Wafikishwa kortini kuhusu ARV bandia za TPI zilizosambazwa na MSD

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam pia ni Mkurugenzi Mkuu Kiwanda cha Kutengeza Dawa (TPI Ltd) Ramadhani Madabida na wenzake watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka matano ya usambazaji wa Dawa bandia za kurefusha maisha kwa waathirika wa UKIMWI na kuisababishia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) hasara ya zaidi ya Sh. milioni 148.3. 

Mbali na Madabida washtakiwa wengine ni Meneja Uendeshaji Seif Shamte, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam na Meneja Masoko, Simon Msoffe, Mhasibu Msaidizi Fatma Shango, Sadiki Materu na Evans Mwemezi. 

Walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Nyigulila Mwaseba aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo.
Kesi hiyo ya Uhujumu uchumi namba 5 ya mwaka 2014, ilifikishwa jana katika viunga vya mahakama hiyo saa 3:13 asubuhi huku washtakiwa wakiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu wa jeshi la polisi na kuhifadhiwa kwenye chumba cha mahabusu ya mahakama kabla ya kupandishwa kizimbani. 

Kimaro aliudai kuwa shitaka la kwanza linamkabili mshitakiwa Madabida, Shamte, Msoffe, na Shango, wanadaiwa kwamba Aprili 5 ,2011 jijini Dar es Salaam waliuza na kuisambazia Idara ya Bohari Kuu ya Madawa makopo 7776 ya dawa bandia aina ya Antiretroviral ambazo zinajumuisha gramu 30 za Stavudine,gramu 200 za Verirapine na Batch namba OC 01.85 zikionesha zimezalishwa Machi 2011 na kuisha muda wake Februari 2013 kwa lengo la kuonesha ni dawa halisi aina ya Antiretroviral wakati wakijua si kweli. 

Shitaka la pili pia la usambazaji wa dawa hizo ambalo linawakabili washtakiwa hao wane ambapo wanadaiwa kwamba,wakiwa na nyadhifa zao hizo,waliisambazia Bohari kuu ya madawa kopo 4476 za dawa aina ya Antiretroviral ambazo zinajumuisha gramu 30 za Stavudide,gramu 200 za Nevirapine na gramu 150 za Lamivudine zenye batch namba OC 01.85 zikionesha zimezalishwa Machi 2011 na kuisha muda wake Februari 2013 kwa lengo la kuonesha ni dawa halisi aina ya Antiretroviral wakati wakijua si kweli. 

Katika shitaka la tatu washitakiwa hao pia wanadaiwa kwamba Kati ya Aprili 12 hadi 29, 2011 jijini Dar es Salaam wakiwa na nia ya kudanganya kwa pamoja walijipatia Sh.148,350,156.48 kutoka Kitengo cha Bohari Kuu ya Madawa baada ya kudanganya kwamba fedha hizo ni malipo ya dawa halisi aina ya Antiretroviral wakati wakijua si kweli. 

Kimaro aliendelea kudai katika shitaka la nne linamkabili Sadick na Evans ambao wanadaiwa kwamba, katika tarehe tofauti kati ya Aprili n5 na 13 mwaka 2011, jijini Dar es Salaam wakiwa kama waajiriwa wa Idara ya Bohari Kuu ya Madawa kama Meneja udhiditi Ubora na Ofisa udhibiti ubora, huku wakijua nia ya kutendeka kwa kosa ambalo ni kusambaza dawa bandia,walishindwa kutumia nyadhifa zao kudhibiti kosa hilo lisitendeke. 

Shitaka la tano, linawakabili washitakiwa wote ambao wanadaiwa kwamba kati ya Aprili 5 hadi 30,2011, kwa nafasi zao na kutotekeleza majukumu yao ipasavyo waliisababishia bohari Kuu ya Madawa kusambaziwa dawa hizo bandia na hivyo Bohari kupata hasara ya Sh. 148,350,156.48 . Baada ya kusomewa mashitaka hayo,washtakiwa wote walikana tuhuma hizo na upande wa Jamhuri ulidai kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Pia, upande wa Jamhuri ulidai kwamba hauna pingamizi na dhamana kwa washtakiwa wote. Hakimu Mwaseba alisema washtakiwa watakuwa nje kwa dhamana kama watakuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakatoa fedha taslimu Sh.12,365,513 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo ya fedha kwa kila mshitakiwa. 

Hata hivyo, ni washtakiwa wawili tu -wa kwanza na wa tano Madabida na Materu - walitimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana huku wengine walipelekwa mahabusu hadi Februari 24, mwaka huu kesi yao itakapotajwa.

via Michuzi blog