[video] Membe asema: “Chama inabidi sasa kichague nani anafaa kuwa kiongozi”

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amekitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM), kiruhusu mgombea wa urais mwakani, kujulikana ifikapo Desemba.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya CCM, White House mjini Dodoma, mara tu baada ya kutoka kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM, Membe alikiri kwamba aliitwa kuhusiana na mbio za urais wa Tanzania mwaka 2015.
"Nazungumza nanyi kwa sababu mbili; moja katika wiki moja iliyopita nimepata meseji nyingi sana na
watu wakiuliza kulikoni kuitwa Dodoma. Pili, ni kweli ninatoka kuhojiwa katika Kamati ya Maadili, wote tuliitwa kuhojiwa," 
Membe aliwaambia waandishi wa habari.

Aliisifu kamati hiyo inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, kwa kusema:
"Kamati yetu ya Maadili imejipanga vizuri sana, na msidanganyike, wanauliza maswali mazito, maswali magumu ama unayoyafanya wewe au mashabiki. Lakini yote yanalenga katika kukiimarisha chama, katika kuimarisha ushindi kwa mwaka 2015 na kuimarisha maadili. Yale ni mambo mazito  
"Makubwa matatu ambayo Kamati ya Maadili inayauliza, kubwa kabisa ni uzukaji ghafla wa makundi makubwa ambayo yanazaliwa kila watu wanapodhani fulani anafaa kuwa kiongozi. Tunafanyaje kukifanya chama chetu kiwe na kundi moja litakalokwenda mwakani kwenye ushindi. 
"Lakini la pili pia ni suala zima la fedha kama msingi wa ushindi. Inatokeaje watu wanatumia mamilioni, mabilioni ya pesa katika kujinufaisha na kujiandaa kwenda kwenye uchaguzi.  
"Lakini tatu ni media, ninyi waandishi wa habari, mnalishwa vitu gani, mmemeza nini vichwani mwenu mpaka muone kinachosemwa na fulani ni cha maana hadi kitoke katika magazeti na kingine kikisemwa na fulani, hata kikiwa cha maana kisitoke kwenye magazeti, mmemeza mdudu gani." 
Membe aliitaka kamati hiyo iendelee kufanya kazi yake, akidokeza kuwa bado kuna watu wataitwa, lengo likiwa ni kuwa na chama imara, kitakachokwenda mwakani kuvishinda vyama vingine:
"Lakini la pili, nadhani sasa itafika mahala kwamba chama sasa itabidi kichague kiongozi au nani wanafaa kuwa viongozi, ili kufanyike midahalo kwa mfano, ili wananchi wajue tunapokwenda mwaka 2015, candidate wa Chama Cha Mapinduzi ni nani? Lazima tufike hapo. 
"Tukiacha kila mwanachama aombe, kila binadamu anayejiona anavaa nguo ya kijani na ana hela aombe, tutakiangusha chama chetu. Na kwa hiyo, nadhani mwelekeo sasa ni wa kushauri. 
"Na watu kama sisi tunashauri, ni vizuri sasa chama kikajipanga na kiwe na candidate, yaani kiwe na watu ambao haraka haraka wapitishwe ili inapofika kwa mfano Desemba mwaka huu, Chama Cha Mapinduzi kinajua nani anachukua bendera ya chama chetu mwakani. Ili chama chetu kiwe kimoja, kisimegukemeguke," 
Membe alionya kuwa iwe ni mwiko kwa mtu yeyote ndani ya chama kutumia fedha kama nguzo ya ushindi wake, akisema uongozi wa Taifa hauwezi kununuliwa na fedha.
"Na mimi nawaambia waandishi wa habari, chezeni mtaona, hatuwezi kuruhusu uongozi wa nchi hii au kiongozi wa juu anunue kama biashara ya njugu dukani. Mkiacha hilo linaendelea, ninyi waandishi wa habari ni sehemu ya kulaumiwa duniani. 
"Hamuwezi kuwa na kiongozi anayenunua uongozi kwa njia yoyote ile, iwe ya fedha au jambo jingine lolote lile. Na hili ndio Kamati ya Maadili inakemea na mimi najiunga nao, lazima kukemea. Huwezi kununua uongozi wa Taifa kwa namna nyingine yoyote ile. Na tutakuwa watu wa ajabu Watanzania kama tutaanza kufanya biashara ya uongozi wa kitaifa," 
alieleza Membe.

Akigusia suala lililotamatia alisema:. 
"La tatu na la mwisho nililotolea ushauri, na ambalo nataka niwaambie na waandishi wa habari, ni uongozi. Uongozi wa chama chetu, cha Mapinduzi, ndio uongozi unaotegemewa duniani, chama hiki kimefanya mambo mengi mno, na kwa hiyo lazima kuwe na mwongozo. 
"Mwongozo rasmi unaotakiwa kufuatwa na WanaCCM kuanzia ngazi ya matawi kuja mpaka huku juu kwamba unapofika wakati wa uongozi, utumie hatua zipi, uzingatie nini ili usivunje na kukiuka maadili. Mashabiki nao wafanye nini ili wasikiuke maadili, ili tuweze kwenda pamoja. 
"Kwa hiyo ni Kamati ya Maadili inayouliza maswali magumu sana, sana sana, kwa watu wanaosemwa kwamba wanaweza kuwa viongozi, lakini Kamati ya Maadili inayosikiliza ushauri, lakini ni Kamati ya Maadili inayotaka chama hiki kiende katika uchaguzi mwakani kikiwa strong yaani cha nguvu, united yaani chama kimoja na kikiwa na uhakika wa ushindi.  
"Na mimi nasema wazi kwa vyovyote vile tukizingatia hayo, Chama Cha Mapinduzi kitapeta miaka 60 ijayo, hakuna atakayeingia hapo."
Aliwageukia tena waandishi wa habari, akisema lazima wapime, waandike ya wote wote, na wasibague.
"Lakini narudia, waandishi wa habari lazima muwe objective, waandishi wa habari lazima mpime, waandishi wa habari ndio mnaoweza kuamua direction ziende wapi, lazima muandike ya watu wote wanaozungumza bila kuchagua mambo fulani ya fulani tuyaandike yote, na mwingine akisema hata akisema nini tusiandike yote, mtaiua nchi, mtajiua ninyi wenyewe, objectivity ya vyombo vya habari ni kuandika habari taarifa zote au habari zote kwa manufaa ya Watanzania wote, msiwanyime Watanzania nafasi ya kuyazungumza. 
"Kwa mfano haya niliyoyazungumza, kuna watu mtakwenda kuyachuja, Membe kazungumza hiki, tusiseme kwa sababu tutamuudhi fulani, hiki kisiandikwe tutamuudhi fulani. Halafu zitabaki tv tu," 
alisema Membe na kukataa kuulizwa maswali kwani alikwishaulizwa ndani.