Dar es Salaam, Februari 19, 2014 -- Kampuni ya mawasiliano ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania imejumuika na washindi wake 48 wa iliyokuwa Promosheni ya Timka na Bodaboda iliyodumu kwa kipindi cha miezi mitatu (3) kutoka Oktoba mwaka jana hadi Januari mwaka huu huku ikijivunia kuboresha maisha ya mamia ya Watanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Tanzania, Salum Mwalim amesema ni furaha kwa sababu wametimiza azma ya kubadili maisha ya Watanzania.
“Lengo letu lilikuwa ni kuja na promosheni itakayokuwa na zawadi ambazo zitabadili maisha ya wateja wetu, kutengeneza fursa za ajira na kuwategenezea vipato vya kuboresha maisha.” Alisema na kuongezea “Leo tunafuraha kuona kuwa lengo letu limetimia.”
“Ni azma ya wakati wote ya Vodacom kubuni na hatimae kuja na mambo mapya sokoni yatakayoendela kututofautisha sisi na wengine tukiakisi mahitaji ya wateja wetu moja kwa moja pamoja na kutengeneza fursa za kuyabadili maisha yao.” Alisema Mwalim.
Aliongeza kuwa kupitia promosheni hii, Vodacom wanajivunia kutoa Bodaboda 430 ambazo wateja wamejishindia sehemu mbalimbali za Tanzania. Hii ina maana kwamba kampuni hiyo imefanikisha malengo matatu ambayo ni pamoja na :- Kuchangia kustawisha maisha ya washindi na ya familia zao kwa kuwapatia vyombo vya usafiri kwani umuhimu wa bodaboda katika sekta ya usafiri kwa sasa hapa nchini kamwe haiwezi kupuuzwa.
Mwalim alisema “tumengeneza ajira nyingi kutokana na ukweli kwamba bodaboda hizi zinatumiwa kwa shughuli na malengo ya kibiashara. Wateja wetu ama wamejiajiri au kuajiri vijana wa kuziendesha na kuzisimamia kibiashara. Hivyo basi kwa wastani tu sio chini ya ajira 300 ambazo tumezitengeneza sehemu mbalimbali ya nchi kupitia washindi wetu”.
“Mbali na hapo, Vodacom imechangia kuleta unafuu na urahisi wa usafiri na usafirishaji. Kama tunavyotambua, bodaboda kwa sasa zimekuwa na msaada mkubwa katika kutoa huduma ya usafiri hasa maeneo ya vijijini na yaliyo pembezoni na miji. Ni wazi kwamba sio tu zimeleta riziki majumbani bali hata kuokoa maisha ya watu ambao wanapatwa na dharura zinazohitaji kukimbizwa hospitalini.” Alisema Mwalim.
Alihitimisha kwa kusema kuwa “Rai yetu kwa washindi wote ni kutambua thamani ya kile tulichowapatia kwa kuhakikisha kwamba wanazitunza pikipiki hizi ili ziweze kuwasaidia kwa kipindi kirefu zaidi huku. Pia nawaomba mzingatie matumizi salama ya Bodaboda ikiwemo sheria za usalama barabarani kila siku.”