Wanachuo Kleruu wagoma wakidai huduma ya maji na umeme


Habari kwa mujibu wa gazeti la MAJIRA zinasema kuwa Wanafunzi wa Chuo cha Ualimu cha Kleruu, kilichopo Gangilonga katika Manispaa ya Iringa, walifanya mgomo wa kutoingia darasani na kuandamana wakipinga kukatiwa umeme na maji kwa kipindi cha wiki tatu mfululizo. 

Maandamano hayo yalianzia chuoni hapo jana kwenda nyumbani kwa Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Christine Ishengoma ili aweze kuingilia kati tatizo hilo, lakini yalidhibitiwa na Jeshi la Polisi wakiwa wamekaribia katika Shule ya Msingi Um-Salam.

Baadhi ya wanafunzi chuoni hapo, walisema Shirika la Umeme nchini (TANESCO), mkoani humo liliamua kukata umeme kutokana na deni la sh.milioni 2.5. 

Walisema mbali ya chuo hicho kukosa umeme, pia hakina maji kwa wiki tatu; hivyo wanafunzi wanashindwa kusoma hasa kipindi cha usiku na kutumia muda mwingi kutafuta maji ambayo wanayapata katika umbali mrefu.
"Kama Serikali ya Mkoa itashindwa kuingilia kati ili kutatua kero hii ni bora chuo kifungwe hadi huduma hizi zitakaporudi tena" 
walisema wanafunzi hao.

Akizungumza na Majira, Rais wa Serikali ya Wanafunzi chuoni hapo, Manfred Joachim, alisema wametii amri ya polisi; lakini watayafanya tena leo baada ya kukamilisha taratibu zote pamoja na kupata kibali cha polisi.
"Tumeamua kutumia njia ya kuandamana ili kuongeza msukumo kwa uongozi wa chuo na Serikali watatue kero hii ili wanafunzi waweze kupata huduma ya umeme na maji kwani hivi sasa tunaishi katika mazingira magumu sana. Hatuwezi kujisomea usiku na mafunzo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT) ya mesimama, wanafunzi wamekata tamaa hawajui hatima yao wakati ada wamelipa" 
Alisema na kuongeza kuwa, wakati mwingine wanakaa zaidi ya siku tatu bila kuoga na wanapouuliza uongozi wachuo juu ya tatizo la maji, huambiwa hawana fedha za kulipia huduma hiyo.

Mlenga
Bw. Mlenga

Akizungumzia sakata hilo, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Bw. Anjelist Mlenga, alikiri kuwepo kwa matatizo hayo na kuongeza kuwa, hata uongozi wa chuo unawaonea huruma wanafunzi lakini wamekosea taratibu za kudai haki zao.
"Sijui kiasi cha fedha ambacho kinadaiwa na watoa huduma za umeme na maji, Mkuu wa chuo amekwenda wizarani kufuatilia fedha hizo kwani wao ndio wenye jukumu la kulipia huduma hizi" 
Aliwaomba wanafunzi chuoni hapo wawe watulivu wakati matatizo hayo yakishughulikiwa ambapo ombi la wanafunzi kutaka chuo hicho kifungwe hadi huduma hizo zitakaporejea ni jambo ambalo linazungumzika.