Albert Sanga: Tumefika pazuri, akili zitakujaHivi karibuni kulikuwa na habari iliyotikisa vyombo vya habari hasa kwenye mitandao ya kijamii iliyohusu usaili wa idara ya uhamiaji. Idara hiyo ilitangaza nafasi zisizozidi sabini lakini walioitwa kwenye usaili walikuwa waombaji zaidi ya elfu kumi (10,000). Usaili ule ulifanyika kwenye uwanja wa taifa kiasi kwamba ukitazama zile picha ungedhani lilikuwa ni rundo la watazamaji wa mpira wa miguu.

Tukio lile lilizua hisia tofauti miongoni mwa wengi, wengi wakimwaga lawama kwa serikali na kuonesha hofu yao kuhusu tunakoelekea na hili tatizo la ukosefu wa ajira. Binafsi nilipoliona tukio lile nililitazama kwa jicho jingine na nilifurahi, kuona tumefika mahala pazuri kama utakavyoona kwa kadiri ninavyoendelea kuchambua hapa.

Kwanza ifahamike kwamba tatizo la ukosefu wa ajira lipo dunia nzima. Hata zile nchi zinazotufadhili tatizo hili linawatafuna kule kwao. Mathalani ukosefu wa ajira nchini Marekani ni asilimia 6.1% na

Uingereza ni asilimia 6.8%, ilhali Tanzania ni asilimia 11.7%. Kwa hiyo tunapolitazama tatizo hili tuhakikishe tunalipatia sura ya kidunia kitu kitakachotusaidia kufikiria na kupata majibu halisi kwa mujibu wa hali inayoendelea ulimwenguni pote.

Katika nchi nyingi zilizoendelea na hata katika mataifa mbalimbali yanayoendelea Afrika ikiwemo Misri, Nigeria, Tunisia na nyingine; ukosefu wa ajira ndio ulioboresha ujasiriamali. Baada ya kuona ajira hakuna, baada ya kuona serikali imeelemewa, wananchi wengi katika mataifa hayo walianza kuumiza vichwa namna ya kujikwamua kama mtu mmoja mmoja. Ndipo ubunifu wa biashara, kuona fursa ndogo na kubwa kulipoendelea kuwa sehemu ya utamaduni na maisha ya kila siku kiuchumi.

Kinachowafanya vijana wengi katika nchi yetu Tanzania, kutoona namna ya kujiajiri ni kwamba bado shida hazijawapiga ipasavyo na kama zimewapiga ipasavyo basi bado hawajazinduka. Wengi wa vijana wetu wanapomaliza masomo yao bado hawajafikia hatua ya kukosa chakula, kukosa pa kulala na pengine kukosa mavazi.

Hata wakiwa hawana ajira wanakula, wanapo pa kulala na wanavaa vizuri. Wanamudu haya kwa sababu jamii na familia zetu nyingi bado tuna utamaduni wa kijamaa. Kijana anahitimu masomo yake leo lakini anaweza kuishi kwa mjomba, kaka, dada, mzazi, binamu, mtu wa kutoka eneo moja; hata kwa mwaka mzima akila, akilala na akivaa eidha kwa kisingizio cha kutafuta ajira ama kwa kigezo cha “kwa sababu hana ajira”.

Huu mtindo unachangia sana kudumaza akili za ubunifu kwa vijana wetu wasomi, hawaoni fursa kwa sababu hakuna kitu kinachowalazimisha kuziona. Shida, matatizo na changamoto ni kani (nguvu) zenye mchango mkubwa kumsukuma mtu kuziona fursa.Kwa kadiri shida, matatizo na changamoto zinavyozidi kuwa kubwa ndivyo ambavyo uwezekano wa mtu kuona fursa ndogo ndogo unavyozidi kuongezeka. Kama hujabanwa vizuri na matatizo ni rahisi kudharau fursa fulani fulani.

Hebu tujiulize hadi sasa ni vijana wangapi wanahitimu vyuo vikuu na kuthubutu kwenda kutafuta vibarua vya kukata majani ya mifugo kwa wafugaji? Ni wasomi wangapi baada ya kukosa ajira wamediriki kuanza biashara ya kutembeza maji mitaani, kwenye stendi na sehemu zenye watu?

Tunao vijana wangapi wahitimu wa shahada, stashahada na vyeti wenye nguvu na afya zao ambao baada ya kukosa ajira wameamua kukaa kwenye masoko mbalimbali kufanya tenda za kushusha mizigo? Niambie tuna vijana asilimia ngapi ambao wanauthubutu wa kuweka tai zao chini na kuamua kuwafuata wenye maduka ili wawe vibarua wa kusogeza mizigo stoo? Kilimo kinalipa, lakini ni vijana wangapi wenye shahada zao ambao wanaweza kuweka vyeti vyao kwenye makabati kisha wakapiga kambi vijijini huko mashambani kwa ajili ya kulima?

Kimsingi vijana hawawezi kuona kuwa kukata majani ni fursa hata kama wana digrii kwa sababu bado shida hazijawapiga vizuri. Hawawezi kuona kana kwamba kutembeza maji mtaani ni fursa kwa sababu wanapo pa kulala, wanapo pa kula, wanazo simu za gharama zinazowafariji kwa mitandao ya kijamii na bado wanavaa vizuri.

Nakuthibitishia kuwa kijana iwe ana shahada ya uzamili, shahada, stashahada ama cheti, ikitokea mambo yamemuwea magumu kabisa; hana pa kulala, hana pa kula hana mavazi ya kuvaa; hawezi kukataa kazi ya kufyeka majani, hawezi kudharau kazi ya kulima, hawezi kujivunga kwenda kushusha mizigo stendi wala hawezi kudharau fursa yeyote hata kama itamletea shilingi hamsini. Atathubutu, atatenda na atafanikiwa!

Ukienda kule Nigeria ni kawaida kukuta vijana wenye shahada za uzamili na shahada wakipiga rangi za viatu mitaani, wakiuza maji na wakizunguka na bidhaa kiumachinga. Hata kule Misri kilichoibua hasira za maandamano yaliyoung’oa utawala wa Rais Husein Mbarak ilikuwa ni baada ya askari wa jiji kumnyanyasa kijana msomi wa chuo kikuu ambae aliamua kujiajiri kwa kuanzisha banda la ‘umachinga’ baada ya kukosa ajira.

Vijana wasomi kuwa machinga, wapiga debe, wabeba mizigo, wakata majani na wakulima wadogo wadogo; mtu anaweza kusema ni ‘bomu’. Lakini ukweli ni kwamba hiyo ni nukta nzuri. Wasio na ajira (wawe wasomi ama wasiosoma) wanapopatwa changamoto kiuchumi kisha wakawa tayari kuzichangamkia fursa ndogo ndogo na zinazodharauliwa, hiyo ni hatua nzuri sana.

Mara nyingi nimekuwa nikisema na kurudia kuwa tatizo la Tanzania sio ukosefu wa ajira bali kuna umasikini mkubwa wa kifikra unaosababisha watu kutouona uwezo wao wa ndani na kushindwa kuona fursa zinazowazunguka. Hapa ndipo tunapotakiwa kuwekeza sio kumwaga misaada na mikopo ya fedha pekee.

Ongea na vijana(wasomi na wasiosoma), kina mama, na wengine kuhusu kujikwamua kiuchumi; kilio chao watakueleza ni ukosefu wa ajira na kuhusu kujiajiri watakutolea machozi kwamba wanakosa mitaji (fedha). Sasa jaribu kuwachukua vijana wasomi waulize huu ukosefu wa fedha ni kiasi gani kinahitajika katika biashara zipi?Wengi utaona wanakutajia biashara kubwa kubwa za mamilioni ya fedha.

Kitu ninachosema na kusisitiza ni kuwa tatizo la ukosefu wa ajira litaendelea kuwa kubwa mpaka pale wahusika watakapoweza kuwa na ufahamu wa “kiupambanaji” ambao unaiona shilingi elfu moja kama mtaji mkubwa. Bahati mbaya ni kuwa tuna kizazi cha wasomi (na watanzania wengi) ambao utafutaji wa maarifa sio kipaumbele kwao.

Lakini katika kitabu changu, kwenye chambuzi zangu na kwenye semina zangu nimekuwa nikieleza kwa mifano namna unavyoweza kuzalisha fedha pasipo fedha. Hivyo utabaini kuwa sababu nyingine ya vijana wetu wasomi na Watanzania kwa ujumla kulalamika kuwa wanashindwa kujiajiri kwa kukosa fedha (mtaji) ni kwa sababu hawana maarifa ya namna ya kuzalisha fedha pasipo fedha. Maandiko matakatifu yanaonya kuwa “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa”

Wasomi wetu wana maneno mengi ya kujitetea na kulalamika kwa sababu bado wanaishi kwa falsafa za kale katika zama mpya. Enzi hizo ilikuwa “soma upate kazi” lakini siku hizi ni “soma utengeneze kazi”. Kwa zamani nchi yetu ilikuwa chini kielimu, waliokuwa wakisoma walikuwa wachachena wote ilibidi kupata kazi kutokana na mahitaji.

Siku hizi mwamko wa elimu umekuwa mkubwa, shule na vyuo vinaongezeka kila siku, kwa hiyo ndoto za “soma upate kazi” inazidi kuyeyuka. Msomi yeyote ambaye anasoma kwa mtazamo wa “soma upate kazi” ni rahisi sana kuchanganyikiwa anapoingia mtaani na kukuta kazi hamna.

Kwa hiyo, tatizo hili la ajira linavyozidi kuongezeka, tunavyozidi kuwa na vijana wengi wasomi wasio na kazi mtaani, ndivyo maisha yatakavyozidi kuwa magumu zaidi na zaidi. Huu mtindo wa kijamaa wa kula, kulala na kuvaa kwa mjomba, kaka, binamu; unazidi kuisha kutokana na ugumu wa maisha.

Maisha yanapozidi kuwa magumu kwa waliokosa ajira, wajomba wanapoendelea kuchoka kulisha na kulaza wasio na ajira; itakuja nukta ambayo aliekosa ajira hatakuwa na namna isipokuwa kuziona fursa hata zile fursa ndogo ndogo zinazodharauliwa ziwezazo kumuokoa kiuchumi. Hapo ndipo ninaposema tumefika pazuri, kwa sababu akili zitakuja.

Hili wimbi la ukosefu wa ajira halina haja ya kulihofia kwa sababu hizi akili za watanzania wengi haziwezi kubadilika tusipopitia tunapopita sasa. Vijana wetu wamekuwa wavivu wa kubuni, hawana maono kuhusu kesho zao, wamekuwa mabingwa wa kuchagua kazi, wana ndoto za maisha makubwa ya kulala masikini na kuamka matajiri, hawana utamaduni imara wa kujifunza na kujisomea kuyajua maisha halisi kutwa kucha wanahangaika kuota maisha ya ‘mamtoni’, maisha ya kwenye filamu na maigizo. Akili kama hizi sio rahisi sana kubadilika mpaka shida ziwachakaze kisawasawa, hapo ndipo watazinduka.

Kwenye kitabu changu cha “Ni wakati wako wa Kung’aa” katika sura inayoeleza namna mtu unavyoweza kuzalisha fedha pasipo kutumia fedha, nimeeleza nguvu mbili ziitwazo “Push power” na “Pull Power” zinavyowasukuma watu kutafuta mafanikio. Nimeeleza kuwa unapokuwa katika matatizo makubwa halafu kukawa hakuna namna unayoweza kutulia ama kurudi nyuma, hapo unatakiwa kutumia “push power”.

Hii ni nguvu ambayo inaambatana na mtu pale anapobaini kuwa akitulia na kulia-lia matatizo yatammaliza; hivyo anaamua kupambana. Na anapokuwa akipambana huku akijua kuwa alikotoka ni kubaya na hakufai kurudi, basi hataacha kupambana zaidi na zaidi.Wakati utakuja ambapo mtu aliekosa ajira yeye mwenyewe atainuka kwenda kuchakarika pasipo kuililia serikali.

Kuna mazingira ambayo serikali imekwisha yaandaa yanayoweza kuwasaidia watu kujiajiri lakini hayajatumika kwa asilimia 100%. Kabla ya kuilalamikia na kuililia serikali hebu yatumike kwa asilimia 100%. Lakini hili tatizo la ukosefu wa ajira tupende ama tusipende litatuletea akili za kujitegemea na kupambana.

Inawezekana kila Mtanzania kuwa mshindi wa kiuchumi!

Makala hii imeandikwa na:
Albert Sanga, 
Iringa.
0719 127 901