama inayoonesha gari na dereva wana vigezo vya kutembea njia kuu bila ukaguzi hadi mwisho wa safari; isipokua tu iwapo atatenda kosa. Hili linawezekana kabisa ikiwa ni pamoja na kuwawezesha askari wa vituo vingine kuhakiki (validate) ukaguzi husika.
 4. Pamoja na unyeti wa kazi za walinzi hawa wa usalama wetu, ni vema wakatambua umuhimu na unyeti wa muda katika kulitoa taifa letu hapa lilipo. Ni shida kidogo unapokwenda umbali wa 50km na kutumia masaa kadhaa kwa sababu tu ya ukaguzi wa kila hatua chache au kwa sababu askari fulani alijisikia vizuri kukuonesha mamalaka yake kwa kukuweka barabarani muda mrefu au kukupeleka kituoni bila kosa
 5. Polisi wetu watambue kuwa karne ya watu kujazana Dar es Salaam imepitwa na wakati. Ni wazi kabisa kuwa kwa sasa baadhi ya watu wanaweza kufanya kazi au shughuli zao za kipato DSM na wakaishi nje ya mji kama vile Kibaha, Mlandizi, Ruvu, Bagamoyo, Msata Chalinze na hata Morogoro. Hii inasaidia kupunguza msongamano ndani ya mji na kuwawezesha watu kufanya shughuli zingine za uzalishaji hasa kilimo ambacho ni ngumu kufanya hapa mjini. Kwa mfumo wa kupotezeana muda barabarani ulioko sasa, hili haliwezekani; sio kwa vile maeneo haya ni mbali sana au kuna foleni; bali ni kwa sababu ya ukaguzi wa polisi ambao ungeweza kuboreshwa na kuokoa muda.
 6. Jeshi la polisi lishirikiane na wataalamu wengine nje ya jeshi lao kuona namna ambavyo watasimamia sheria na taratibu za barabarani kwa rasilimali watu ndogo (askari wachache) na bado wakafanikisha majukumu yao kwa ufanisi mkubwa. Hii haitaondoa tu usumbufu na matumizi mabaya ya rasilimali watu na muda, bali itapunguza hata shutuma na rushwa zinazohusishwa sana na askari hawa (bila kujali ni za kweli au uongo)

Mwalimu MM