Taarifa ya TGNP kuhusiana na uteuzi wa Wajumbe wa Bunge la Katiba

11/02/2014


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Ijumaa Februari 8, 2014 Rais Jakaya Kikwete alitangaza majina ya wajumbe 201 wa Bunge la Katiba, watakaoshirikiana na wajumbe wengine ambao ni wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wapatao 357, wajumbe wa Baraza la wawakilishi Zanzibar wapatao 81 Jumla kuu inalifanya Bunge la katiba kuwa na wajumbe 639.

Kwa mujibu wa sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka namba 81 ya 2013, Rais amepewa mamlaka ya
kuteua wajumbe wa Bunge hili kwa kushauriana na rais wa Zanzibar baada ya kupelekewa mapendekezo ya majina kutoka kwa makundi yote ya wananchi.

Sisi wanaharakati wa masuala ya Kijinsia, haki za binadamu, demokrasia na utawala bora tumefuatilia kwa makini mchakato huu tukiwa pamoja na wenzetu wa mashirika mengine ya kiraia na baadhi ya makundi na kupendekeza majina ya wataalamu wa masuala ya kijinsia na haki za binadamu ambao wangeweza kutoa uchambuzi wa kina na kushiriki kutetea baadhi ya vifungu vya rasimu ambavyo vinabeba sauti za wananchi kwa mustakabali wa taifa letu.

Mchakato huu wa uteuzi umekuwa na mapungufu na sura tofauti kama ilivyokuwa katika kipindi cha kujadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba 2013.

Kukosekana kwa ushiriki mpana wa uwakilishi wa makundi halisi yaliyoko pembezoni na kuchomeka majina ya watu wasiostahili kwenye nafasi za makundi mengine kutasababisha mapungufu makubwa ya uwakilishi katika mchakato huu.

Tumesikitishwa na kuingizwa kwa majina ya wanasiasa kwenye kundi la NGO na kuwaacha wawakilishi wa asasi za kiraia wakati wanasiasa walikuwa na uwakilishi mkubwa kwenye kundi lao la watu 40. Aidha kundi la watu wenye mlengo unaofanana nalo hatukupewea tafsiri halisi kuwa ni watu kuitoka kundi gani au ni kina nani badala yake wameingia wanasiasa na kulifanya Bunge hili la katiba kuwa na wanasiasa wengi zaidi ya makundi mengine.

Wanaharakati tunahoji nini ilikuwa tafsiri ya watu wenye malengo yanayofanana? Baada ya wanasiasa kuteuliwa kupitia kundi lao la wajumbe 40 hawakutakiwa kuingia tena kupitia kundi hili la pili badala yake wangezingatia makundi yaliyokuwa yamebaki.
Tunajiuliza kwa hali hii ya kujaza wanasiasa kwenye haya makundi ya wananchi tutapata katiba mpya tunayostahili kuwa nayo? Tunadai uwakilishi zaidi wa makundi mengine kwenye hili Bunge kwa sababu:-

(i)Wabunge wa sasa hawakuchaguliwa kwa kuzingatia uwiano wa kijinsia na makundi yaliyoko pembezoni

(ii) Wabunge wa sasa wamechaguliwa kwa kuzingatia mfumo na ushawishi na itikadi za vyama vyao vya siasa; na sifa zilizopelekea kuchaguliwa kwao na hadidu zao za rejea zimejikita katika kusimamia na kutetea katiba iliyopo na siyo kitunga Katiba;
Tunaendelea kudai usawa wa Kijinsia katika mchakato huu kwani msingi wa kijinsia haujazingatiwa kama vile Itifaki ya Maputo, AU Constituent Act, AU Shared Values na CEDAW na Mkataba wa Watoto (CRC) zinavyotamka.

Mwisho tunataka masuala muhimu ya wanawake ambayo yameonekana kwenye rasimu ya pili ya Katiba yaheshimiwe na wajumbe wa Bunge hili na yasitolewe bali yaboreshwe ili kutoa nafasi ya ushiriki kamili wa wanawake na wanaume katika mgawanyo wa rasilimali za Taifa na kwenye fursa za uongozi.
Imetolewa na:

Signed

Lilian Liundi
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
TGNP Mtandao