Walioruhusu ujenzi wa ghorofa linalochunguila Ikulu wahukumiwa


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imewahukuu aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Makumba T. Kimweri na mwenzake na Richard Maliyaga kifungo cha kwenda jela miaka tisa au kulipa faini ya sh. milioni 15, kila mmoja kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka yaliyoruhusu ujenzi wa ongezeko la ghorofa sita katika jingo refu la ghorofa 12 lililopo kwenye mtaa wa Chimara na kusababisha lichungulie Ikulu ya Rais jijini humo.

Hata hivyo Kimweri (60) na Maliyaga (55) walinusurika kwenda jela baada ya kulipa faini ya
hukumu hiyo iliyosomwa na aliyekuwa Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, (kwa sasa ni Hakimu Mfawidhi wa mahakama ya Kilosa), Sundi Fimbo ambaye ndiye aliyesikiliza shauri hilo.

Awali, Hakimu Fimbo alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa hati ya mashitaka ya kesi ina jumla ya makosa matano na ilifunguliwa chini ya Kifungu cha 31cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, No 11 ya mwaka 2007.

Hakimu Fimbo ayataja makosa hayo kuwa ni:-

Moja: Kuruhusu ujenzi wa jengo hilo lenye ghorofa 12 bila kufanya upembuzi endelevu.

Pili, Tatu na Nne: Kutoa kibali cha kujengwa kwa jengo hilo wakati hawakuwa na mmlaka ya kutoa kibali hicho bali Mamlaka ya Mipango Miji ya Manispaa ya Ilala ndiyo ilikuwa na mamlaka ya kutoa kibali cha kufanyiwa marekebisho ya matumizi ya jengo hilo.

Tano: Matumuzi mabaya ya madaraka ambapo washitakiwa walitumia madaraka yao vibaya kwa kuruhusu mabadiliko sakafu katika ujenzi huo ambao mabadiliko hayo yaliruhusu kinyume cha sheria kuongeza idadi ya ujenzi zaidi wa ghorofa saba kwenda juu wakati jengo hilo lilistahili kujengwa ghorofa sita tu na hivyo kufanya jengo hilo sasa kuwa na jumla ya ghorofa 12.

Mshitakiwa wa kwanza aliakabiliwa na kosa la kwanza, pili na la tano wakati mshitakiwa wa pili alikabiliwa na kosa la tatu, nne na tano.

Hakimu Fimbo alisema kwanza anashangaa hadi sasa Manispaa ya Ilala ilishindwa kuchukua hatua kuhusu ujenzi wa jengo hilo lilojengwa kinyume na sheria ambalo lipo katika ukanda wa usalama “security zone”, wakati Sheria inaipa mamlaka Manispaa ya Ilala kuchukua hatu.

“Ajabu sana kwani Manispaa ya Wilaya ya Ilala ilikuwa na mamlaka ya kuchukua hatua za kisheria kuhusu ujenzi wa jengo hilo ambalo umekiuka sheria za nchi lakini ilishindwa kufanya hivyo… sasa nafikiri kupitia hukumu hii naona ni muda muafaka sasa kwa Manispaa hiyo kutekeleza yale hukumu hii ya mahakama kuhusu ujenzi wa jengo hilo ambalo haujakdthi matakwa ya sheria za nchi,”alisema Hakimu Fimbo.

Alisema anaukataa utetezi wa washitakiwa uliokuwa ukidai kuwa hawakuwa wakijua kumruhusu mwekezaji ambaye ni Kampuni ya Royal Orchard Inn kujenga maghora zaidi juu kwani kuna vielelezo vilivyotolewa na wakili wa TAKUKURU, Leonard Swai kuwa kuna barua ya Katibu Mkuu Kiongozi iliyokuwa ikienda kwa washitakiwa hao ikiwaambia waombe kwanza kibali kwa mamlaka ya Mipango Miji cha mabadiliko ya matumizi ya adhi katika Kitalu Na. 45 na 46 Mtaa wa Chimala, lakini kwa maslahi yao binafsi walipuuza agizo la barua hiyo na kuamua kujitwisha madaraka ambayo hawana wakaamua kuruhusu ongezeko la ujenzi wa ghorofa za saba zaidi juu.
“Kwa hiyo mahakama hii inakataa utetezi wao kuwa walikuwa hawana taarifa iliyowataka waombe kibali cha mabadiliko ya matumuzi ya ardhi hiyo ambayo ni eneo la Ukanda wa Usalama,…kama washitakiwa hao wasingevunja kifungu cha 32 cha Sheria ya Makazi No. 8 ya mwaka 2007 ni wazi mwekezaji ambaye ni kampuni ya Royal Orchard Inn Ltd asingeweza kunufaika katika mkataba wa jengo hilo ambalo ni baina ya serikali na kampuni hiyo”
“Ni sahihi kabisa kama washitakiwa hao wasingevunja sheria , hakuna njia mwekezaji huyo angeweza kupata uniti 19 ni kama amepangisha na anachukua kodi kila mwezi na kwamba kifungu cha 31 cha Sheria ya Takukuru ya mwaka 2007 kinaonyesha washitakiwa walinufaika binafsi na ujenzi huo wa ghorofa hilo kinyume na sheria na kwa maana hiyo mahakama upande wa jamhuri umeweza kuthibitisha kesi yake bila kuacha mashaka,” 
alisema Hakimu Fimbo.

Baada ya kuwatia hatiani na kabla ya kutoa adhabu aliwataka mawakili wa pande zote mbili kusema chochote kama wanacho. Wakili wa TAKUKURU, Leonard Swai alieleza kuwa hana rekodi za washitakiwa kuwa kama huko nyuma waliwai kutiwa hatiani kwa makosa ya jinai ila akaiomba mahakama itoe adhabu kwa wengine ambao wamekuwa wakijijengea majengo bila kufuata sheria na hasa ukizingatia urefu wa jengo unahatarisha usalama wa makazi ya Rais wa nchi (Ikulu).

Kwa upande wa wakili wa washitakiwa Henri Masaba, Pascal Kamala aliomba mahakama hiyo itoe adhabu nyepesi kwa sababu washitakiwa hao watendaji wa mara ya kwanza na ni wagonjwa.

Hakimu Fimbo akitoa adhabu alisema kila kosa moja ni jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh.milioni tano kwa kila kosa. Hivyo kila mshitakiwa atakwenda jumla ya miaka tisa kwa sababu kila mshitakiwa na akabiliwa na jumla ya makosa matatu au atalipa jumla ya Sh. milioni 15 .

Ndipo washitakiwa wote walifanikiwa kulipa faini ya fedha na kuaachiwa huru.

Akizungumza na waandishi wa habari za mahakamani nje ya mahakama baada ya hukumu hiyo kutolewa, wakili wa TAKUKURU, Swai alisema kwanza amefurahishwa na hukumu hiyo nzuri na ambayo ni salamu kwa wale wote wanaojenga majengo kiholelaholela na pia ni sifa kwa PCCB (TAKUKURU).

Alisema kesi hiyo iliendeshwa na PCCB kwa kifungu cha 40 (1) na (2) cha Sheria ya PCCB, ambacho kinaipa mamlaka PCCB ndani ya miezi sita kuanzia hukumu ilipotolewa na mahakama kuhusu kesi yoyote iliyoshitakiwa kwa sheria ya PCCB, kutaifisha mali husika. Katika mazingira ya kesi hii, PCCB, ndani ya muda huo, inayo mamlaka ya kutaifisha ghorofa ya 7-12 ya jengo.

Kesi hiyo ilianza Julai mwaka 2013 kwa washitakiwa kufikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na mashitaka hayo waliyotiwa hatiani nayo jana.

--- Shukurani kwa taarifa: Gazeti la Uhuru na blogu ya Happy Katabazi