NW Majaliwa ashusha cheo, avua madaraka Ofisa Elimu, Walimu Wakuu


NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Waziri mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Kassim Majaliwa amemvua madaraka kwa kumshusha cheo Ofisa elimu shule za sekondari wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hanji Yusuph Godigodi kwenda kuwa mwalimu wa kawaida wa sekondari kutokana na Ofisa huyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kazi na kufanya ubadhirifu wa shilingi milioni 268 za maendeleo ya elimu ya sekondari wilayani humo.

Aidha amewashusha vyeo Wakuu wa shule za sekondari sita za wilaya hiyo kwenda kuwa walimu wa
kawaida, kutokana na walimu hao wakidaiwa kushirikiana na Ofisa huyo wa sekondari kufanya ubadhirifu wa fedha hizo.

Hatua ya Naibu Waziri huyo kuwashusha vyeo viongozi hao ilifikiwa katika kikao ambacho alikuwa akizungumza na Walimu wa shule za msingi na sekondari wilayani humo, ambacho kiliketi kwenye ukumbi wa Uvikambi uliopo mjini hapa na kwamba Waziri huyo yupo katika ziara yake ya kikazi wilayani
Mbinga kwa muda wa siku mbili.

Waziri Majaliwa aliwataja wakuu wa shule za sekondari wilayani Mbinga ambao wameshushwa madaraka kuwa ni William Hyera ambaye ni wa shule ya sekondari Maguu, Clemence Sangana anatoka shule ya sekondari Mkuwani, Method Komba, Langilo sekondari, John Tillia, Ukilo sekondari, Leonard Juma, Luli
Sekondari huku akimtaja kwa jina moja mwalimu Konga ambaye yupo sekondari ya Kihangimahuka.
“Nimekwazwa sana na maendeleo ya shule za sekondari hapa Mbinga maafisa elimu na walimu wakuu mnatumia fedha za maendeleo kinyume na taratibu, mnalipana posho na sio kufanyia kazi husika kama serikali ilivyopanga hivyo naagiza katika hawa niliotengua nyadhifa zao wasaidizi wao nawapandisha vyeo kuanzia sasa, wachukue nafasi hizo mapema wakati utaratibu wa barua za kuwathibitisha unafuata,” alisema Majaliwa.
Alisema fedha hizo zilizotafunwa zililenga kufanya kazi ya kununua vitabu kwa shule za sekondari wilayani humo lakini anashangaa kuona kwamba utekelezaji husika kama serikali ilivyopanga haujafanywa.

Alifafanua kuwa katika fedha hizo shilingi milioni 108 ilibidi zitumike kununua vitabu hivyo, na zinazobakia zifanye shughuli zingine za maendeleo husika katika shule hizo.
“Fedha za mgao wa vitabu mnazitumia vibaya mna ajenda gani na hizi fedha?, ofisa elimu nimemrudisha darasani akafanye kazi ya kufundisha ili iwe fundisho kwa wengine,” alisema.
Kadhalika Naibu Waziri huyo alieleza kuwa Ofisa elimu huyo wa shule za sekondari wilayani Mbinga Hanji Godigodi, ameshindwa kusimamia ipasavyo maendeleo ya shule hizo na kuifanya wilaya hiyo kushika nafasi ya tatu kutoka mwisho kati ya shule 4,337 kitaifa, katika mtihani wa matokeo ya kidato cha nne mwaka jana.

Alisema tatizo kama hili lililojitokeza hapa Mbinga, lipo maeneo mengi hapa nchini na linatokana na Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa halmashauri, kutosimamia ipasavyo malengo yaliyowekwa na serikali ikiwemo
kufanya ziara za kutembelea shule za sekondari ili waweze kubaini matatizo yaliyopo.
“Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi nimebaini kuwa hamtembelei shule hizi, muda mwingi mnakaa ofisini na kutengeneza mambo ambayo hayafanani kabisa na mahitaji halisi ya wananchi, sasa naagiza ondokeni ofisini nendeni kwa wananchi mkasikilize matatizo yao na kuyafanyia kazi haraka”, alisisitiza Majaliwa.
Majaliwa aliongeza kuwa serikali itaendelea kuwajibisha watendaji wazembe ambao wanaonekana kutotimiza majukumu ya kazi walizopewa, ili kuweza kujenga heshima ya taifa hili na kuwatendea haki wananchi kwa kuwapa huduma bora.

Kwa upande wa shule za msingi mkoani Ruvuma, waziri huyo alisikitishwa na suala la watoto waliomaliza darasa la saba mwaka jana ambao wamefaulu kwenda sekondari, Watoto 1,956 hadi sasa hawajaripoti kwenda shule huku akiutaka uongozi husika wa mkoa huo kuhakikisha kwamba, ifikapo mwezi Aprili mwaka huu wahakikishe wanatoa taarifa kwake juu ya maendeleo ya watoto hao kwamba wawe wamekwenda kuripoti katika shule walizopangiwa kinyume na hapo serikali itachukua hatua kwa watendaji husika.

--- via blogu ya DEMASHO News