Taarifa Wizara ya Fedha kuhusu suala la pensheni kwa Wabunge

JAMHURI YA MUUNGANO YA TANZANIAWIZARA YA FEDHA

TANGAZO KWA UMMA

Katika siku za hivi karibuni, baadhi ya magazeti yamekuwa yakitoa taarifa za upotoshaji juu ya suala la kuongezeka kwa malipo ya pensheni kwa Waheshimiwa Wabunge. Magazeti hayo yanadai kwamba Mheshimiwa Waziri wa Fedha amethibitisha ongezeko hili. Taarifa hizo ziliendelea kudai kwamba Waheshimiwa Wabunge watakapostaafu watastahili kulipwa shilingi 160 milioni kila mmoja.

Kwa kupitia tangazo hili, tunaeleza kwamba, Mheshimiwa Waziri wa Fedha hajawahi kuongea na Mwandishi wa Habari yeyote kuhusu suala la nyongeza ya pensheni ya Waheshimiwa Wabunge na maelezo kwamba Mheshimiwa Waziri alithibitisha taarifa za ongezeko hilo sio kweli bali ni maelezo binafsi ya Waandishi wa Habari hizo na suala hilo halipo Serikalini wala Bungeni.

Aidha, tunapenda kuwaasa Waandishi wa Habari kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao na kuacha kuwachonganisha Wabunge na Wananchi wanaowaongoza kwa kuwapotosha kwa masuala ambayo hayana ukweli na uthibitisho wowote.

KATIBU MKUU – WIZARA YA FEDHA

5 FEBRUARI, 2014