Bunge Maalum la Katiba litaendelea ilivyopangwa - Sitta

* Akidi itatimia bila UKAWA

Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya Khamis akizungumza na waandishi wa habari leo (hawapo pichani ) kuhusu kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ndogo za Bunge jijini Dares Salaam. (picha: Magreth Kinabo/MAELEZO)

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Samuel Sitta, amesema kuwa Mkutano wa Bunge hilo, utaendelea kama ulivyopangwa Agosti 5, mwaka huu mjini Dodoma.

Amesema kuwa licha ya baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo, kuendelea na msimamo wao wa kutaka kususia vikao vitakavyoanza mapema mwezi ujao, lakini bado kuna mambo muhimu ya kujadiliwa.

Mwenyekiti huyo ametoa kauli hiyo leo mjini Dar es Salaam, katika taarifa yake iliyosomwa kwa niaba
yake na Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya Khamis wakati wa mkutano wa waandishi wa habari.
“Kamati hiyo, imeamua kupendekeza kwa Kamati ya Uongozi kwamba Bunge Maalum la Katiba liendelee kwa sababu yapo masuala mengi muhimu ya kikatiba ambayo yanatuunganisha kama vile usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi na kuikarabati Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
“Mambo mengine ni kurekebisha kikatiba masuala ya Muungano, haki za wakulima, wafugaji, wasanii na makundi mengineyo na ukomo wa vipindi vya uongozi,”
alisema Sitta katika taarifa hiyo.

Aidha aliongeza kwamba uamuazi huo, umefikiwa baada ya wajumbe wa Kamati hiyo waliohuduria ambao walikuwa zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe wote, ambapo waliendelea na kikao.

Alisema hatua ya baadhi ya wajumbe kwenda kwa wananchi na maoni yao imekuwa siyo muafaka na si wakati wake, hivyo Bunge hilo liwajibike katika siku za usoni kujibu upotoshwaji wowote kuhusu mchakato wa katiba kadri unavyojitokeza.

Aliongeza kwamba Kamati hiyo, inaona kwamba kwa kuendelea kulisusia Bunge hilo, na kupuuza wito wa jamii kupitia makundi mbalimbali pamoja na madhehebu ya dini inatilia shaka dhamira halisi ya viongozi wa kundi hili la wasusiaji kupuuzia juhudi zote za usuluhishi, kunazua mashaka kuhusu lengo la ususiaji kwamba pengine agenda ya viongozi hawa ni nyingine na siyo upatikanaji wa Katiba.

Alisema Kamati hiyo inarejea kwamba wajumbe hao 629 wamekabidhiwa jukumu adhimu na la kihistoria kwa niaba ya Watanzania jukumu ambalo hutokea baada ya miongo kadhaa ya uhai wa Taifa lolote.
“Tutakuwa hatuwatendei haki Watanzania ikiwa hatutafikia maridhiano yanayotuwezesha kukamilisha kazi tuliyopewa,” 
alisisitiza.

Mwenyekiti huyo alisema katika ngwe ya pili inayoanza mapema mwezi ujao mkutano wa Bunge hilo, uzingatie upya baadhi ya Kanuni za Bunge hilo, ambazo ni kikwazo katika kuhakikisha kwamba kazi ya kujadili na hatimaye inayopendekezwa inakamilika ndani ya siku 63 zilizosalia kisheria, kati ya hizo siku 60 ni za nyongeza na tatu zilizokuwa pungufu za siku 70 za awali.

Alisema Kamati hiyo, inaendelea kutoa wito wa wajumbe waliosusia mikutano ya Bunge hilo, kurejea katika Bunge hilo, ambalo pekee ndiyo lina uwezo wa kisheria wa kutatua matatizo yaliyopo.

Amesema kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 54 kifungu cha nne na tano ya Kanuni za Bunge Maalum la Katiba, aliteua Kamati ya Mashauriano ya wajumbe thelathini (30) kujadili matatizo yaliyojitokeza Dodoma katika mkutano ulipita lakini wajumbe kutoka Chama cha CUF, CHADEMA na NCCR Mageuzi,walikisusa kikao cha jana Julai 24 mwaka huu.
“Jitihada mbalimbali zilizofanywa na sekretarieti pamoja na mwenyekiti hadi asubuhi ya siku ya mkutano hazikuweza kuwashawishi wajumbe hao wasusiaji kuhudhuria kikao, alisema Sitta katika taarifa yake.
Aliitaja athari za kutoendelea na mchakato uliopangwa wa kuandaa na hatimaye kuipigia kura Katiba mpya ni pamoja na kupoteza mabilioni ya fedha za wananchi zilizokwisha tumika katika kazi, baya zaidi ni kuiweka rehani amani ya nchi yetu kwa kuukuza mno mgogoro wa katiba na kuwagawa wananchi kwa propaganda hadi uchaguzi mkuu 2015. --- Taarifa ya Winner Abraham na Rose Masaka

---------------------------

Akidi itatimia bila UKAWA

WAKATI wajumbe wa Bunge la Katiba wanaounda Kamati ya Mashauriano wakifanya kikao chao jijini Dar es Salaam jana, imeelezwa kuwa vikao vya bunge hilo vilivyopangwa kuanza mapema mwezi ujao mjini Dodoma, vitafanyika kama kawaida.

Kikao cha jana kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini hapa, kilifanyika bila kuwapo kwa wajumbe kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Tangu awali, Ukawa walikwishasema kwamba hawatashiriki katika kikao hicho pamoja na kupokea wito kutoka kwa Sitta.

Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya kikao cha jana zilisema kwamba, Kamati hiyo ilimhsauri Sitta kuendelea na vikao vya Bunge hilo vinavyotarajia kukaa kwa siku 60 kukamilisha mapitio ya Rasimu ya Katiba.

“Akidi itatimia bila hata Ukawa kurejea bungeni, labda tatizo kidogo litakuwa kwa upande wa Zanzibar.

“Lakini zipo taarifa kuwa miongoni mwa waliotoka bungeni Aprili mwaka huu, wapo ambao kwa sasa hawana imani sana na Ukawa, na hawa watarejea bungeni, hivyo huenda hata upande wa Zanzibar nako akidi ikatimia,” alisema mjumbe mmoja wa Kamati ya Mashauriano kutoka Zanzibar.

Jana, Sitta alizungumza na waandishi wa habari akisema vikao vya Bunge hilo vitaanza kama kawaida asubuhi ya Jumanne, Agosti 5 mwaka huu hata kama Ukawa hawatakuwapo bungeni.

“Hii ni kutokana na ushauri tuliopewa na Kamati ya Mashauriano ya Bunge iliyokutana leo. Lakini kama Ukawa watataka kuja, wanakaribishwa,” alisema Sitta.

Ukawa wamekuwa katika msimamo wa kutokwenda Dodoma kwa namna yoyote hadi pale Bunge la Katiba litakaporejea kwenye mjadala wa Rasimu iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

Kumekuwa na jitihadi nyingi za kuwataka warejee ambazo zimegonga ukuta, na hata sasa bado Watanzania wanasubiri taarifa kutoka katika kikao kingine kilichomalizika juzi kati ya Ukawa, CCM na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi. --- Taarifa kwa mujibu wa gazeti la MTANZANIA