Nape Nnauye: “...tofauti kubwa ya mimi na wao”

Imeandikwa na Bashir Nkoromo —  KATIBU wa NEC Itikadi na Uenezi-CCM Nape Nnauye amesema, ndoto aliyokuwa nayo ya kazi ambayo angependa kufanya alipokuwa hajawa mwanasiasa ni kuwa Mwanajeshi rubani wa ndege.

Amesema maandalizi ya kutimiza ndoto hiyo alikuwa ameianza kwa kuweka kipaumbele kwenye masomo ya fani hiyo ikiwemo fizikia na jiografia wakati anamaliza kidato cha nne.

Nape mwenye umri wa miaka 37, sawa na umri wa CCM, amesema hayo jana alasiri alipododoswa na watangazaji kwenye kipindi cha 'Power Jam' katika Kituo cha Radio cha East Africa, kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, ambao walitaka awaambie wasikilizaji ni kazi ya fani ipi aliyokuwa akiipenda kuifanya asingekuwa mwanasiasa.
"Kazi niliyopienda zaidi ni kuwa Mwanajeshi, tena Mwanajeshi mwenyewe ambaye ni rubani wa kurusha ndege za kijeshi...Na hata nilipokuwa namaliza kidacho cha nne, nilikuwa nimejiandaa zaidi katika masomo ya fani hiyo ikiwemo fizikia na jiografia"
alisema Nape.

ANAVYOJITOFAUTISHA NA WANASIASA WA VYAMA VYA UPINZANI

Akizungumzia tofauti iliyopo kati yake na wanasiasa walipo kwenye vyama vya upinzani kama walivyotaka kujua watangazaji hao, Nape alisema, tofauti kubwa iliyopo ni kwamba yeye ni mwanasiasa ndiyo sababu yupo kwenye chama cha CCM ambacho ni cha siasa lakini wapinzani siyo wanasiasa bali ni wana harakati kwa sababu wapo kwenye vyama vya harakati siyo vya siasa.
"Unajua mimi ni mwanasiasa ndiyo sababu nipo kwenye Chama Cha Mapinduzi ambacho ni chama cha siasa, lakini hao wengine ni wana harakati ndiyo sababu wapo kwenye vyama vya harakati. Na hii ndiyo tofauti kubwa ya mimi na wao"
alisema Nape.