Raha na karaha ya Bunge la Katiba huko Dodoma

Mji wa Dodoma umefurika watu huku huduma mbalimbali za kijamii kama vile vyakula na vyumba vya kulala wageni vikipanda bei.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti la NIPASHE lililofanikiwa kupita katika baadhi ya nyumba za kulala umejionea ukarabati katika nyumba hizo lakini ukabaini kuwa nyingi zilikuwa zimejaa na tayari wafanyabiashara waliuwa wamepandisha kodi. Pia gharama za bidhaa mbalimbali zimepanda bei.

MALAZI
Vyumba vya kulala wageni vya kawaida vilivyokuwa vinapangishwa Sh. 15,000 sasa
vinapangishwa kwa Sh. 20,000 na vile vya Sh. 20,000 Sh. 30,000.

VYAKULA
Nyama inauzwa Sh. 6,000 kwa jilo moja badala Sh. 5,000 ya awali, huku samaki wabichi aina ya Sato waliokuwa wakiuzwa kilo kwa Sh. 6,000 sasa ni Sh. 7,000. Kuku wa kienyeji waliokuwa wakiuzwa Sh. 8,000 sasa wanauzwa kati ya Sh. 10,000 hadi 12,000.

USAFI

Wafanyabiashara wadogo wadogo wameondolewa huku mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Dodoma ikifanyiwa usafi wa hali ya juu. Aidha, taa za barabrani ambazo zilikuwa zimeanguka kwa kugongwa na magari zote zimefanyiwa mategenezo na sasa zinafanyakazi.

USALAMA

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema jeshi hilo kwa kwa kushirikiana na vyombo vya dola vitahakikisha kuwa wajumbe wa Bunge hilo wanafanyakazi kwa usalama.

Alisema watahakikisha kuwa wanaweka doria za pikipiki na magari ili kuwapo na hali ya utulivu. Pia, wanafanya misako ya kuwakamata wahalifu ambao wanaweza kusababisha uvunjifu wa amani
“Tumeongea na viongozi wa mitaa kuimarisha ulinzi shirikishi na kila mwananchi ambaye ataona jambo lisilo la kawaida kutoa taarifa polisi,”

MALALAMIKO

Baadhi ya wakazi wa mjini Dodoma waliozungumza na gazeti la NIPASHE wameiomba serikali kuwadhibiti wafanyabiashara wanaopandisha bei kiholela.

Brian John alisema imeibukana tabia ya wafanyabiashara na wamiliki wa nyumba za kulala kupandisha bei kiholela bila kujali kipato cha wageni hao.

Winnie Binamu alisema upandaji huo wa bei za bidhaa ambao wakati mwingine hufikia mpaka zaidi ya mara tatu ya kawaida umekuwa ukiwaumiza na kusababisha ugumu wa maisha kwa watu wa kawaida waishio katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Dodoma.