TGNP Mtandao
P.O. Box 8921, Dar es Salaam, TANZANIA; Gender Resource Centre, Mabibo Road,
Tel. 255 022 2443205/2443286/2443450;
Mobile 255 0754 784050, 0715 784050; 0784 784050 Fax 255 022 2443244; Email [email protected] ; web www.tgnp.org
21/02/2014
TAARIFA KWA UMMA
WABUNGE BUNGE MAALUM LA KATIBA WASILIPWE POSHO ZAIDI
TGNP Mtandao tumesikitishwa na taarifa za wajumbe wa Bunge maalum la Katiba lililoanza Februari 18, 2014, kudai nyongeza ya posho kutoka shilingi 300,000/= hadi sh. 500,000/= kwa siku. Sisi TGNP Mtandao kama shirika linalotetea haki na usawa wa kijinsia katika kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wote hatukubaliani kwa namna yoyote na madai hayo ya wajumbe kudai posho zaidi kwa wakati huu ambao taifa lina uhaba mkubwa wa fedha na deni la taifa likiongezeka kwa kasi kubwa hadi kufikia trilioni 27.
Inasikitisha kuona wawakilishi tuliowatuma Dodoma kujadili rasimu ya Katiba mpya akili na mawazo yao yote
yakielekezwa katika posho. TGNP tunajiuliza Shilingi 300,000/= kwa siku ni kidogo? Hicho kiasi ni zaidi ya mshahara wa baadhi ya watumishi serikalini na sekta binafsi ambao wanapambana kulea familia kwa mshahara huo huo na pindi wakidai kuongezewa maslahi yao wabunge wameshindwa kuwatetea?. Ni wabunge hawa ambao wameshidwa kupigania haki za wanawake na wanaume wanaopata kima cha chini cha mishahara kipandishwe. TGNP Mtandao tunapinga mpango huu wa kuongeza posho kwasababu unajenga tabaka miongoni mwa jamii na ndani ya Bunge na kuiingizia serikali mzigo wa gharama ambazo mwishowe atazilipa mwananchi masikini.
Pia suala la posho tunaliona kama mbinu inayotumiwa na wanaisasa wachache wasio na uzalendo kutaka kuvuruga mchakato wa katiba mpya kwa kuhamisha mijadala yenye tija katika kuandika katiba mpya. Tunawataka wanasiasa kuheshimu mchakato huu ambao unatumia gharama kubwa za walipa kodi na kuhakikisha wananchi wanapata katiba mpya inayobeba masuala na sauti zao. Kamati iliyoundwa kufuatilia posho isipoteza muda kujadili suala hilo na kupelekea kuongezwa kwa muda wa Bunge hili zaidi ya siku 70.
Tunatoa rai kwa wajumbe wote wa Bunge hili kuwa makini na kauli zao na kufanya kazi waliotumwa Dodoma kwa maslahi ya taifa na anayeona kwamba fedha hazimtoshi anapaswa kurudi nyumbani ili kutoa nafasi kwa wazalendo wa Taifa hili kuandika katiba ya Tanzania. Aidha wanaovuruga mchakato huu wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kuliingizia taifa hasara.
Imetolewa na:
Signed
Lilian Liundi
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
TGNP Mtandao