[audio] "Haturudi kwenye Bunge Maalum la Katiba" - UKAWA

Viongozi wakuu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wakishikana mikono mara baada ya kuongea na waandishi wa habari kutoa tamko la UKAWA kuhusu wito wa Viongozi wa Dini wa kurudi Bungeni.

Kutoka kulia ni Profesa Safari Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi Mosena Nyambabe, Mwenyekiti wan CHADEMA Freeman Mbow, Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia, Katibu Mkuu wa CHADEMA Wilbrod Slaa, Mbunge Sakaya na Julius Mtatiro wakiwa nje ya Makao Makuu ya CUF

Ripoti ya Dina Chahali, via VOA - Umoja wa katiba ya wananchi- UKAWA na Mwenyekiti wa Bunge maalum la katiba Tanzania bado wanavutana juu ya uendeshaji wa bunge hilo maalum la katiba jambo linalozusha shaka juu ya mustakbali wa upatikanaji wa katiba mpya nchini Tanzania.

Wajumbe wanaounda UKAWA chini ya uenyekiti wa mwenyekiti wa taifa wa chama cha CUF Profesa Ibrahim Lipumba wameendelea na msimamo wake wa kutokurejea katika bunge maalum la katiba linalotarajiwa kuanza tena vikao vyake Agosti tano mwaka huu, kwa siku 60 zilizoongezwa na Rais Kikwete ambapo ilitarajiwa wakikamilisha awamu hiyo itarudishwa kwa wananchi kwa ajili ya
kura za maoni.
Imeelezwa kwamba ili Katiba inayopendekezwa iweze kupata uhalali wa kupitishwa kwake, sheria inaweka sharti kwamba ni lazima ikubalike na pande zote za muungano kwa zaidi ya theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote kwa kila upande.

Wakitoa tamko juu ya msimamo wao jijini Dar es Salaam, Alhamis viongozi wa UKAWA akiwemo mwenyekiti wa chama cha CUF, Profesa. Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa chama cha CHADEMA Freeman Mbowe na mwenyekiti wa chama cha NCCR MAGEUZI James Mbatia, wamesema wako tayari kurudi bungeni pindi rasimu hiyo ya katiba iliyowasilishwa bungeni na tume ya mabadiliko ya katiba ambayo ni maoni ya wananchi, itakapojadiliwa na si vinginevyo.

UKAWA waliondoka bungeni April 16 baada ya kususia bunge maalum la katiba kwa madai kwamba bunge hilo halijadili rasimu yenye maoni ya wananchi ambayo iliwasilishwa bungeni hapo na Jaji Joseph Warioba pamoja na kulaumu kwamba bunge hilo linaendeshwa kibabe kwa kufuata matakwa ya chama tawala cha CCM kinachosisitiza kuwepo na serikali mbili ya muungano badala ya iliyopendekezwa katika rasimu ya pili ya muungano wa serikali tatu.

Hadi kikao cha kwanza cha bunge maalum la katiba huko mjini Dodoma kilipoahirishwa April 25 mwaka huu kupisha bunge la bajeti, wajumbe wa UKAWA walikuwa wamesusia vikao na kuanza kuzunguka maeneo mbalimbali nchini kuwaeleza wananchi kwamba walichosusia ni mwenendo mbovu wa bunge hilo.